Dar es Salaam. Serikali imetangaza nafasi mpya 526 za kazi kwa Watanzania wenye sifa zinazohitajika, katika taasisi mbalimbali za umma zikiwamo hospitali ya Muhimbili (MNH), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Chuo cha Mweka na nyinginezo.
Tangazo hilo lililotolewa jana Julai 14, 2025, linaainisha kuwa nafasi hizo ni kwa ajili ya kada za afya, wanyamapori, elimu, uhasibu, sheria, teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), wahandisi, wasaidizi wa afya, madereva na mafundi mbalimbali.
Katika orodha hiyo, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) inaongoza kwa kutangaza nafasi nyingi zikiwemo za madaktari bingwa wa fani mbalimbali ikiwamo upasuaji, magonjwa ya ndani, watoto, afya ya akili, macho, masikio na koo. Aidha, nafasi za wataalamu wa uhandisi wa vifaa tiba, wataalamu wa macho, teknolojia ya mionzi, audiometri, usalama wa mtandao na wahasibu pia zimetangazwa.
Kwa upande wa Tawa, nafasi zimetangazwa kwa ajili ya maofisa wanyamapori (Conservators), rangers, maofisa maendeleo ya jamii, maofisa sheria, wahasibu, maofisa ununuzi, maofisa utalii na wataalamu wa mifumo ya kijiografia (GIS). Pia, nafasi za madereva, wapishi, mapokezi na mafundi mbalimbali wa umeme, useremala, rangi, na mitambo mizito zipo wazi.
Chuo cha Mweka kimepanga kuajiri mhadhiri msaidizi mmoja wa usimamizi wa wanyamapori pamoja na askari mmoja wa hifadhi (Ranger).
Serikali imesisitiza kuwa waombaji wote lazima wawe na elimu na uzoefu unaoendana na nafasi husika, na wanatakiwa kuwasilisha maombi kupitia mfumo wa kielektroniki wa ajira wa serikali (recruitment portal) kabla ya tarehe iliyowekwa.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, baadhi ya nafasi zina masharti ya umri wa waombaji kutopitiliza miaka 25 au 30 kulingana na kada husika.