Singida. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija amesema ushirikiano madhubuti kati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na wadau mbalimbali hususan Mahakama, umekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya Mfuko huo.
Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kati ya majaji wa Mahakama ya Rufani na NSSF kinachofanyika mkoani Singida, Jaji Mwarija amesema ushirikiano huo umewezesha wadau kujadili changamoto kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kubuni mbinu bora za kuboresha huduma kwa wanachama.
Aidha, amewapongeza waandaaji wa kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kwa kushirikiana na NSSF.
Amesema kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2021–2025), hususan nguzo yake ya tatu inayolenga kuhusisha wadau katika utoaji wa haki.
Amesisitiza pia umuhimu wa kushughulikia changamoto za masuala kama mirathi kwa pamoja kwa kuunda mifumo thabiti ya kutambua wategemezi na kurahisisha upatikanaji wa haki.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema tangu Serikali ilipofanya maboresho makubwa ya sheria mwaka 2018, NSSF imekuwa chombo pekee kinachotoa huduma za hifadhi ya jamii kwa sekta binafsi na kwa walio katika ajira binafsi.
Amesema kupitia marekebisho ya Sheria ya NSSF Sura ya 50 ya mwaka 2024, wanachama sasa wanaruhusiwa kuchangiwa na waajiri zaidi ya mmoja.
Amesema vipindi vya uchangiaji vya zaidi ya miaka 60 vinatambuliwa na adhabu ya kuchelewa kuwasilisha michango imeshushwa kutoka asilimia 5 hadi 2.5. Aidha, walio katika sekta isiyo rasmi sasa wanaruhusiwa kujiunga kwa lazima kupitia mpango maalumu.
Mshomba amebainisha kuwa thamani ya Mfuko imeongezeka kutoka Sh4.5 trilioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh9.6 trilioni ifikapo Juni 2025, sawa na ongezeko la asilimia 98.
“Pia michango ya wanachama imepanda kutoka trilioni 1 hadi trilioni 2.16, na mapato yatokanayo na uwekezaji yameongezeka kutoka Sh527.1 bilioni hadi bilioni 543.5,” amesema mkurugenzi huyo.
Pia, amesema thamani ya vitega uchumi vya Mfuko imeongezeka na kufikia trilioni 8.2 kutoka trilioni 7.4. akizungumzia malipo ya mafao, Mshomba amesema yamefikia Sh947.2 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikilinganishwa na Sh884.8 bilioni ya mwaka uliotangulia ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.
Aidha, alieleza dhamira ya Mfuko kulipa mafao ya wastaafu ndani ya saa 24 baada ya kustaafu, lengo linalowezeshwa na maboresho ya TEHAMA ambapo huduma za NSSF kwa sasa zinatekelezwa kwa asilimia 90 kwa njia ya kidijitali.
“Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2025, idadi ya wanachama wachangiaji imeongezeka hadi 1,816,026 kutoka 1,358,882 mwaka uliotangulia, ongezeko la asilimia 19,” amesema Mshomba.
Amesema mabadiliko ya kisheria yameruhusu kila Mtanzania aliye katika sekta ya kujiajiri kujiunga na mpango wa hifadhi ya jamii, hatua inayoongeza uhakika wa kipato na usalama wa baadaye kwa wananchi.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya waajiri kutowasilisha michango kwa wakati au kuwasilisha kiwango kidogo tofauti na mishahara halisi ya wafanyakazi wao.
Hata hivyo, NSSF inaendelea kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu umuhimu wa kuwasilisha michango kwa wakati na kwa usahihi.
Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Mahakama ya Rufani, Shabani Ally Lila, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, ameishukuru NSSF kwa kuratibu kikao kazi hicho.
Amesema hilo limekuwa jukwaa muhimu la kujadili kwa pamoja namna ya kulinda haki za wanachama na kuhakikisha mafao yanalipwa kwa wakati na kwa haki.
Naye Bupe Kibona, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama ya Rufani, amesema kikao kazi hicho kimewapa maarifa ya kina kuhusu taratibu na mfumo wa NSSF, jambo litakaloisaidia mahakama kushughulikia kesi zinazohusu hifadhi ya jamii kwa haraka na kwa usahihi zaidi.
Amesema mpango wa NSSF Scheme ni hatua chanya inayowawezesha Watanzania wote kujiunga na kunufaika na mafao ya hifadhi ya jamii.