Dar es Salaam. Baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mitaala mipya kwa shule za msingi na sekondari, sasa ni zamu ya vyuo vikuu, mitaala iliyohuishwa inaanza kutumika katika mwaka mpya wa masomo 2025/2026.
Hatua hii ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilitoa muda mfupi baada ya kuingia madarakani Machi 19, 2021 alipoelekeza kuangaliwa upya kwa mfumo wa elimu ili utengeneze wanafunzi wenye ujuzi.
Kama ilivyofanyika kwa ngazi ya shule za msingi na sekondari, mapitio ya mitaala yalifanyika pia kwa ngazi ya elimu ya juu na mitaala hiyo itaanza kutumika katika mwaka wa masomo 2025/2026.
Kufutia hilo, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imewataka waombaji wa shahada ya kwanza kusoma miongozo na programu za vyuo husika kabla ya kuomba ili kuondoa uwezekano wa kuchagua kozi ambazo hazipo.
Akizungumza leo Jumanne, Julai 16, 2025 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema miongoni mwa vitu vinavyopaswa kuangaliwa kwa umakini na waombaji wa shahada ya kwanza ni programu za vyuo husika.
“Leo tunafungua awamu ya kwanza ya dirisha la udahili katika mwaka mpya wa masomo itakayodumu kwa siku 26, msisitizo kwa waombaji ni kusoma miongozo na kupata taarifa rasmi kutoka vyuo husika sio kusikia habari za mtaani.
“Unataka kusoma programu fulani, hakikisha kwamba inapatikana kwenye hicho chuo unachotaka kusoma, kwa maboresho haya ambayo yamefanyika upo uwezekano kuna programu zimefutwa au kubadilishwa hivyo ni lazima uwe makini,” amesema Profesa Kihampa na kuongeza.
“Soma mwongozo wa TCU pia ingia kwenye tovuti ya chuo au wasiliana na chuo moja kwa moja ili kujua taratibu za kutuma maombi na kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo ili kujiridhisha.
Profesa Kihampa pia ametoa angalizo kwa waombaji na wazazi kuwa makini na vishoka na watu wanaojiita madalali wa vyuo kwani mfumo wa elimu ya juu hauna utaratibu huo.
Awamu ya kwanza la dirisha la udahili imefunguliwa leo Julai 15 na linatarajiwa kufungwa Agosti 10, 2025.
Kwa muda mrefu kilio cha waajiri kwamba wahitimu wengi wa vyuo vikuu hawana uwezo wa kufanya kazi kutokana na kukosa stadi muhimu ambazo zinahitajika kwenye soko la ajira.
Imekuwa ikielezwa vyuo haviwaandai vyema wahitimu wake kuingia moja kwa moja kwenye uzalishaji, hali inayowalazimu waajiri kuingia gharama ya kuwafundisha upya ili kuwaweka katika misingi inawawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Kupitia Mradi wa wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET) changamoto hiyo ilianza kufanyiwa kazo ambapo yamefanyika mapitio ya mitaala kwa kuwahusisha waajiri, wazoefu katika nyanja mbalimbali za uzalishaji.
Kufanikisha hilo, kiasi cha Sh18.23 bilioni kilitengwa kwa ajili ya kuhuisha na kuandaa mitaala mipya kwa taasisi za elimu ya juu na kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inaendana na kujibu mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Mchakato wa mapitio ya mitaala ya elimu ya juu ulihusisha kuundwa kwa kamati za ushauri wa viwanda zinazowahusisha wadau katika sekta mbalimbali ambao kwa pamoja walipitia mitalaa na kushauri nini kiwepo kulingana na uhitaji wa soko la ajira na maendeleo ya teknolojia.
Akizungumzia hilo, mdau wa elimu wa Catherine Francis amesema kwa muda mrefu mfumo wa elimu unahitaji kufanyiwa maboresho ili kuendana na mahitaji ya sasa.
Amesema kinachoonekana sasa ni kuzalishwa kwa wahitimu wengi ambao hawana sifa za kuajiriwa au wanasoma masomo ambayo hayawajengei maarifa yatakayowawezesha kufanyia kazi na matokeo yake kuonekana hawafai.
“Ni jambo la ajabu kwa kijana ambaye amesoma hadi chuo kikuu halafu anaishia kuuza mitumba, haina maana kwamba mitumba sio biashara lakini je kweli tunampeleka kijana akasome chuo na kuhitimu shahada ya kuuza mitumba?
“Kuna tatizo mahali ambalo kama taifa tunapaswa kuliangalia kwa kina na kutafuta ufumbuzi wake kabla hatujaelekea kubaya zaidi, hali ni mbaya elimu ipo ila inatakiwa kuwa msaada kwa wanafunzi sasa kama maboresho yamefanyika tunatarajia kuona matokeo chanya,” amesema.
Catherine amebainisha kuwa Tanzania inahitaji mfumo wa elimu unaotengenezwa katika namna ambayo itamfanya mwanafunzi kuyatumia maarifa aliyoyapata shuleni katika kutatua changamoto mbalimbali anazokutana nazo.