NYOTA wa Fountain Gate, Wiliam Edgar amesema pamoja na kufanikiwa kuibakisha timu Ligi Kuu, lakini malengo yake hayakutimia akitoa matumaini yake msimu ujao.
Edgar ambaye alikuwa na kiwango bora kikosini hapo akitupia mabao sita, anakumbukwa kwa historia yake ya kuipandisha Mbeya Kwanza kucheza Ligi Kuu Bara 2022-2023 na kinara wa mabao Ligi ya Championship msimu wa 2021/22 akifunga 22.
Katika msimu uliomalizika hivi karibuni, Fountain Gate ambayo ilianza vyema ligi hadi kukaa kileleni kwa muda, ilijikuta ikinusurika kushuka daraja baada ya ushindi wa jumla wa mabao 4-1 dhidi ya Stand United katika play off.
Timu hiyo iliyoweka makazi yake mkoani Manyara, ilimaliza Ligi Kuu nafasi ya 14 kwa pointi 29, ikaanza kucheza play off dhidi ya Tanzania Prisons na kufungwa jumla ya mabao 4-2 kabla ya kuwaondoa Stand United mchujo wa pili.
Akizungumza na Mwanaspoti, staa huyo amesema licha ya kuwa na kiwango bora na kufanikiwa kuibakisha timu Ligi Kuu, lakini hesabu zake hazikwenda sawa kama alivyokuwa amepanga hapo awali.
Amesema idadi ya mabao sita aliyofunga kwa msimu wote, haikuwa hesabu yake kwani alihitaji kuwa miongoni mwa wanaowania kiatu cha ufungaji bora wa ligi, akitoa matumaini msimu ujao kuwa atafanya kweli.
“Kujua kama nitabaki au sitabaki Fountain Gate tuliache, lakini kimsingi nashukuru kwa kumaliza salama msimu na kubaki Ligi Kuu, haikuwa kazi rahisi kwakuwa tulisubiri hadi play off, tulipambana wachezaji, viongozi tukashirikiana na kubaki salama.
“Malengo yangu ilikuwa kupambania nafasi ya mfungaji bora lakini haikuwa bahati yangu, naenda kujipanga msimu ujao kwani lolote linawezekana, nishukuru sapoti ya wachezaji, mashabiki na uongozi tangu mwanzo hadi mwisho,” amesema winga huyo.