Mtwara. Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Balozi Omari Ramadhani Mapuri, amewataka wasimamizi wa uchaguzi kusoma na kuelewa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kufuata kwa makini maagizo yote yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume.
Amesisitiza kuwa ufanisi na uaminifu katika usimamizi wa uchaguzi unategemea kwa kiasi kikubwa uelewa wa taratibu, sheria na miongozo ya Tume hiyo.
Mapuri ameyasema hayo leo, Julai 15, 2025, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu yanayoanza tarehe 14 hadi 17 Julai kwa Waratibu wa Uchaguzi wa mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo, maofisa Uchaguzi, pamoja na Maafisa Ununuzi 136 kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara.
Amesema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kutambua kuwa uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali ambazo zinapaswa kufuatwa na kuzingatiwa kwa umakini.
Mapuri amesisitiza kuwa uelewa na utekelezaji sahihi wa taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi ulio huru, wa haki na unaoaminika.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpigakura, Giveness Aswile akizunguza na wasimamizi wa uchaguzi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa maofisa hao yanayofanyika mkoani Mtwara
“Wote tunafahamu kama uchaguzi ni mchakato unao jumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kutuatwa na kuzingatiwa na ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri.
“Niwaase msiache kusoma Katiba, sheria, kanuni, taratibu na miongozo. Fuatilieni maagizo mbalimbali yaliyo tolewa na yatakayotolewa na tume na uluzeni mpate kujua kwenye maeneo mtakayopata changamoto mbalimbali yatakayo kuwa na changamoto ili kuwarahisishia katika utendaji wenu,” amesema Mapuri.
Mapuri amewataka wasimamizi hao kushirikisha vyama vyote vya kisiasa vyenye usajili kamili katika hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, kanuni, sheria na maelekezo mbalimbali.
“Jitahidini na mjiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi. Washirikisheni wadau wa uchaguzi katika maeneo mbalimbali hususani sheria kanuni na miongozo iliyotolewa na tuma na wanastahili kushirikishwa,” amesema Mapuri.
Pia, Mapuri amesema wasimamizi hao waende wakafanye utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalumu ya mahitaji husika na kuahakikisha kuna mpangilio mzuri utakaoruhusu kufanyika uchaguzi kwa utulivu na amani.
“Ajira za watendaji wa vituo zizingatie kuwaajiri watendaji wenye uweledi wanaojitambua wazalendo waadilifu na wachapakazi na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawanasifa ya kufanya shughuli za uchaguzi,” amesema Mapuri.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari a Elimu ya Mpiga Kura wa INEC, Giveness Aswile amewaomba waratibu hao walinde nafasi walio ipata kwani bado ni vijana na wanasafari ndefu katika utumishi wa uma.
Aswile ameyasema hayo wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo Balozi Omar Ramadhani Mapuri.
“Niwapongeze kwa kuchaguliwa na Tume kupata nafasi ni jambo moja na kulinda nafasi uliyoipata ni jambo lingine. Wengi wenu ni vijana safari yenu katika utumishi wa umma bado ni ndefu kwa hiyo nategemea kile kilicho kufanya wewe katika kundi kubwa ukachaguliwa utaendelea kukifanya kwa kuwa makini katika kazi unayo kwenda kuifanya.
“Kwa kuzingatia kifungu cha 6 na 8 cha sheria ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani namba 1 ya mwaka 2024 tume katika kikao chake kilichofanyika tarehe 18 na 20 kimeteua na kuridhia waratibu wa usimamizi wa uchaguzi wa mikoa majimbo na kata kusimamia na kuratibu shughuli za uchaguzi,” amesema Aswile.
Aswile amesema kwenye kila mkoa kuna mratibu wa uchaguzi 1 na idadi yao kuwa 26 kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar wana waratibu katika mikoa yote ya Pemba na Unguja.
Mafunzo hayo yalitanguliwa na watendaji hao wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kula kiapo kilicho ongonzwa na Hakimu Allex Kalagaza Robert.