Dodoma. Licha ya jitihada za Serikali kuhakikisha wanafunzi wote waliodahiliwa kujiunga na elimu ya juu wanapata mikopo, bado wengine wameshindwa kunufaika na utaratibu huo na kukatisha ndoto zao.
Hatua hiyo, imeifanya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSO), kubuni namna ya kuanza kusaidia kukabiliana na changamoto ya baadhi ya wanafunzi kukosa ada na hivyo kukwama kudahiliwa ingawa wana sifa za kuendelea na masomo.
Ubunifu huo unahusisha mpango wa hatifungani ili kupata fedha za kuwalipia ada wanafunzi wanaokumbana na changamoto za kukosa ada.
Rais wa Udoso, Jacqueline Humbaro anasema wazo hilo lianzia katika Serikali ya wanafunzi ya mwaka 2024/25,ikiwa ni mpango mkakati wa Serikali ya wanafunzi ulioanzishwa mwaka 2023/24 ambao unakwenda hadi mwaka 2027/28.
“Wizara ya mipango na fedha ya serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, ilipewa nguvu ya kutafuta vyanzo vya mapato, hivyo kuanzia mwaka 2022, viongozi walikuwa na wajibu wa kuacha fedha wanapomaliza muda wao, ”anasema.
Anasema kuanzia mwaka 2022 hadi 2024, serikali za wanafunzi ziliacha fedha zilizofikia Sh100 milioni.
Anasema kwa kutumia fedha hizo, Udoso ilibuni utaratibu wa kuwekeza katika hati fungani katika Benki Kuu (BoT) baada ya kujiridhisha ni uwekezaji salama ambao hauna hasara.
“Ili kuweka utaratibu unaoeleweka na kuufanya kuwa endelevu, tuliandaa kanuni za kuendesha mfuko huo mwaka jana,”anasema rais huyo.

Anasema hoja hiyo pia ilipitishwa na baraza la 90 la chuo na kisha kupitia Benki ya CRDB ambao ni wakala wa BoT, walifanikiwa kuweka hati fungani ya Sh100 milioni kwa kuanzia Desemba mwaka 2024 ambayo itakwenda hadi Mei 22, 2039.
“Kupitia uwekezaji huu Serikali (Udoso) itakuwa ikipokea faida kila mwaka ya Sh15.49 milioni, fedha hizo zitatumika kufadhili wanafunzi wenye uhitaji ambao wanashindwa kufanya usajili kwa kukosa ada,”anasema.
Jacqueline anasema programu hiyo itaanza na wanafunzi watakapokelewa chuoni hapo Oktoba mwaka huu na kuwa maombi ya wanafunzi wanaohitaji ufadhili huo watatakiwa kuanza kuomba kuanzia sasa.
Alipoulizwa kilichowasukuma, Jacqueline anasema katika chuo hicho wamekuwa na changamoto kubwa ya baadhi ya wanafunzi kushindwa kufanya mitihani kwa kukosa ada.
“Unaweza kukuta hana mkopo ama mwingine anao lakini mdogo, kwa hiyo fedha ilikuwa imewekezwa na serikali za nyuma kama tatu hivi zilizoacha fedha,”anasema na kuongeza:
“Kufikia mwaka wetu ilikuwa imefika Sh100 milioni ambayo haikutakiwa kutumika, ukiangalia kwa uhalisia wetu sisi wanafunzi hatuwezi kufanya biashara,”anasema.
Anasema chini ya mfuko huo kila ndaki itakuwa ikitoa mwanafunzi mmoja kwa ajili ya ufadhili ambao wataweza kusomeshwa na mfuko kila mwaka wa masomo.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Udom, Profesa Lugano Kusiluka anasema wanao uzoefu kutoka vyuo vingine kuwa fedha za Serikali za wanafunzi zinatakiwa zitumike na viongozi wakati huo na sehemu nyingine ni lazima ziishe kabla hawajaondoka.
“Na wakati mwingine tumeshuhudia ugomvi kati ya viongozi wa serikali ya wanafunzi dakika za mwisho wakinyang’anyana fedha zilizobaki. Mimi na wenzangu katika menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwanza tulishangazwa lakini tuliunga mkono asilimia 100,”anasema.
Anasema wakati mchakato huo unaendelea hawajawahi kusikia mgongano ndani ya Serikali ya wanafunzi ikimaanisha wote waliona ni wazo jema ambalo lingeacha historia na kuanzisha hamasa kubwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo anasema
Serikali kwa kiasi kikubwa imekuwa ikigharamia elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu.
Hata hivyo, anasema mahitaji ni makubwa mmno ukilinganisha na bajeti inayotengwa, ingawa kila mwaka imekuwa ikiongezeka.
Anasema mwaka wa fedha 2024/25, Serikali ilitoa mkopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na stashahada kwenye fani za sayansi na ufundi , Sh787.4 bilioni ambapo takribani wanafunzi 248,331 walinufaika.