KOCHA wa Pazi, Karimu Bakari Mbuke amesema mechi zilizosalia dhidi ya Real Dream, UDSM Queens, Twalipo Queens, DB Lioness, Kigamboni Queens na Vijana Queens zipo ndani ya uwezo wao kuhakikisha wanashinda na kutinga hatua ya robo fainali.
Mbuke licha ya kukiri Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) msimu huu ni ngumu hasa kwa timu za wanawake wanaojituma kwa bidii ili kupata bonasi kila wanaposhinda mechi, lakini wanajipanga kufikia malengo yao.
“Mfano misimu ya nyuma tulikuwa tunafungwa kwa vikapu vingi dhidi ya JKT Stars Queens ambayo imecheza fainali mara nyingi, ila mechi iliyopita imetuzidi kikapu kimoja, haikuwa mechi rahisi hadi inaisha, unaona wachezaji wangu wanavyoumia kuzikosa pesa,” alisema Mbuke na kuongeza;
“Wanaposhindania pesa ndivyo wanavyofanya timu ifanikiwe, maana wanajituma unaweza ukaona kuna mabadiliko makubwa,” alisema Mbuke na kuongeza;
“Tumecheza jumla ya mechi tisa, tumeshinda nne dhidi ya Ukonga Queens, City Queens, Mgulani JKT Queens na Kurasini Divas, tumepoteza dhidi ya DB Troncati, JKT Queens, Polisi Queens na Tausi na Jeshi Stars.”
Timu inaposhinda mechi katika ligi hiyo wachezaji, watu wa benchi la ufundi kila mmoja anapata Shs 87,500.