Dar es Salaam. Wanazuoni nchini wametaka mabadiliko ya Sheria ya Vyuo Vikuu ili kuruhusu ushiriki huru wa wanazuoni katika kuchagiza mijadala na maendeleo ya demokrasia na elimu ya uchaguzi nchini.
Hayo yamejiri katika mahojiano maalumu na Mwananchi kufuatia maoni kuwa taasisi za elimu nchini zimekuwa kimya katika ajenda za demokrasia na uchaguzi tofauti na ilivyozoeleka.
Sheria hiyo inawazuia wanafunzi wa vyuo vikuu kufanya siasa wakiwa vyuoni, jambo ambalo limetafsiriwa kama kuzuia ukuaji wa vijana bora kiuongozi kuanzia wakiwa vyuoni hadi watakapoingia uraiani kuanza maisha halisi ya kisiasa.
Wanasiasa na wachambuzi wa siasa wamekuwa na maoni tofauti wakilalamikia ukimya wa vyuo vikuu katika kuonya, kukosoa na hata kushauri na athari zake kwa ustawi wa taifa.
Awali, akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Habari na Mambo ya Nje wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), John Mrema amevituhumu vyuo vikuu kwa kuacha jukumu lake la msingi la kufanya tafiti na kuchagiza fikra za mabadiliko katika taifa, akidai sasa vimeshuka hadhi yake na kuwa kama sekondari za kata.
“Zamani tuliviona vyuo vikuu vikiongoza makongamano makubwa ya kitaifa na kutoa taarifa za kitafiti ikiwemo kuendesha mijadala iliyoibua fikra za mabadiliko. Kwa sasa vyuo vyetu vimeacha njia na kubaki kama sekondari za kata tu ambazo hazina ajenda yoyote ya mabadiliko katika nchi,” amesisitiza Mrema.
Mrema amedai kuwa ukimya wa vyuo si suala la kupuuzwa kwani jamii inakosa fursa ya kupata mawazo ya kitaalamu na kitafiti ambayo yanatokana na wasomi hasa wanaotoka vyuo.
“Inashangaza sana kuviona vyuo vikuu vikikaa kimya na kutunga kanuni za kuwazuia vijana kushiriki siasa huku vikifundisha sayansi ya siasa ambayo wanaoisoma wanazuiwa kuishiriki, kama taifa lazima tujiulize tunaelekea wapi”.
Alitolea mifano viongozi maarufu nchini wakiwemo Joseph Warioba na Jakaya Kikwete ambao walianza siasa wakiwa vyuoni na jinsi ushiriki siasa vyuoni ulivyowajenga kiuongozi.
Akizungumzia hatua hiyo, aliyekuwa mhadhiri na Balozi mstaafu, Dk Benson Bana ameeleza kusikitishwa na ukimya wa vyuo vikuu akitahadhalisha kuwa ukimya wa wasomi nchini unapelekea jamii kuamini taarifa za mitandaoni zisizo na utafiti wa kutosha.
Dk Bana amesisitiza kuwa vyuo vikuu vina wajibu mkubwa kwa jamii kufuatilia, kutafiti na kuendesha makongamano yenye kuibua mijadala ya kitaifa juu ya maoni ya umma na kutoa dira ya mwelekeo kutokan na tafiti juu ya hali halisi na mahitaji makuu kwa wakati huo.
“Ni kweli kabisa, wanazuoni tumenyamaza, binafsi tangu nilipostaafu uongozi wa Redet na utumishi ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nimekaa kimya lakini bado ni mzalendo na Mtanzania mwenye nafasi ya kutoa mchango wangu pale ninapohitajika.
“Yapo mengi sana yanaongelewa na umma lakini yanakosa tafiti za wanazuoni na kuiacha jamii ibaki na maoni ya mitandaoni tu,” amesema Dk Benson alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumanne Julai 15, 2025.
Dk Bana amesisitiza kuwa wanazuoni hawapaswi kukaa kimya hasa katika kipindi hiki ambapo taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu ili watu wapate taarifa za kitafiti juu ya ajenda za kisiasa zinazosukumwa na makundi mbalimbali na kujua maoni ya umma yapo upande gani.
“Tafiti za wasomi zingeweza kuchambua ajenda zinazoendelea mfano, leo tungefanya uchaguzi nani angeibuka, ajenda ya No reforms, No election, wananchi wanamaoni gani na mengine mengi yanayosema yangeweza kuipa jamii dira na mwelekeo wa kujua msimamo wa umma” amesema.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo ameeleza kusikitishwa na mifumo ya kisheria inayowabana wanazuoni kushiriki mijadala huru juu ya ajenda za kisiasa huku akidai mabadiliko ya katiba kuwa ndiyo yatawezesha vyuo vikuu kuongoza jamii katika tafiti na taarifa za kitaalamu bila kuingiliwa na makundi mengine.
“Wanazuoni mnataka waongee nini katika mazingira haya ambayo sheria imewanyima nafasi hiyo? Sheria imezuwia vyuo kufanya siasa kwahiyo mwanazuoni anapotoa hoja anaonekana anafanya siasa chuoni. Sasa katika hali hii mkuu wa chuo kipi ataruhusu chuoni kwake lifanyike kongamano kubwa la kisiasa? amehoji Dk Masabo.
Mwanazuoni huyo amebainisha kwamba ili jamii inufaike na tafiti na maoni ya wasomi vyuoni, mabadiliko ya sheria yanahitajika katika kuwaandaa kushiriki na kusimamia tafiti za masuala ya kisiasa zaidi ya kushiriki siasa kama wapigakura pekee.
“Wanafunzi hawaruhusiwi siasa vyuoni, hata wanaozungumza wakizungumza kisichotarajiwa wanaonywa, yanahitajika marekebisho ya sheria kwanza ndipo wanazuoni tulaumiwe kwa ukimya siyo katika mfumo unaotenga baadhi ya makundi kushiriki siasa,” amesisitiza.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Udsm, Dk Richard Mbunda amewataka wadau wa siasa kuacha kusubiri wanazuoni pekee kwani siasa si ya watu fulani bali kila mmoja atimize wajibu wake ili kuweza kufikia mabadiliko ya kweli.
“Kubwa hapa ni uoga, watu wamekuwa waoga katika kuzungumzia masuala ya msingi ya nchi, uoga huu upo kila mahali, si kwa wanahabari, wanasiasa, hata wanazuoni tunakumbwa na tatizo la uoga vilevile,” ameongea Dk Mbunda.
Mhadhiri katika kitivo cha sayansi ya jamii chuoni hapo, amebainisha kuwa matukio ya kuona wale wanaojitokeza hadharani na ajenda za msingi wanashughulikiwa yanarudisha nyuma ushiriki wa makundi katika ajenda za masuala muhimu ya kitaifa hasa ya kisiasa na uchaguzi.
“Pia lipo tatizo la kiuchumi, mijadala mingi vyuoni hufanyika kwa ufadhili hasa kutoka mashirika kama USAIDS, utawala wa Donald Trump umesitisha misaada ya mashirika hayo kwa hiyo hii nayo imeathiri uwezo wa taasisi nyingi kufanya makongamano haya,” ameongeza Dk Mbunda.
Tanzania inajiandaa kuingia katika uchaguzi mkuu Oktoba 2025 huku vyuo vikuu vikiwa kimya katika majukwaa ya hoja juu ya uchaguzi huo na masuala mengine ya kisiasa tofauti na ilivyozoeleka. Hali hiyo imeibua mitazamo tofauti katika makundi tofauti nchini.
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesisitiza haja ya vyuo vikuu kurejea katika jukumu lake la kijamii ili kwezesha kujenga uelewa wa kitaalamu katika masuala ya kisasa kwa jamii nchini.
“Tangu miaka ya 1970 vyuyo vikuu vimekuwa nguzo mhimu katika kusukuma agenda za kisaisa, hata Mwalimu Nyerere alikwenda sana pale UDSM lakini kwa sasa vyuo vimeacha jukumu lake hili muhimu kwa jamii. Vyama vya siasa tunaathirika pakubwa na hili,” amesema Shaibu.