Mamia ya waombolezaji wafurika kwenye mazishi ya mfanyabiashara aliyejiua Moshi

Moshi. Mamia ya waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro wamefurika kwenye mazishi ya mfanyabiashara maarufu mjini Moshi na Dodoma, Ronald Malisa (35) aliyejiua kwa kujinyonga nyumbani kwake.

Malisa anatarajiwa kuzikwa leo jioni, Julai 15, 2025  nyumbani kwake eneo la Msufuni, Msaranga ambapo tayari shughuli ya kuaga mwili inaendelea nyumbani hapo.

Julai 10, mwaka huu Malisa, aliripotiwa kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia shuka kwenye choo cha nyumba yake eneo la Msufuni, Msaranga huku Jeshi la Polisi likidai chanzo ni msongo wa mawazo uliotokana na tatizo la afya ya akili.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 11, 2025 na Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa mfanyabiashara huyo inadaiwa siyo tukio la kwanza kutaka kujiua na kwamba kwa mara kadhaa alifanya jaribio la kujiua kwa kunywa sumu lakini aliokolewa na familia.

“Mnamo saa 12:30 asubuhi Julai 10, 2025 huko Msaranga, mfanyabiashara mkazi wa Dodoma na Msaranga aligundulika kufariki kwa kujinyonga kwenye dirisha la choo kilichopo chumbani kwake kwa kutumia shuka,” alisema Kamanda Maigwa.


Katika mazishi hayo, ulinzi umeimarishwa kufuatia umati wa watu uliopo kwenye eneo ambalo ibada ya mazishi ya mfanyabiashara huyo inaendelea.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi.

Related Posts