Dar es Salaam. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Askofu Josephat Gwajima amesema yeye ataendelea kuwa mwanachama wa chama hicho na wala hana mpango wa kukihama.
Askofu Gwajima ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (CCM) anayemaliza muda wake, amesema hayo leo Jumatano, Julai 16, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali. Hata hivyo Gwajima hakuelezea kuhusu hatua yake kutochukua fomu kugombea ubunge Jimbo la Kawe katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huuu.
Pamoja na mambo mengi aliyozungumza, Gwajima ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima amesema licha ya ushauri anaoutoa kutowapendeza wengi juu ya masuala mbalimbali, hana mpango wa kuhama.
“Mimi bado ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi na nitaendelea kuwepo,” amesema.
Kiongozi huyo wa kiroho amesema mara nyingi watu wasiopenda mema ukizungumza jambo la kusahihisha ama kuweka sawa: “Wanasema aaaa!! Anataka kuhama CCM, mimi bado nipo CCM, tutabanana humuhumu ndani mpaka paka paeleweke kukae vizuri. CCM ni chama cha demokrasia, kama yalivyo madhumuni yake,” amesema Askofu Gwajima