RC Songwe aagiza udhibiti wa magendo mpaka wa Tunduma

Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame ameiagiza kamati ya usalama Wilaya ya Momba kuandaa mpango kazi wa namna ya kukabiliana na usafirishaji bidhaa kwa njia zisizo rasmi (magendo) katika mpaka wa Tunduma kati ya Tanzania na Zambia.

Makame ametoa agizo hilo leo Julai 15, 2025 baada ya kupokea ripoti hali ya makusanyo ya mapato mpakani hapo kutoka kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Songwe, Said Mwamloso.

Katika ripoti yake, Mwamloso amebainisha changamoto kubwa kuwa ni uwepo wa njia nyingi zisizo rasmi za kuvusha magendo.

Ili kukabiliana na changamoto ya uvushaji wa magendo mpakani Tunduma, Mkuu wa Mkoa, Makame ameitaka kamati ya ulinzi na usalama kuweka mpango madhubuti wa kukabiliana na magendo ambao utakuwa ni mwarobaini wa kuwarahisishia TRA kukusanya mapato kwa wingi.

“Ili kuongeza ukusanyaji mapato, kamati ya ulinzi na usalama katika Wilaya ya Momba, hakikisheni mnatatua changamoto ya vipenyo katika Mji wa Tunduma vinavyotumika kupitishia magendo na kupunguza jitihada za ukusanyaji mapato ya Serikali,” amesema Makame.

Katika hatua nyingine, Makame amekipongeza kituo cha pamoja cha forodha Tunduma (OSBP) kwa kukusanya zaidi ya Sh203 bilioni na kuvuka lengo la ukusanyaji mapato, huku kikichangia zaidi ya asilimia 85 ya makusanyo yote ya TRA katika mwaka wa mapato 2024/2025 katika Mkoa wa Songwe.

Amesema kituo cha pamoja cha forodha cha Tunduma ni miongoni mwa kituo muhimu ambacho kwa kiasi kikubwa ni kisaidizi cha Bandari ya Dar es Slaam kwa sababu asilimia 65 mpaka 70 ya mizigo hupitia katika mpaka wa Tunduma ikielekea katika nchi za kusini mwa Afrika.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Songwe, Said Mwamloso akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame katika kituo cha pamoja cha forodha mpaka wa Tunduma.



“Nawapongeza wafanyakazi wa kituo cha pamoja cha forodha (OSBP) kwa kufanikiwa kuvuka lengo na kukusanya zaidi ya Sh203 bilioni katika mwaka wa mapato uliopita. Ili kuendelea kufanya vizuri katika mapato, jiwekeeni malengo ya ukusanyaji kuanzia ya mwezi, robo mpaka mwaka,” amesema Makame.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi kituo cha OSBP, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Songwe, Said Mwamloso amesema wamefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh203 bilioni, sawa na asilimia 109 ya mapato kwa msimu wa mapato wa 2024/2025.

Amesema pamoja na kuvuka malengo ya ukusanyaji katika mpaka wa Tunduma, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha ukusanyaji mapato ambazo ni pamoja na upande wa Zambia kutokuwa na mfumo wa OSBP.

Amesema hilo limesababisha mpaka kuwa na vipenyo vingi vinavyotumika kupitisha magendo, kuwepo soko la mazao katikati ya mpaka na kuwepo kwa eneo dogo la maegesho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo amesema licha ya kuwepo vipenyo vingi vya kuvusha magendo, limekuwa tatizo kubwa linalosababisha mapato mengi kupotea.

Related Posts