Stein, Tausi zafanya kweli BDL

STEIN Warriors na Tausi Royals zimeonyesha makali katika Ligi ya Kikapu Dar es Salaam kwa kuibuka na ushindi katika michezo yao kwenye Uwanja wa Donbosco Upanga, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza, Stein iliyopanda daraja mwaka huu, iliichapa DB Oratory kwa pointi 57-47, na kuonyesha kuongeza kiwango kadiri ligi inavyoendelea, huku Kocha wa timu hiyo,  Karabani Karabani akisema mipango yao ni kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika (BAL).

Timu hiyo inayoongoza kuwa na wapenzi wengi, iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 14-9 na 14-11 na hadi mapumziko iliongoza kwa pointi 28-20, huku robo ya tatu DB Oratory ikiongoza kwa pointi 21-11, na robo ya nne Stein ikapata pointi 18-6.

Brian Mramba aliifungia Stein pointi 20, huku Isaya Aswile akiipa pointi 15 DB Oratory.

Katika mchezo mwingine uwanjani hapo, Polisi Stars iliifunga Kigamboni Queens kwa pointi 70-41, hulku ikiongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 18-13, 14-7, 21-14 na 17-7.

Faith Mziray wa Polisi Stars alifunga pointi 21, akifuatiwa na Merina Remmy aliyefunga 11, huku Sada Ally wa Kigamboni Queens akifunga pointi 15.

Tausi yaifinya Ukonga Queens

Kazi ilikuwepo kwa Tausi Royals iliyoinyoa Ukonga Queens  kwa pointi 48-41, katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Hata hivyo, ushindi kwa timu hiyo haukupatikana kirahisi na iliwalazimu Tausi kupindua meza robo ya tatu na nne.

Ukonga Queens iliongoza robo ya kwanza kwa pointi 9-6,  baadaye Tausi ikapata pointi 15-12 na hadi mapumziko zilifungana pointi 21-21.

Kocha wa Tausi alimwingiza Tukusubira Mwalusamba aliyezima kasi ya Ukonga Queens kutokana na uwezo wa kupora mipira  bila ya kufanya madhambi na kutoa asisti.

Katika mchezo huo, Juliana Sambwe wa Tausi alikuwa kivutio kwa kuonyesha uwezo mkubwa wa kuituliza timu na kuichanganya Ukonga Queens iliyopoteza, huku Tukusubira akiwa na kazi ya kupora mipira (Steal). 

Tumaini Ndossi wa Tausi alifunga pointi 21 akifuatiwa na Juliana aliyefunga 14, huku kwa Ukonga, Nyajima Manji alifunga pointi 13, akifuatiwa na Sophia Warioba aliyefunga 11.

Related Posts