Arusha. “Kinachoniuma zaidi nawaza ni nani nitakayemuamsha asubuhi tena kwenda naye msikitini?” Hayo ni maneno ya Yusuph Omary, baba mzazi wa watoto wawili waliogongwa na gari na kufariki dunia papo hapo wakati wakielekea msikitini kwa ajili ya sala ya alfajiri, saa 11 asubuhi.
Omary amesema hayo kufuatia vifo vya watoto wake wawili waliogongwa na gari aina ya Toyota Hiace wakati wakivuka barabara wakiwa wameshikana mikono.
Ajali hiyo imetokea alfajiri ya Julai 13, 2025 katika eneo hilo la Ngulelo jijini Arusha.
“Yaani mimi nimepata uchungu rohoni sana lakini ninachomshukuru Mungu kwanza ninachoamini kwa dini yangu mimi, watoto wangu wamekufa kwa sababu tulikuwa tunaenda kwenye ibada licha ya kwamba hatukuwa tumefika,” amesema.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Ngulelo katika barabara Kuu ya Arusha-Moshi ambapo baba huyo akiwa na watoto wake hao, gari hilo lilikuwa likipita ‘wrong sight’,ikiwa haijawasha taa,ilipowakaribia watoto hao iliwasha taa na kuwagonga ambapo kutokana na giza awali walikuwa hawajaliona gari hilo.
Akizungumza na Mwananchi jana Julai 14, 2025 nyumbani kwake Mtaa wa Tindigani, Kata ya Kimandolu, baba huyo amewataja watoto hao waliofariki kuwa ni Salmin Yusuph (11) na mwanafunzi wa darasa la tano na Samir Yusuph (9) mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Kimandolu.
Akisimulia tukio hilo, baba huyo ameeleza siku ya tukio akiwa na watoto wake hao walikuwa wakielekea msikitini kuswali ambapo imekuwa kawaida yake kwenda nao msikitini kila siku asubuhi na jioni.
Omary ameeleza kuwa siku zote wamekuwa wakivuka barabara hiyo kuelekea msikitini na hata akiwa amesafiri watoto hao huelekea msikitini pamoja na kwamba siku ya tukio gari hilo lilipowakaribia watoto hao liliwasha taa na kuwagonga.
“Ni kawaida yangu kuwaamsha saa 11 kwenda msikitini, tunavuka salama na tunarudi hususani jana tumefika kama kawaida tumefika pale tukahamia barabara nyingine na kuangalia magari ya Ngulelo kwenda mjini.
“Gari imetoka mjini ikienda Ngulelo ikiwa ‘wrong sight’ (uapande usio wake) haiwashi taa imekuja kuwasha taa kama mita mbili baada ya kuona watoto karibu, kulikuwa kuna giza inakuja kuwasha taa watoto wangu nilikuwa nao karibu na kama ni kugongwa ilikuwa tugongwe wote ni Mungu tu ameniepusha.
“Watoto wakagongwa, namshukuru Mwenyezi Mungu nilikuwa nawapeleka watoto wangu msikitini naamini watoto wangu wamekufa kwa sababu walikuwa wanaenda kwenye jambo la heri,” alisema.
Omary ameeleza kuwa watoto hao wamekuwa wakivuka barabara hiyo (barabara nne) kila mara hata wanapotumwa dukani na mama yao.
“Kinachoniuma zaidi nawaza ni nani nitakayemuamsha asubuhi tena kuondoka kwenda naye msikitini, ina maana ile gari inawasha taa hapa mimi siyo ujanja wangu kwamba nimerudi nyuma au nimefanyaje, watoto iliwashtua walikuwa wameshikana mikono wakati wanavuka nikiwa nyuma yao.
“Basi kilichowakuta kimewakuta ile gari imeonekana ni Hiace ila sikuwa na jinsi ya kuchunguza lile gari ilikuwa haikuwasha taa mwanzo na ilikuwa kwenye mwendo mkali. Baada ya kupiga kelele kuomba msaada watu walikuja, watu walikimbiza ile gari ila ilishaenda mbali,” ameeleza.
Kwa upande wake mama mzazi wa watoto hao, Amina Hussein ameeleza kuwa katika familia hiyo walijaliwa kupata watoto watano ambapo kwa sasa wamebaki watoto watatu baada ya wawili hao kufariki dunia kwa kugongwa na gari.
“Watoto walikuwa wanaenda kusali kufika barabarani wakapata hiyo ajali, nilienda kushuhudia wakiwa wameshafariki, watoto wangu walikuwa wawili kwa kweli walikuwa watoto wenye tabia nzuri, wanapenda mambo ya Mungu kwa kweli nasikitika sana watoto wangu kuondoka pamoja.
“Tunaomba ajali kama hizi zinapotokea zifuatiliwe na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria. Tulikuwa na watoto watano ila wamebaki watatu. Kiukweli inaniumiza sana nimeumia mno, siyo mara ya kwanza,” anasema.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Stella Mziray, ameliomba Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kuendelea kutoa elimu kwa madereva pamoja na watumiaji wa barabara ili kuepusha ajali.
“Kiukwlei ni huzuni sana kwa familia na jamii nzima maana kuondokewa na watoto wawili inauma sana. Jeshi la Polisi lisichoke kutoa elimu ya barabarani kwa waendesha vyombo vya moto na watumiaji wa barabara,” anasema.
Mmoja wa wanafamilia, Hassan Omary amesema miili ya watoto hao inasafirishwa kuelekea Soni wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga kwa ajili ya maziko.
“Tumepata msiba mzito ila tunaomba Serikali isisitize zaidi tunavyoendesha vyombo vya moto, tuzingatie sheria za barabarani ili kuepusha ajali zinazoepukika,” amesema.