TIA kuwapunguzia gharama, safari wanaosaka elimu Zanzibar

Unguja. Wakati Serikali ya Tanzania ikitoa Sh15.9 bilioni kujenga Taasisi ya Uhasibu (TIA) kampasi ya Zanzibar, hatua hiyo imetajwa kuwapunguzia mzigo wanafunzi hususani waliopo kazini kufuata taaluma hiyo nje ya Zanzibar.

Hayo yamebainishwa leo Julai 15, 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania, Profesa William Pallangyo katika maonyesho ya wiki ya elimu ya juu yanayofanyika katika viwanja vya Mnazimmoja Unguja Zanzibar.

Profesa Pallangyo amesema wanafunzi wengi walikuwa wakihangaika kufuata elimu hiyo Tanzania bara, lakini wakaona kuna umuhimu wa kuweka kampasi kisiwani humo ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa fedha za ujenzi huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikitoa zaidi ya ekari 20 kwa ajili ya chuo hicho.

“Baada ya kuona umuhimu wa kusogeza huduma karibu na wananchi TIA imekuja Zanzibar kampasi hii inajengwa Mkoa wa Kusini Unguja, hivyo hakuna sababu tena ya kusafiri kwenda Tanzania Bara kufuata elimu kama ilivyokuwa awali,” amesema na kuongeza;

“Tunazishukuru Serikali zote mbili, kwa sababu kulikuwa na usumbufu wa kupata elimu, lakini kwa sasa baada ya kuweka kampasi hii watu watasoma hapa hapa bila kutaka kusafiri kwenda sehemu nyigine,” amesema.

Amesema kuwa ujenzi huo kwa sasa umefikia asilimia 20, na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 16 ijayo, kwani ni mradi wa miezi 24.

Tayari sehemu ya kwanza ya mradi huo, ambayo ilipangwa kutekelezwa kwa miezi minane, imekamilika kama ilivyopangwa.

Baada ya kukamilika kwa mradi mzima, eneo hilo litakuwa na mabweni, majengo ya utawala, pamoja na madarasa, na litakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja.

Hata hivyo, kwa sasa taasisi hiyo katika kampasi ya Zanzibar wanatoa cheti cha awali na shahada ya uzamili katika uhasibu na rasilimali watu katika eneo lao la muda Michenzani mall.

“Hii ndio fursa ya kipekee kwa watu wanaotafuta elimu, tunawafahamisha kuwa tupo Zanzibar wanakaribishwa wajifunze na kupewa miongozo mbalimbali,” amesema.

Profesa Pallangyo amesema “Kuna mambo mengi ya usimamizi wa fedha kuweka hesabu vizuri, ushauri na kuhusu masuala ya masoko na tafiti kuhusu mambo yanayosumbua jamii na taifa kwa ujumla kwa hiyo watasaidia kufanya kazi hizo vizuri,” amesema.

“Elimu unaipata hapahapa Zanzibar amaabyo watu wangeitumia zaidi kuifuata maeneo mengine lakini itamsaidia mtumishi wa umma kuendelea na kazi huku akiwa aansoma tofauti na ilivyokuwa awali mtu analazimika kuacha kazi kisha kufuata elimu,” amesema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Aida Juma Maulid amesema ni faraja kubwa kuona wamejitokeza kuweka kampasi hiyo kisiwani humo kwani watasaidia wanafunzi wengi pasi na kuangaika kusafiri kwenda mbali kusaka taaluma.

“Mimi nafarijika kuleta huduma hii hapa Zanzibar, wanafunzi wengi wanajiunga kutokana na umahiri wao wa kufundisha na fani zao za kipaumbele, kwa hiyo tuwashajihishe wajiunge, waje watapata kudahiliwa moja kwa moja,” amesema

Amesema ni vyema kuchagua fani za kipaumbele ili baadaye iwe rahisi katika upatikanaji wa ajira na maeneo ambayo yana upungufu wa wafanyakazi.

Baadhi ya wanafunzi ambo wamemaliza elimu ya sekondari wanasubiri kujiunga na elimu ya juu wamepongeza hatua hiyo kwani itawapunguzia gharama na usumbufu na kwamba baada ya kutembelea banda hilo wameelezwa mengi namna wanavyoweza kunufaika katika kozi wanazotaka kusomea.

“Nimefahamu kwa undani kozi hii, nikimaliza kazi zipi nitafanya na nitakuwa nani nashukuru hatua hii hakika ni vyema kuendelea mambo kama haya yanatufungua uwezo wanafunzi,” amesema Salum Said Juma aliyemaliza kidato cha sita na anataka kusomea kozi ya usafiri na usafirishaji.

Related Posts