Watu milioni 14 hatarini kufa, kisa kusitishwa misaada ya USAID

Dar es Salaam. Nchi 132 ambazo zilikuwa zikinufaika moja kwa moja na ufadhili kutoka kwa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), ziko hatarini kupoteza jumla ya watu 14 milioni kufikia mwaka 2030 baada ya kufungwa rasmi kwa shirika hilo la kutoa misaada.

Utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la sayansi la Lancet unaeleza kwa kina jinsi hatua zilizopigwa katika miongo miwili iliyopita kupunguza vifo vya watoto na watu wazima,  zinavyoweza kuporomoka kufutia hatua hiyo.

“Makadirio yetu yanaonyesha kuwa, kama hatua za kupunguza ufadhili zilizotangazwa na kutekelezwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025 hazitaondolewa, idadi kubwa ya vifo vinavyoweza kuepukika vinaweza kutokea kufikia mwaka 2030,” wamesema watafiti.

Tofauti na kazi za utafiti za awali ambazo zilijikita tu kwenye athari za moja kwa moja za kiafya, utafiti huu mpya umeangazia pia athari mbadala ambazo pia zinaweza kusababisha vifo na kupoteza njia za kujikimu, na kueleza kuwa pia zinaathiri afya ya watu.

Mipango isiyo ya afya iliyofadhiliwa ni pamoja na misaada ya kifedha, kupunguza umaskini, elimu, na miradi ya maji na usafi wa mazingira.

“Makadirio yetu mara nyingi huwa juu zaidi kwa sababu yanazingatia si tu athari za moja kwa moja za miradi ya afya ya USAID kama tafiti za awali, bali pia athari pana za misaada ya USAID. Athari hizi zinaweza kuwa zimechangia sana katika mafanikio ya shirika hili kupunguza vifo,” wameeleza.

Wanasayansi hao wamesema kati ya mwaka 2000 na 2023, vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vilipungua kutoka 10.1 milioni hadi 4.8 milioni.

Hata hivyo, wanaonya kuwa hatua ya kusitisha msaada wa USAID inaweza kuvuruga mafanikio hayo na kufanya iwe vigumu kufikia Lengo la Maendeleo Endelevu la kupunguza vifo vya watoto hadi chini ya 25 kwa kila watoto 1,000 ifikapo 2030.

Uamuzi wa kufunga USAID ulitangazwa na Waziri wa Masuala ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kupitia hotuba ya maneno 900 iliyopewa jina “Make Foreign Aid Great Again”.

Raia wa Marekani hawapaswi kuendelea kulipa ushuru kusaidia serikali zisizofanya kazi katika mataifa ya mbali.

Utafiti unaonyesha kuwa kati ya 2001 hadi 2021, msaada wa USAID ulisaidia kupunguza malaria na magonjwa yaliyopuuzwa kwa zaidi ya asilimia 50 duniani.

Takwimu zinaonyesha kuwa ufadhili wa USAID ulipunguza vifo vya watoto kwa asilimia 44 na vifo vya watu wote kwa wastani wa asilimia 15.

Jumla ya vifo milioni 91 viliepushwa, ikiwa ni pamoja na vifo milioni 30 vya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.

Watafiti wanatahadharisha kuwa athari ya kukatiza msaada huo ni sawa na janga la kimataifa au vita vikuu,  tofauti yake wanasema  janga hili linaweza kuzuiliwa kwa mabadiliko ya kisera.

Related Posts