Arajiga, Hamdani wateuliwa kuchezesha CHAN 2024

Zikiwa zimesalia siku 17 kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewatangaza rasmi waamuzi watakaochezesha michuano hiyo.

Katika orodha hiyo yenye jumla ya majina 75, Tanzania inawakilishwa na Ahmed Arajiga wa Manyara na Ally Hamdani Saidi kutoka Mtwara.

Tanzania ni nchi itakayoandaa mechi na tukio la ufunguzi wa fainali za CHAN 2024, zitakaofanyika kuanzia Agosti 2 hadi Agosti 30, 2025, huku ikishirikiana na Kenya na Uganda.

Arajiga ni miongoni mwa waamuzi bora ambao wamekuwa wakichezesha mechi nyingi za kimataifa na sasa ameteuliwa kusimamia katikati katika michuano hiyo, huku Hamdani akichaguliwa pia akiwa mwamuzi msaidizi.

Kwa Kenya, mwamuzi wa kati aliyeteuliwa ni Nyagrowa Dickens Mimisa huku msaidizi ni Mwangi Samuel Kuria, wakati upande wa Teknolojia ya Usaidizi wa Video (VAR) aliyeteuliwa ni Stephen Yiembe. Upande wa Uganda, waamuzi wa kati ni Lucky Razake Kasalirwe na Shamirah Nabadda, huku mwamuzi msaidizi ameteuliwa, Ronald Katenya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Tanzania, Nassoro Hamduni alisema ni fahari kubwa kuona tumepata marefa watakaotuwakilisha katika fainali hizo, huku akiwapongeza na kuwataka kujivunia kwa hatua waliyofikia.

“Hii inaonyesha wazi tumepiga hatua kubwa sana kwa sababu wapo waamuzi wengi na wazuri lakini kupata nafasi hiyo kwetu ni mafanikio, shukrani ziende kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kamati yangu pia ya waamuzi,” alisema Hamduni.

Kabla ya michuano hiyo kupangwa kufanyika Agosti, awali CAF ilipanga ichezwe Februari Mosi hadi 28, mwaka huu, lakini ilisogezwa mbele kupisha kukamilika kabisa kwa maandalizi kufuatia ukaguzi uliofanywa kuonesha baadhi ya viwanja vya kuchezea mechi na mazoezi havikuwa tayari.

Lakini kabla ya kusogezwa mbele, Januari mwaka huu CAF ilitangaza waamuzi 65 waliopenya kwenye mchujo na kutangazwa watachezesha fainali hizo ambapo Tanzania ilitoa wawili. Alikuwepo Ahmed Arajiga na Frank Komba ambaye ni mwamuzi msaidizi.

Katika orodha hiyo, Arajiga aliteuliwa katika kundi la waamuzi 26 wa kati, huku Komba akichaguliwa katika kundi la waamuzi 25 wasaidizi. Kundi lingine la VAR hakukuwa na Mtanzania.

Kitendo cha michuano hiyo kusogezwa mbele, CAF ikaendesha semina ya pili ya maandalizi ya CHAN iliyofanyika Cairo nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi 25, 2025 ambapo waamuzi watatu kutoka Tanzania, Ahmed Arajiga, Frank Komba na Hamdani Said waliteuliwa kushiriki.

Semina hiyo ndiyo ilikuwa ya mwisho kabla ya CAF kutaja majina ya waamuzi watakaochezesha michuano ya CHAN wakiwemo Watanzania wawili, Arajiga na Said, huku Komba akikosekana.

Katika orodha ya CAF yenye majina ya watu 75, waamuzi wa kati ni 26, waamuzi wasaidizi 26 na wakufunzi 5, huku upande wa VAR kukiwa na waamuzi 18.

Morocco ndiyo nchi iliyotoa watu wengi kwenye orodha hiyo ambao ni saba, ikifuatiwa na Algeria (6), kisha Cameroon (4), huku wenyeji Tanzania ikiwa na wawili, wakati Kenya na Uganda zina watu wao watatu kila moja.

Fainali hizo za CHAN 2024 zitashirikisha timu za taifa kutoka nchi 19, ufunguzi wake ni Agosti 2, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ikiikutanisha Tanzania dhidi ya Burkina Faso.

Mbali na mechi ya ufunguzi, CAF imepanga fainali itachezwa kwenye Uwanja wa Kasarani nchini Kenya, Agosti 30 na ile mechi ya kuwania mshindi wa tatu itachezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Uganda, Agosti 29.

Kundi A mechi zake zitachezwa kwenye Uwanja wa Kasarani, zikishirikisha Kenya, Morocco, Angola, DR Congo na Zambia, huku kundi B zikichezwa Dar es Salaam, zikiundwa na Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Mechi za kundi C ambazo zitachezwa Uganda, zitashirikisha Uganda, Niger, Guinea, Afrika Kusini na Algeria, huku kundi D ambalo mechi zake zitapigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, litashirikisha Senegal, Congo, Sudan na Nigeria.

Mashindano ya CHAN 2024 yatafuatiwa na ya AFCON 2027, ambapo Tanzania, Uganda na Kenya zitakuwa wenyeji.

Waamuzi wa kati ni Ahmed Arajiga (Tanzania), Adissa Abdoul Raphiou Ligali (Benin), Messie Jessie Oved Nvoulou (Congo), Kpan Clement Franklin (Ivory Coast), Malala Kabanga Yannick (DR Congo), Ahmed Nagy Mosa Mahmoud (Misri), Tsegay Teklu Mogos (Eritrea), Jammeh Lamin (Gambia), Nyagrowa Dickens Mimisa (Kenya), Ahmed Abdulrazg (Libya), Diakhate Ousmane (Mali), Milazare Patrice (Mauritius), Loutfi Bekouassa (Algeria), Diouf Adalbert (Senegal), Jelly Alfred Chavani (Afrika Kusini), Aklesso Gnama (Togo), Melki Mehrez (Tunisia), Lucky Razake Kasalirwe (Uganda), Vincent Kabore (Burkina Faso), Brahamou Sadou Ali (Niger), Brighton Chimene (Zimbabwe), Mefire Abdou Abdel (Cameroon), Bouchra Karboubi (Morocco), Shamirah Nabadda (Uganda), Kech Chaf Mustapha (Morocco) na Houssam Benyahya (Algeria).

Waamuzi wasaidizi ni Ally Hamdani Said (Tanzania), Ngila Guilain Bongele (DR Congo), Lucky Kegalogetswe (Botswana), Sanou Habib Judicael Oumar (Burkina Faso), Emery Niyongabo (Burundi), Rodrigue Menye Mpele (Cameroon), Amaldine Soulaimane (Comoros), Alao Salim (Benin), Fasika Biru Yehualashet (Ethiopia), Jawo Abdul Aziz (Gambia), Addy Roland Nii Dodoo (Ghana), Mwangi Samuel Kuria (Kenya), Joel Wonka Doe (Liberia), Nassiri Hamza (Morocco), Yacouba Abdoul Aziz (Niger), Dieudonne Mutuyimana (Rwanda), Omer Hamid Mohammed Ahmed (Sudan), Wael Hanachi (Tunisia), Ronald Katenya (Uganda), Eleyeh Robleh (Djibouti), Ettien Eba Medard (Ivory Coast), Abeigne Ndong Amos (Gabon), Sirak Samuel (Eritrea), Malondi Chany (Congo), Adel Abane (Algeria) na Diana Chikotesha (Zambia).

Kwa upande wa wakufunzi kuna Mohammed Guezzaz (Morocco), Janny Sikazwe (Zambia), Evarist Menkouande (Cameroon), Mohamed Houssein Ali (Djibouti) na Boubaker Hannachi (Tunisia).

Katika VAR, kuna Mahmoud Ashour (Misri), Dahane Beida (Mauritania), Lahlou Benbraham (Algeria), Bamlak Tessema Weyesa (Ethiopia), Samir Guezzaz (Morocco), Hamza El Fariq (Morocco), Issa Sy (Senegal), Atcho Prierre Ghislain (Gabon), Daniel Lareya (Ghana), Abongile Tom (Afrika Kusini), Yasir Abdalaziz (Sudan), Viana Letticia (Eswatini), Maria Rivet (Mauritius), Akhona Zennith Makalima (Afrika Kusini), Jermoumi Fatiha (Morocco), Ghorbal Mustapha (Algeria), Stephen Yiembe (Kenya) na Atezambong Fomo Carine (Cameroon).