KUNA kitu kilikuwa kinaendelea kati ya kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi na viongozi wa Simba ambacho kimemalizika kwa mmoja wao kununa.
Kocha huyo maarufu nchini anayeinoa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini alikuja nchini na mzigo akitaka kununua mashine moja ndani ya Simba.
Alipowaita mezani tu wamalize mambo, Simba wakatuna. Wakamwambia Steven Dese Mukwala hauzwi ng’o wala usihangaike.
Mukwala ambaye ni raia wa Uganda, alitua Simba msimu uliomalizika akitokea Asante Kotoko ya Ghana akiwa ndie mfungaji bora wa ligi hiyo kwa kumaliza na mabao 14.
Nabi ameliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli kwamba Mukwala alikuwa kwenye hesabu zake lakini mambo yamebadilika. Alisema kuwa kwa upande wa Kaizer ilikuwa tayari kukamilisha kila kitu ambacho Simba ilitaka ila ugumu umekuwa kwa mabosi wa mchezaji.
“Usajili wa Mukwala kwenda Kaizer umekwamishwa na klabu yenyewe kwani hawako tayari kumuuza kwani bado haijapata mbadala.
“Tayari tumeshaanza kuwekeza nguvu kwa mchezaji mwingine, kwani hakuna muda wa kupoteza na hili ndio dirisha kubwa la kujenga kikosi,” alisema Nabi ingawa tetesi za awali zilidai kwamba Kaizer ilikuwa tayari kutoa zaidi ya Sh500 milioni.
Tetesi kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa wanaitaka fedha ya Kaizer lakini wameshindwa kumuachia mshambuliaji huyo kwa sababu bado hawajapata mbadala wake ingawa kuna wataalamu wako sokoni wakifanya kazi maalumu ya kusuka kikosi.
“Simba imepiga hesabu za mbali na imeona haitaweza kumuuza mshambuliaji huyo ambaye tayari alishaonyesha kiwango bora, huku ikiwaza ugumu wa soko la washambuliaji ulivyo.
“Hivyo imefanya uamuzi ya kumbakiza kwani bado ana mkataba na rekodi nzuri, hivyo kama wataendelea na uamuzi huo basi huenda msimu ujao akaendelea kuuwasha,” kilisema chanzo chetu.
Nabi anaijua vizuri Ligi ya Tanzania akibeba makombe kadhaa alipokuwa Yanga enzi hizo, kwasasa ana presha ya kupata mafanikio na Kaizer ambayo ni kati ya klabu kubwa za Sauzi.
Mukwala alisaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Simba, huku msimu wake wa kwanza akiumaliza kwa kufunga mabao 13 na usumbufu wake kwa mabeki umeonekana kuwakosha Wanamsimbazi.
Msimu uliomalizika, Simba ilishika nafasi ya pili, ikiwa imecheza mechi 30 na kufikisha jumla ya pointi 78, huku ikilikosa Kombe la Ligi Kuu Bara kwa mara ya nne mfululizo, mara zote likienda kwa watani wao, Yanga.