Kilwa. Mvuvi Mussa Kibarabara (25), mkazi wa Wilaya ya Kilwa, amefariki dunia wakati akivua dagaa katika Bahari ya Hindi, huku mwingine akiripotiwa kupotea.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Julai 15, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi John Imori amesema kuwa Kibarabara alikwenda kuvua dagaa Jumatatu ya Julai 13, 2025 majira ya usiku katika pwani ya Songosongo Kilwa Kivinje.
Imori ameendelea kusema kuwa Kibarabara alikuwa anavua dagaa kwa kutumia boti yake ya Salsabili, lakini alipoteza maisha hukohuko baharini na mwili wake ulipatika Julai 14 saa saba usiku.
“Hawa wavuvi wa dagaa mara nyingi wanakwenda baharini usiku, sasa wakati akiwa kwenye majukumu yake, umauti umemkuta hukohuko hadi jana saa saba usiku mwili wake ulipopatikana,” amesema Kamanda Imori.
Mwili wa Kibarabara ulichukuliwa jana asubuhi na kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Kilwa Kivinje kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Hata hivyo, Mwanachi Digital lilimtafuta mshauri wa Beach Managment unit (BMU) Kilwa Masoko, Ally Kambili ambaye amesema kuwa Kibarabara alikuwa mvuvi wa dagaa katika Pwani ya Songosongo iliyopo Kilwa kivinje.
Amesema mvuvi huyo alikwenda kuvua dagaa Julai 13, 2025 akiwa na boti yake ya uvuvi, lakini hakuweza kurudi tena hadi jana ulipokutwa mwili wake akiwa amekufa.
“Kibarabara ni mvuvi wa hapa Songosongo, ni kijana mdogo sana, kiukweli kifo chake kimetuumiza sana sisi wavuvi wenzie, lakini tumshukuru Mungu kwa yote na tunakwenda kumsitiri mwenzetu leo kijijini kwao Lymaliyao saa nne asubuhi,” amesema Kambili.
Wakati huohuo Kamanda Imori amesema kuwa pwani hiyo ya Songosongo amepotea mvuvi tangu Julai 7, 2025 aliyejulikana kwa jina la Abdul Kawinga (23) Mkazi wa Mtwara alipokwenda kuvua dagaa katika mwamba wa Kimbolwa Mwakatoni uliopo Nyuni maeneo ya Songosongo.
Imori amesema kuwa wenziwe waligundua kuwa mwenzao mmoja hayupo baada ya kuona dingi moja haijawashwa taa.
“Kawinga amepotea akiwa katika dago la nyuni akifanya shughuli za uvuvi wa dagaa jitihada za kumtafuta zilianza mara moja, lakini hadi sasa hajapatikana,” amesema kamanda.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limewataka wavuvi wote, hususan wale walioko katika maeneo ya pwani, kuwa makini na kufuatilia kwa karibu taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).
Wito huo umetolewa ili kusaidia kupunguza matukio ya vifo na upotevu wa wavuvi wanapokuwa baharini, kufuatia ongezeko la matukio ya aina hiyo mkoani Lindi ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.