Simba, MVP Uganda wako mezani

INAELEZWA Simba Queens inaelekea kukamilisha usajili wa winga wa Kampala Queens ya Uganda, Zainah Nandede kwa mkataba wa miaka miwili.

Simba Queens ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu uliopita kwa tofauti ya mabao dhidi ya JKT Queens zote zikikusanya pointi 47.

Winga huyo aliyeibuka na tuzo ya mchezaji bora wa mwaka huu Uganda (FUFA Female MVP), tayari ameaga rasmi ndani ya Kampala Queens kabla ya kujiunga na Simba Queens ya Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini Uganda, huenda Nandede akavaa uzi wa Msimbazi msimu ujao kwani tayari kila kitu kiko kwenye hatua za mwisho kukamilika.

Inaelezwa kama Simba itampata nyota huyo itakuwa imelamba dume kutokana na ubora wake, hata hivyo mbali na Wekundu wa Msimbazi timu za wanawake za Al Ahly ya Misri, Arab Contractors (Al Mokawloon), na Phoenix Marrakech ya Morocco zilikuwa pia zinawania saini ya mchezaji huyo katika dirisha hili la uhamisho.

“Mkataba wa Nandede na Kampala Queens ulikuwa unamalizika mwezi Agosti mwaka huu, mchezaji amekubali kucheza Tanzania kwani anaona kuna nafasi ya kucheza na kuonekana kwa sababu hana uhakika na Misri kama atacheza,” kilisema chanzo.

Msimu uliopita, Nandede alifunga mabao manane na kutoa asisti mbili, akisaidia Kampala Queens kutwaa ubingwa wa ligi mbele ya wapinzani wao wa jadi, Kawempe Muslim.

Nandede pia amewahi kuwa sehemu ya vikosi vya timu za taifa za vijana za Uganda (U17 na U20), kabla ya kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha wakubwa cha Crested Cranes.

Related Posts