Salomon Kalou ataja nondo tatu za Ecua

KAKA wa nyota wa zamani wa Chelsea na Ivory Coast, Salomon Kalou, aitwaye Bonaventure Kalou, ameweka wazi sifa tatu zinazomtofautisha kiungo mpya anayetajwa kujiunga na Yanga SC, Celestin Ecua.

Staa huyo inaelezwa amejifunga mkataba wa miaka miwili Jangwani akitokea Zoman FC. Bonaventure, 47, ambaye alicheza soka la kulipwa kwa mafanikio kuanzia Ivory Coast ambako alitamba akiwa na ASEC Mimosas hadi Ulaya alipozitumikia klabu kama PSG, Feyenoord, Auxerre na Lens alitaja mambo hayo kuwa ni nidhamu, ukomavu wa kiakili na kiu ya mafanikio.

“Ecua pamoja na kuwa na umri mdogo ni kiungo mshambuliaji mwenye nidhamu na kipaji kikubwa,” alisema Bonaventure alipozungumza na Mwanaspoti akiwa kwao Abidjan.

“Ana uelewa mzuri wa mchezo, anajua wakati gani apige pasi, asogee au ashambulie. Ni yule aina ya mchezaji anayewafanya wengine kuwa bora zaidi uwanjani,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Bonaventure, nguvu kubwa ya Ecua ipo kwenye ukomavu wake na tamaa ya mafanikio. “Hapotezwi na umaarufu wala mitandao ya kijamii. Anafanya kazi kwa bidii, anakubali kusikiliza na hana majivuno. Sifa hizi ni nadra sana kwa vijana wa sasa,” alisisitiza.

Ecua anaripotiwa kukataa ofa kutoka klabu za Tunisia na Morocco baada ya Yanga kuwasilisha projekti iliyomvutia zaidi, ikiwamo ushiriki wa timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Yanga imewahi kufaidika na usajili wa Waivory Coast kama Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua, na imeendelea kufuatilia vipaji kutoka Afrika Magharibi kama sehemu ya mkakati wake wa kutawala tena ukanda huu.

Hata hivyo, Bonaventure ametoa tahadhari kwa mashabiki wasiwe na matarajio ya haraka, akisisitiza kuwa Ecua anahitaji muda kuzoea mazingira mapya, lugha na aina tofauti ya soka.

“Soka la Afrika Mashariki ni tofauti na alilolizoea. Lakini yeye hujifunza haraka na ana akili ya kupambana,” alisema.

Aidha, Bonaventure aliisifia Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ushindani wake mkubwa, akisema kuwa mapenzi ya mashabiki na ushindani wa mechi kubwa kama Kariakoo Derby vinampa kijana huyo mazingira bora ya kukuza kipaji chake barani Afrika.

Related Posts