WHO yakabidhi vifaa tiba maeneo yaliyoathiriwa na Marburg

Bukoba. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeikabidhi Serikali ya Tanzania msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh112 milioni kwa ajili ya kurejesha hali ya awali ya huduma za kiafya katika maeneo yaliyokumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg.

Mlipuko wa ugonjwa wa Marburg uliotokea Tanzania mkoani Kagera kuanzia Machi 2023 katika Wilaya ya Bukoba, ambapo watu sita walifariki dunia kati ya visa tisa vilivyoripotiwa.

Januari 20, 2025 kupitia tovuti ya Wizara ya Afya ilitagaza mlipuko wa pili katika Wilaya ya Biharamulo ambapo jumla watu 10 walipoteza maisha, kati ya hao wawili walithibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Marburg na wanane wakihesabiwa kama visa vinavyowezekana.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani, Dk Galberth Fadjo amesema shirika hilo limekuwa na jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa namna linavyochukua hatua za haraka juu ya kudhibiti magonjwa yenye nguvu kama Marbug ili kuepuka madhara ya kupoteza watu wengi unapotokea mlipuko ndo maana wametoa msaada huo wa vifaa tiba.

“WHO itaendelea kukabiliana na dharura kwa uharaka katika kupambana na magonjwa ya mlipuko, wito kwa mamlaka kutumia vifaa hivyo kutoa elimu ya kiutaalamu kwa watakaovitumia na kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kupambana na magonjwa ya mlipuko,” amesema Dk Fadjo.

Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa katika Wizara ya Afya, Dk Elias Kwesi amesema  vifaa vilivyopolewa ni vitanda na magodoro yake (20), ndoo (86) pamoja na stendi zake za kunawia mikono, mashine watano za kufulia nguo na Cardiac Monitors (20) kwa ajili ya ufuatiliaji wa matibabu ya wagonjwa na vifa vyote vina thamani Sh112.98 milioni.

“Tunashukuru WHO, hii ni sehemu kurejesha hali ya awali ya huduma za afya katika hospitali ya halmashauri ya Biharamulo na Muleba na ugonjwa huo umetupa funzo ambapo na Wizara ya Afya itaendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kutoa taarifa ya dharura.

“Wanapoona ugonjwa usio wa kawaida, kuimarisha utayari, kushirikisha jamii pamoja na kuunganisha wadau katika kudhibiti mlipuko wa aina yoyote,” amesema Dk Kwesi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Steven Ndaki amewataka wataalamu kuvitunza vifaa hivyo  vilivyotolewa na kuongeza ujuzi wa kuvitumia pamoja na kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo bila kujali kama kuna ugonjwa au hakuna.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Kagera utaendelea kujiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na dharura zote za mlipuko kutokana na mkoa huo kuwa hatarini kwa kupakana na nchi nyingi ambazo zinaongeza mwingiliano wa watu na kuhatarisha magonjwa ya mlipuko.

Related Posts