Nigeria. Mwili wa Rais wa zamani wa Nigeria, Muhammadu Buhari, aliyefariki dunia Jumapili ya Julai 13, 2025 wakati akipatiwa matibabu jijini London nchini Uingereza unatarajiwa kuzikwa leo Jumanne Julai 15, 2025.
Buhari aliyeiongoza Nigeria mara mbili kama mkuu wa jeshi na Rais, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Al Jazeera leo Jumanne, Gavana wa jimbo hilo, Dikko Radda amesema Buhari atazikwa katika mji aliozaliwa wa Daura katika jimbo la kaskazini la Katsina, mara mwili wake utakaporudishwa kutoka Uingereza.
Imeelezwa mwili wake utawasili Nigeria leo Jumanne na maziko yake yatafanyika baadaye usiku wa leo, kulingana na alivyosema Gavana Radda.
Kwa upande mwingine, Serikali ya nchi hiyo imetangaza leo Jumanne kuwa mapumziko ya umma kwa ajili ya kiongozi huyo wa zamani.
“Sikukuu hii ya umma inatoa fursa kwa Wanigeria wote kutafakari maisha yake, uongozi na maadili aliyodumisha,” amesema Waziri wa Mambo ya Ndani wa Nigeria, Olubunmi Tunji-Ojo.
Pia, Gavana Radda, ambaye alirejea Nigeria jana Jumatatu baada ya kuwa na familia ya Buhari katika mji mkuu wa Uingereza amesema:”Maiti itawasili kesho (leo), saa 12 jioni na mazishi yatafanyika saa 2 usiku,” ameongeza akinukuliwa na BBC pamoja na TVC News Nigeria.
Hadi sasa nyumbani kwake tayari kumejaa waombolezaji huku marafiki na familia wakisubiri kuwasili kwa mwili wake.
Kiongozi wa Kiislamu, Abdullahi Garangamawa ameiambia BBC kuwa ingawa yeye alikuwa Rais wa zamani, hakutakuwa na mazishi ya kiserikali bali kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, Buhari atazikwa haraka iwezekanavyo.
Kwingineko, Rais wa zamani, Goodluck Jonathan, aliyeshindwa na Buhari katika uchaguzi wa mwaka 2015, amemtaja kiongozi huyo kama mtu aliyejitolea katika kutimiza wajibu wake na aliitumikia nchi kwa uzalendo.
Naye, mtawala wa zamani wa kijeshi, Jenerali Ibrahim Babangida, ambaye alimpindua Buhari katika mapinduzi ya 1985, pia amesema Buhari ni mtu ambaye hata katika kustaafu kwake alibaki dira ya maadili kwa wengi na mfano wa unyenyekevu katika maisha ya umma.
Rais wa sasa Bola Tinubu, anatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo, ametangaza muda wa siku saba za maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya mtangulizi wake.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa Jumapili jioni, Tinubu alisema taifa litatoa heshima zake za mwisho kwa kiongozi huyo wa zamani kwa kushusha bendera zote za taifa nusu mlingoti kote nchini kuanzia Jumapili.
Ikumbukwe Buhari aliongoza nchi hiyo kwa mara ya kwanza kama kiongozi wa kijeshi, alihudumu mihula ya urais mfululizo kati ya 2015 na 2023. Alikuwa mwanasiasa wa kwanza wa upinzani kupigiwa kura madarakani tangu nchi hiyo irejee kwenye utawala wa kiraia.