UCHAGUZI MKUU 2025: Mawakala wa fedha mtegoni

Dar/mikoani. Mawakala wa huduma za kifedha mitandaoni wamejikuta mtegoni, baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuweka wazi mpango wake wa kuwamulika kwa kina kujua iwapo wanatumiwa kusambaza miamala ya rushwa kwa wajumbe.

Mpango huo wa Takukuru ni sehemu ya juhudi za kudhibiti vitendo vya rushwa, vinavyodaiwa kufanywa na watiania wa nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi ili wajenge ushawishi kwa wajumbe wawapigie kura za maoni.

Kwa mujibu wa Takukuru Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, mawakala wa miamala ya fedha wanapaswa kuchukua tahadhari na kufuata miongozo ya kazi zao hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, leo Jumanne Julai 15, 2025 kuhusu rai iliyotolewa na Takukuru, mawakala hao walisema ni vigumu kwao kutambua kama miamala inayopitia mikononi mwao inahusiana na vitendo hivyo.

Ingawa mawakala wanasema hivyo, miongozo ya kazi yao inawataka kutotuma fedha kwa namba ya mtu asiyefika ofisini kwao, jambo wanalosema hawana elimu ya kutambua miamala yenye viashiria vya rushwa, hivyo wanajikuta wakihudumu katika mazingira ya sintofahamu na hatari kisheria.

Miongozo na utaratibu wa huduma za kifedha kwa mawakala, inaeleza ni kosa kutuma fedha kwa mtu asiyekuwepo eneo la kazi na kufanya hivyo inawezekana ukatuma kwa mtu asiye sahihi.

“Inakuwa vigumu kwa wakala kujua iwapo fedha aliyopewa kutuma ni rushwa au vinginevyo, kwa kuwa jukumu la wakala ni kutoa huduma kwa mteja,” amesema Maria Antony, wakala wa fedha Moshi, Kilimanjaro.

“Huwezi kujua kama hii pesa ni ya rushwa au ya matumizi mengine. Mtu anaweza kutuma laki tano, milioni moja, hata zaidi, lakini sisi hatuwezi kuuliza ni kwa ajili ya nini, tunachotazama ni jina liwe sawa na muamala ukamilike,” amesema Maria Antony, wakala wa fedha mjini Moshi.

Wakala mwingine, Sasha Lema amesema kuna wakati mteja anapeleka namba zaidi ya moja akitaka zote zitumiwe fedha, jambo linalowapa wakati mgumu kujua iwapo wanaotumiwa ni wajumbe au wateja kama wengine.

“Yawezekana mtu anayetoa au kuweka fedha ni mteja wa kila siku au ni mpya lakini ni ngumu kumhoji dhamira na lengo la yeye kutuma hiyo fedha hata kama anatuma kwa watu wengi au anaweka hela nyingi, tupewe elimu kufahamu nini cha kufanya katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi,” amesema Lema.

Ukiacha nyakati za uchaguzi, amesema kuna wakati wanakuwa na wateja wenye vibarua wengi, katika malipo wanakabidhi namba zao kwa wakala watumiwe fedha.

Kwa upande wa Hussein Jackson anayefanya kazi ya uwakala Tabata, Dar es Salaam, amesema wakala anapaswa kutumia vitabu vya taarifa za muwekaji na mpokeaji, lakini mawakala wengi hawavitumii.

“Sheria inasema lazima ujaze taarifa za mteja, kama jina, namba ya kitambulisho kikiwepo cha Nida na mawasiliano, lakini wateja wengi hawafanyi hivyo na ukilazimisha anaondoka kwa kuwa hana muda wa kufanya hivyo,” amesema Jackson.

James John amesema ni mara nyingi wanapewa fedha kwa ajili ya kutuma na hakuwahi kuhoji kuhusu sababu za kutuma na taarifa za mpokeaji.

“Miaka iliyopita tulihitaji kitambulisho cha mtu ili aweze kutuma au kutoa fedha za kiwango chochote ila kwa sasa huo utaratibu haufanyiki,” amesema John.

Wakala mwingine, Ezekiel Ryoba amesema idadi ya watu wanaoweka fedha kwenye simu imeongezeka, inakuwa vigumu kwao kufuatilia kwa undani kila mteja.

Kwa upande wa Bahati Joseph, amesema elimu ndilo jambo la msingi wanalopaswa kupatiwa katika kujitenga na vitendo vya rushwa.

Wakala kutoka mkoani Tanga, Elizabeth Richard amesema kwa mafunzo aliyopokea, ni kosa kutuma fedha kwa mtu asiyekuwepo eneo lako la kazi, kufanya hivyo unaweza kutuma sehemu isiyo sahihi.

Mwongozo huo, amesema unataka iwapo mtu anataka kutuma fedha kwa wengi, zinapaswa kuingizwa kwenye simu yake ndipo asambaze kwingineko.

Hatua hiyo, Elizabeth amesema inasaidia kuzuia mambo ya rushwa au kutumiwa fedha watu wanaokwenda kufanya matukio ya uhalifu.

“Wakala hatakiwi kutuma fedha nyingi kwenda namba usizozifahamu. Kufanya hivyo ni makosa, likitokea tatizo unakosa msaada au ushahidi kuwa fedha ulituma kwa nani,” amesema.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Temeke, Holle Makungu, amewataka mawakala wa fedha na wananchi kwa jumla kuwa waangalifu na kufuatilia kwa karibu mienendo ya utumaji wa fedha kipindi cha uchaguzi.

“Tunapita kila sehemu, tunatoa elimu na tunawaambia wazi kuhusu hatari ya kutumiwa kama njia ya kutoa rushwa, wengine wakielezwa wanashangaa, hawakuwa wanajua kuwa fedha wanazopewa kupitia mawakala zinaweza kuwa sehemu ya vitendo vya rushwa,” amesema Makungu.

Amesema baadhi ya watu wanatuma fedha kwa majina mengi kwa wakati mmoja, jambo linalozua shaka hasa kipindi cha kuelekea uchaguzi.

Makungu amesema kuna ushahidi kuwa baadhi ya fedha hizo hutumwa kwa wajumbe wanaohusika katika mchakato wa uchaguzi, lakini mawakala wa fedha hawajui kinachoendelea kwa kuwa hawafuatilii kwa kina madhumuni ya miamala hiyo.

“Kuna mtu anatuma fedha kwa watu zaidi ya 100 mara moja, hivyo wakala anatakiwa kuuliza, yapo majina ambayo yanafahamika huko mitaani kuwa ni wanachama wa chama fulani,” amesema Makungu.

Kwa upande wa Mkoa wa Kinondoni, mkuu wa taasisi hiyo, Christian Nyakizee ametoa wito kwa wananchi kujiepusha kupokea rushwa, wasinunuliwe haki yao.

“Tunaona kuna haja ya kutoa elimu kwa mawakala wa fedha wasiingie kwenye mtego huu, kila atakayebainika kushiriki rushwa sheria itafuatwa. Wito wangu ni wananchi watoe ushirikiano kwa Takukuru kupitia ofisi zetu au watupigie simu yetu namba 113,” amesema Nyakizee.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Christopher Myava amesema kila kona ya jiji na wilaya zake amepeleka timu na kila mwenye kushukiwa atafuatiliwa kwa njia tofauti tofauti ikiwamo teknolojia hadi ukweli ujulikane.

Amekiri kumekuwepo taarifa za watu wengi kuingia jijini Dodoma wakiwamo wagombea na wasio wagombea.

“Tunatambua kabisa kwamba teknolojia na ujanja umeongezeka, watu wa sasa siyo wale wa zamani, lakini nawaambia kuwa hata watumishi wa Takukuru wa sasa siyo wale wa zamani na kwetu pia tumekuza teknolojia kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Kwa upande wa Mkuu Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo amesema tayari wamepata taarifa ya baadhi ya mawakala wa simu kutumika kuwatumia wajumbe fedha na kwamba wamejipanga kutoa elimu ili kuwaepusha na vitendo vya rushwa.

“Tuna taarifa kwamba baadhi ya mawakala wa simu wanatumika katika vitendo vya rushwa kwa wagombea. Ndani ya wiki hii tumepanga kuwaita mawakala wote wa simu, kwani wakala anapotumika kuwatumia wajumbe miamala ya fedha anafanya kosa na wakati mwingine wanafanya kwa sababu hawajui kama ni kosa.

Sisi tutakaa nao tutawaelimisha wasitumike kuwatumia wajumbe fedha,” amesema Chaulo.

Habari imeandikwa na Devotha Kihwelo(Dar),Rajabu Athumani (Tanga), Joseph Lyimo(Manyara), Habel Chidawali(Dodoma),Mbeya( Saddam Sadick),Flora Temba (Moshi).

Related Posts