Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimethibitisha kuwa viongozi wake wawili wakuu, Brenda Rupia ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi pamoja na Leonard Magere, Mkurugenzi wa Rasilimali, Miradi na Uwekezaji, wameachiwa kwa dhamana baada ya kushikiliwa na Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho leo Jumanne, Julai 15, 2025, viongozi hao wanatakiwa kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati, jijini Dar es Salaam kesho Jumatano, Julai 16, 2025.
Wawili hao walikamatwa kwa nyakati na maeneo tofauti. Magere alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam akiwa njiani kuelekea Uingereza, huku Brenda akikamatwa eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga, akielekea nchini Kenya.
Akizungumza kwa niaba ya chama, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Diaspora, John Kitoka amesema Chadema inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa tukio hilo huku wakisisitiza haki, uwazi na kufuata taratibu za kisheria katika mchakato mzima.
“Tunaishukuru jamii ya Watanzania, wanachama na wapenzi wa Chadema kwa mshikamano na uungwaji mkono wanaoendelea kuonyesha katika kipindi hiki kigumu,” amesema Kitoka kupitia taarifa hiyo.
Endelea kufuatilia Mwananchi.