Msako waanzishwa kubaini wakuu, wamiliki wa shule wanaohatarisha afya za wanafunzi

Bukoba. Serikali mkoani Kagera imeanza operesheni maalumu ya kukagua na kuchunguza shule za msingi na sekondari za Serikali na binafsi ili kubaini walimu wakuu na wamiliki wa shule wanaokiuka kanuni za afya na usalama wa wanafunzi.

Operesheni hiyo inalenga kubaini shule zenye dosari katika miundombinu ya maji safi na salama, chakula, usafi wa mabweni, na vyumba vya dharura vya watoto wa kike, pamoja na mazingira mengine yanayohatarisha afya za wanafunzi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne, Julai 15, 2025, Ofisa Afya wa Mkoa wa Kagera, Yasin Mwinori amesema uchunguzi huo umeanza rasmi Julai 14 na utaendelea kwa shule zote zilizoko ndani ya mkoa huo.

“Tumeanza operesheni maalumu ya kukagua shule zote ili kubaini waliokiuka miongozo ya afya. Mwalimu mkuu au mmiliki yeyote atakayebainika hatutasita kuchukua hatua stahiki,”amesema Mwinori.

Ameongeza kuwa kipaumbele kimewekwa kwa shule zenye mabweni ili kufuatilia idadi ya wanafunzi, hali ya usafi, chakula kinachotolewa, na upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu idadi ya shule ambazo tayari zimebainika na makosa hayo, Mwinori hakutaja majina wala idadi kamili, akisema uchunguzi bado unaendelea.

“Lengo ni kuhakikisha mazingira ya shule yanakuwa salama kwa watoto, hasa wakati huu wa mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kuchochea milipuko ya magonjwa,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kuna jumla ya shule za msingi 1,030 ambapo shule 938 ni za Serikali na 92 ni za binafsi.

Kwa upande wa shule za sekondari, zipo 288 kati ya hizo 220 ni za serikali na 68 ni binafsi.

Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Green Acres Bunazi iliyopo wilayani Misenyi, Jonson Kagya amesema shule yao inazingatia kwa kiwango kikubwa huduma za afya kwa wanafunzi.

Amesema wanapata maji safi yaliyotibiwa kutoka kwenye mifumo miwili ya bomba shuleni, pia tunapata milo mitano kwa siku.

Asubuhi saa mbili kila siku wanapata chai ya maziwa na kifungua kinywa, saa sita mchana mlo wa pili, saa tisa mlo wa tatu, saa 12 mlo wanne na mlo wa mwisho usiku baada ya masomo wanapata chakula pia.

Ofisa Mahusiano na Msemaji wa shule hiyo, Respicius John amesema mkakati wa Serikali ni muhimu na unapaswa kuungwa mkono na shule zote ili kuboresha afya za wanafunzi.

“Tunaiomba Serikali iziruhusu shule nyingine kuja kujifunza kwetu namna tunavyowahudumia wanafunzi kiafya kuanzia kwenye uandaaji wa chakula, matibabu ya maji, hadi mazingira ya mabweni,”amesema.

Related Posts