Dar es Salaam. Walimu wastaafu na waliopo kazini wamebainika kuwa waathirika wakuu wa mikopo umiza inayotolewa na taasisi za kifedha zisizosajiliwa, zenye riba kubwa isiyoeleweka, huku wengi wao wakikopeshwa bila hata kuwa na mkataba halali.
Baadhi ya walimu hao wamejikuta wakikatwa fedha katika mishahara yao kwa miaka mingi bila hata kufahamu deni lililobaki, huku wengine wakikosa kabisa mafao yao yote baada ya kustaafu, kutokana na mikataba ya mikopo ambayo ama hawakuwahi kuiona au kuielewa.
Mwananchi limefanikiwa kuona ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), na kubaini namna walimu wanavyolizwa na mikopo hiyo, huku uzoefu ukionyesha kuwa walimu ndio kada inayoongoza kwa kukopa.
Ripoti hiyo inahusu uchambuzi wa malalamiko yaliyopokelewa na Takukuru kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2021 dhidi ya kampuni na watu binafsi wanaotoa huduma ya ukopeshaji nchini.
Katika ripoti hiyo, kuna matukio ya walimu waliokopeshwa kwa masharti ya ajabu. Kwa mfano, mwalimu mmoja ambaye ni mstaafu, alikopa Sh150,000 lakini akadaiwa Sh62.175 milioni, bila kuelezwa kipindi cha kulipa wala kupewa mkataba wowote.
Mwingine alikopa Sh1 milioni akatakiwa kurejesha Sh24 milioni, fedha ambazo alitakiwa kulipa kupitia mafao yake ya kustaafu.
Ripoti inaonyesha pia mwalimu mstaafau aliyekopa Sh 100,000 na kutakiwa kurejesha 8,469,500. Yupo mwalimu mwingine aliyekopa Sh 2, 000,000 na kutakiwa kulipa Sh 40,835,000.

Ripoti hiyo inachambua malalamiko 195 yaliyowasilishwa kati ya Juni 2019 hadi 2021, na kubaini kuwa walimu ni kundi lililoathirika zaidi, wakiongoza kwa asilimia 66 ya malalamiko yote, likiwa ni pamoja na wastaafu asilimia 43, asilimia 23 walimu waliopo kazini, wafanyabiashara asilimia 12, huku askari wakiwa asilimia nane.
‘’Pamoja na kwamba idadi kubwa ya waliolalamika ni walimu lakini walimu wastaafu ni idadi kubwa ukilinganisha na makundi mengine. Hii inaweza kufasiriwa kuwa walimu wanaostaafu wengi huomba mikopo ili kukidhi haja zao wakati wakisubiri malipo ya mafao yao,’’ inasema sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza;
‘’Uchambuzi umebaini kuwa ni malalamiko sita pekee sawa na asilimia tatu ya malalamiko yote, ndiyo yaliyokiri kuwa wakopeshaji walitumia asilimia ya riba waliyoiandika katika mkataba mkuu katika huduma yao ya ukopeshaji.’’
Ripoti hiyo ya Takukuru inahitimisha kwa kusema: ‘’Uwepo wa wakopeshaji ambao hawafuati matakwa ya sheria, kanuni na taratibu sio tu hulikosesha taifa mapato lakini pia ni huwafilisi wananchi kwa kuwadai riba kubwa isiyoendana na mikopo halisi waliopatiwa kama ilivyoainishwa kwenye matokeo. Hivyo, mamlaka husika yapaswa kuchukua hatua stahiki kwa wakopeshaji wa aina hii ili kunusuru wananchi hawa wenye uhitaji wa mikopo.’’
Mmoja ya mwalimu anayefundisha katika Shule ya Sekondari mkoani Mbeya Zuberi Nguza, anasema ni kweli kuwa walimu wengi hujikuta katika matatizo ya mikopo umiza, kutokana na baadhi ya taasisi za kifedha kuweka masharti magumu, huku wakiamini kuwa walimu ni kundi linalokabiliwa na matatizo ya kifedha kwa kuwa mishahara yao haitoshi.
“Baadhi ya taasisi zinazokopesha huwataka walimu kuacha kadi zao za benki ili wakate fedha moja kwa moja kila mwisho wa mwezi. Matokeo yake, mwalimu hulazimika kuchukua mshahara wake kutoka kwa aliyemkopesha. Hali hiyo imewafanya walimu kulipia deni kubwa zaidi kuliko walichokopa,” anasema Nguza.
Nguza anaongeza kuwa mshahara mdogo ndio chanzo kikuu cha walimu kuingia kwenye mikopo ya aina hiyo, na kuhoji kwa nini makundi mengine ya watumishi hayajakumbwa na hali kama hiyo.
Pia anatoa wito kwa Serikali kuongeza mishahara ya walimu, akisisitiza kuwa wao ni kundi muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Miongoni mwa walimu waliokwama katika mtego wa mikopo umiza ni Amina Luhanga, mwalimu wa Shule ya Msingi Mtoni Kijichi, anayesema hulazimika kukopa kutokana na hali ngumu ya maisha, ingawa mwisho wake huwa ni mateso makubwa kuliko msaada waliotarajia.
“Mara nyingi hatuchukui mikopo kwa tamaa, bali kwa sababu ya hali ya maisha. Mshahara hautoshi. Kuna ada za watoto, matibabu, kodi. Ukiona mtu anakopa kwa masharti ya ajabu ujue tayari yupo kwenye shida kubwa. Unajiingiza kwa matumaini, unajikuta kwenye mtego,” anasema Amina.
Kwa upande wake, mwalimu Prisca Thomas, kutoka Mkoa wa Lindi, anasema moja ya sababu zinazowafanya walimu wengi kuingia kwenye mikopo umiza, ni tamaa ya kupata fedha haraka, hasa kutokana na baadhi ya taasisi za kifedha zisizo rasmi kutotoa masharti mengi kama benki zilizo rasmi.
“Walimu wengi huona mshahara unachelewa, kisha wakiona taasisi fulani inatoa hela bila masharti mengi, wanakimbilia huko. Tatizo ni kwamba wengi hawasomi mkataba. Baadaye wanakuja kushangaa kuwa wamedaiwa fedha nyingi tofauti na makubaliano ya awali,” anasema.
Prisca anawahimiza walimu wenzake kuwa makini kabla ya kusaini mikataba ya mikopo, akisema hali duni ya maisha isiwe sababu ya kuzembea kusoma masharti, jambo linalowaponza kwa kulipia fedha nyingi zisizoeleweka.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Benjamini Nkonya, anasema walimu wengi hujikuta katika hali hiyo, kutokana na uamuzi wa kuiga maisha ya watu wengine wenye kipato kikubwa zaidi huku vipato vyaio vikiwa vidogo.
” Ndio maana walimu wanakimbilia kwenye mikopo ya kausha damu, lakini dawa ya kukomesha hili ni kuwaongezea mishahara walimu,” anasema.
Asemavyo mtaalamu wa uchumi
Mtalaamu na mchambuzi wa masula ya uchumi, Joel Rweyemamu, anasema walimu ndio walengwa wakuu wa taasisi za mikopo kwa sababu ya uhakika wa mapato yao.
“Walimu hulengwa kwa sababu mishahara yao iko kwenye mfumo wa Serikali. Taasisi nyingi zisizo rasmi zinajua watakata moja kwa moja. Hata wastaafu, mafao yao ndiyo kivutio. Serikali inatakiwa kuingilia kati,” anasema.
Aidha, baadhi ya wachambuzi wanasema ipo haja ya kuanzishwa kwa sera maalum ya huduma za kifedha kwa walimu, itakayozingatia ulinzi wa kisheria na ukaguzi wa mikataba.
Serikali yaonya wakopeshaji, wakopaji
Serikali inazitaka taasisi za fedha nchini kutoa elimu kwa wakopaji ili wawe na uelewa mpana kuhusu masharti ya mikopo, viwango vya riba, gharama za ziada, na athari za kutorejesha mkopo kwa wakati kabla ya kusaini mikataba husika.
Hayo yalisema na Machi 28 mwaka huu na Ofisa sheria mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ramadhani Myonga, alipozungumza wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na taasisi zake kwa wananchi wa Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
Alifafanua kuwa taasisi za fedha zinapaswa kutoa taarifa sahihi na mafunzo kwa wateja wao kabla ya kusaini mikataba ya mikopo, ili kuhakikisha wanachukua uamuzi wa kukopa wakiwa na taarifa sahihi.
“Serikali inaendelea kuweka sera na miongozo inayolinda wakopaji dhidi ya unyonyaji wa kifedha na kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa maendeleo ya kiuchumi”, alisema Myonga.
Aliongeza kuwa kukiwa na uwazi katika utoaji mikopo na elimu ikatolewa vizuri kwa wakopaji, kutapunguza unyonyaji wa kifedha na kutawasaidia wananchi kufanya uamuzi sahihi kwenye mikopo wanayoomba.