Mfanyabiashara aliyejiua Moshi azikwa, Kanisa Katoliki likieleza sababu za kumzika

Moshi. Wakati mamia ya waombolezaji wakishiriki maziko ya mfanyabiashara aliyejiua kwa kujinyonga mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Malisa (35), Kanisa Katoliki limeeleza sababu za kumzika licha ya taratibu za kanisa hilo kuwa na msimamo mkali wa kutozika waliojiua.

Padre Festo Urassa wa Parokia ya Mbokomu, Jimbo Katoliki la Moshi, mkoani Kilimanjaro amesema wamemzika mfanyabiashara huyo baada ya kubaini alikuwa na tatizo la afya ya akili.

Akitoa ufafanuzi wa kwa nini kanisa hilo limemzika Malisa mbele ya waombolezaji wakati wa ibada ya maziko, Padre huyo amesema wamefuatilia historia ya marehemu na kujiridhisha kipindi cha nyuma, alikuwa na anasumbuliwa na tatizo la afya ya akili.

Malisa ambaye amezikwa leo Jumanne, Julai 15, 2025 anadaiwa kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia shuka kwenye choo cha nyumba yake, eneo la Msufuni Kata ya Msaranga, Wilaya ya Moshi Julai 10, huku Jeshi la Polisi likidai chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo uliotokana na afya ya akili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 11, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa mfanyabiashara huyo inadaiwa sio tukio la kwanza kutaka kujiua na kwamba kwa mara kadhaa alifanya jaribio la kujiua kwa kunywa sumu lakini aliokolewa na familia.




“Mnamo saa 12:30 asubuhi Julai 10, 2025 huko Msaranga, mfanyabiashara mkazi wa Dodoma na Msaranga aligundulika kufariki kwa kujinyonga kwenye dirisha la choo kilichopo chumbani kwake kwa kutumia shuka,” alisema Kamanda Maigwa.

Akihubiri katika ibada hiyo ya mazishi ambayo imefanyika nyumbani alikozikwa mfanyabiashara huyo maarufu katika Jiji la Dodoma na Mjini Moshi, Padre Urassa amewataka waombolezaji kutouliza maswali mengi na badala yake waiombee familia hiyo.

“Msiulize maswali mengi kwanini imekuwa hivi na vile, nimeuliza nimepata uhakika kabisa kwamba hiki ninachokifanya ni sahihi kabisa, niendelee kuiombea familia na ninyi wote mliojumuika hapa, tuendelee kuwa na ushirikiano mzuri kabisa na familia hii,” amesema Padre Urassa.

Amesema alipopata taarifa za tukio hilo, alifuatilia na alibaini ni Ronald ambaye alimfungisha ndoa na Nancy Minja, Novemba 30, 2024 huku akisema kipindi wapo mafundisho ya ndoa walikuwa ni watu wanaheshimu mafundisho na walihudhuria vipindi vyote.

“Ronald nilikuwa simkumbuki kabisa tena, nilivyosikia hilo jina, nikasema sio huyu aliyefunga ndoa hapa mwaka jana kweli, lakini nilivyokuja kumwona hapa nikajua kuwa ni yeye, kwa kweli walikuwa wanaheshimu mafundisho vizuri na alihudhuria vipindi vyote kama kawaida, kwa kweli tunamwombea labda alikuwa na taarifa njia zake hapa mwishoni huwezi jua,” amasema Padre Urassa.

“Lakini sisi ni kumwombea tu, tunaombeana, ufanye kosa, uwe mtakatifu, usiwe mtakatifu, tunaombeana kwa sababu sisi hatuwezi kujua chochote, tunaweza kusema mambo yako hivi na hivi lakini Mungu yeye ana namna yake kwa hiyo sisi ni kuombena tuu bila kusema kitu chochote.”

Akitoa salamu za pole, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema siku tukio hilo linatokea ilikuwa ni siku ngumu kwake kwa kuwa alikuwa akimfahamu Ronald kwa muda mrefu hata kabla hajateuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Moshi.

“Nawapa pole sana familia, tangu nimefika hapa Moshi yapo matukio kadhaa yametokea na mwezi huu wa Julai kwa kweli nimetikiswa kweli kweli, kumekuwa na matukio mengi lakini siku ya tarehe 10, ilikuwa ni siku ngumu kidogo, kwa sababu nilipokea taarifa za mtu ninayemfahamu, Ronald,” amesema DC Mnzava.

“Ile tarehe 30.11.2024 Ronald anafunga ndoa na Nancy hata bado sijapangiwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Moshi nilikuja kwenye harusi, kwa hiyo ni mtu ambaye ninamfahamu, matukio ambayo yaliripotiwa siku hiyo nikasema basi kwasababu Mungu ameruhusu hali hiyo basi Mungu amemuita kwake mbinguni.”

DC Mnzava amesema Malisa alikuwa mcheshi, mchangamfu, mwenye kupenda watu na akiishi vizuri na wenzake akisema umati wa watu waliokuwepo ni ishara tosha kwamba alikuwa ni mtu wa watu.

Akisoma historia ya marehemu, ndugu wa mfanyabiashara huyo, Shedrack Malisa amesema ndugu yake alifunga ndoa na Nancy Minja, Novemba 30, mwaka 2024 katika Kigango cha Kutukuka kwa Msalaba, Msaranga na kwamba ndugu yao alipatwa na umauti Julai 10, mwaka huu nyumbani kwake.

“Malisa alipatwa na umauti Julai 10, mwaka huu akiwa nyumbani kwake Msaranga, ameacha mjane na watoto wanne, wa kiume wawili na wa kike wawili,” amesema ndugu huyo.

Baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mfanyabiashara maarufu katika Jiji la Dodoma na Mjini Moshi, Ronald Malisa aliyejiua kwa kujinyonga nyumbani kwake eneo la Msufuni, Msaranga, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.



Amesema wamepoteza mtu ambaye alikuwa na moyo wa upendo aliyejali watu bila ubaguzi katika jamii.

“Tunashukuru kwa maisha ya Ronald, alikuwa ni mtu ambaye Mungu aliweka moyo wa upendo kwake wa kujali watu, hakuchagua mkubwa wala mdogo, alikuwa mpambanaji, mcheshi, aliyetoa msaada mbalimbali kushirikiana na jamii katika mambo mbalimbali popote pale alipokuwepo,” amesema ndugu huyo.

Related Posts