Atisa Dipankar, ni mwanazuoni wa kiroho mwenye imani ya Budhha na ana asili ya Bengal aliyeishi kuanzia muongo wa tisa, Karne ya 10 hadi muongo wa sita, Karne ya 11.
Katika uhai wake, Atisa alilizunguka Bara la Asia akifundisha falsafa za maisha na jicho la ndani juu ya mwonekano.
Moja ya nukuu za Atisa ilisema: “Hekima kuu inaona kupitia mwonekano.” “The greatest wisdom is seeing through appearances.”
Nitaitumia wakati wa kukamilisha uchambuzi wangu kuhusu barua ya Humphrey Polepole ya kujiuzulu ubalozi wa Cuba na utumishi wa umma.
Polepole amemwandikia barua hiyo Rais Samia Suluhu Hassan akimweleza sababu za yeye kujiuzulu utumishi wa umma na kujivua ubalozi kuwa anajitenga na uongozi uliopo, ambao ameulalamikia kwa kutoheshimu watu, wala kusimamia haki za watu. Polepole amesema pia uongozi wa sasa haujikiti katika kutatua kero za watu.
Ukiisoma barua ya Polepole kwa mtindo wa kati ya mstari, utauona mzizi wa malalamiko ni uamuzi wa Mkutano Mkuu CCM, kumpitisha Rais Samia kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Hoja hii ipo dhahiri aya ya tano ya barua ya Polepole. Katika aya hiyo ameandika: “Matukio ya hivi karibuni ya wazi ya kukiuka misingi, utamaduni na desturi za Chama cha Mapinduzi (CCM), hususan katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya Chama, ambao kwa kila awamu huwa msingi wa kukihuisha Chama na fursa ya kufanya mageuzi, ambayo kwa pamoja hukipa Chama sura ng’aavu mbele ya umma kabla ya uchaguzi.
“Desturi hii ya kufanya mageuzi ndani ya Chama, imekuwa nguzo muhimu ya ushindi wa CCM mbele ya umma. Imekuwepo kauli maarufu ya CCM, isemayo ‘Chama kwanza mtu baadaye’, mwanzoni mwa mwaka huu, nilipoona kauli hii inafanyika vinginevyo, nimejiuliza mara kadhaa, ni masilahi ya nani yanapiganiwa wakati huu, mtu, kikundi, au Chama taasisi?” Mwisho wa kunukuu.
Januari 19, 2025, Mkutano Mkuu CCM, ulimpitisha Rais Samia kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Polepole anapolalamikia kukiukwa misingi ya uteuzi wa wagombea, halafu moja kwa moja, anaelekeza ukosoaji wake kwa maneno “mwanzoni mwa mwaka”, hapo hakuna ubishi, kwamba analenga kilichofanyika Januari 19, Dodoma.
Katiba ya CCM, imefungua dirisha kwa wanachama wenye sifa, kila baada ya miaka mitano au nyakati za uchaguzi mdogo, kujitokeza kuwania nafasi za uongozi, ambazo hushindaniwa kulingana na kalenda ya Tume ya Uchaguzi.
Dirisha hilo huwa mwanzo wa mchakato wa uchukuaji fomu, ujazaji na kurejesha, kisha hufuata hatua za mchujo hadi uteuzi wa wagombea. Upande wa urais, kuna utamaduni ambao CCM inaishi nao, yaani Rais aliye madarakani anapowania muhula wa pili, huachwa achukue fomu peke yake na huvuka hatua zote za uteuzi.
Utamaduni wa kumwachia Rais aliye madarakani kuwania muhula wa pili bila kupingwa ndani ya CCM, umekuwa ukikutana na changamoto za hapa na pale.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2010, aliyekuwa kada wa CCM, John Shibuda ambaye alikuwa mbunge wakati huo, alitangaza angechukua fomu dhidi ya Rais aliyekuwa madarakani, Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, Shibuda baadaye alitangaza kujitoa. Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020, aliyekuwa kada wa CCM, Bernard Membe ambaye alipata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, aliweka wazi kusudi lake la kuchukua fomu CCM ili kuchuana na Rais aliyekuwa madarakani, Dk John Magufuli. Membe alifukuzwa uanachama CCM kabla ya mchakato kuanza.
Historia hiyo inaonesha kuwa endapo dirisha lingeachwa wazi kwa wana-CCM kuruhusiwa kuchukua fomu ya kuomba uteuzi kuwa mgombea urais kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, kisha wangechukua na kuvuka hatua ya mchujo, Samia angekuwa Rais wa kwanza aliye madarakani kupata upinzani ndani ya CCM. Kurejea kwenye mada, ni kweli uamuzi wa Mkutano Mkuu CCM, Januari 19, ulikuwa nje ya utamaduni wa CCM ambao upo kwenye Katiba ya chama hicho.
Swali la kujiuliza ni je, kwa kutokufuatwa utamaduni huo, Katiba imevunjwa? Tuchakate hoja kuzunguka swali hilo.
Katiba ya CCM, ibara ya 100 (2), inaeleza: “Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, utakuwa ndicho kikao kikuu cha CCM kupita vyote na ndicho kitakachokuwa na madaraka ya mwisho katika kutoa uamuzi wa aina yoyote ile.”
Tafsiri iliyo wazi hapo ni kwamba, Katiba imeweka wazi mchakato wa kumpata mgombea urais CCM. Kamati Kuu imepewa kipande chake, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), nayo ina nafasi yake.
Katiba hiyo hiyo, imetoa mamlaka makubwa kwa Mkutano Mkuu CCM Taifa. Kwamba, uamuzi ambao utafanywa na Mkutano Mkuu CCM Taifa, utakuwa wa juu kabisa na hakuna mtu, watu au chombo kingine chochote ndani ya chama, kinachoweza kupinga au kubatilisha kile ambacho kimeamuliwa na mkutano huo.
Bila shaka, kwa kutambua mamlaka yao kikatiba, wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa, Januari 19, 2025, waliamua kuchukua njia ya mkato kwa kumpitisha Rais Samia kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kisha Dk
Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais Zanzibar. Na baadaye, Samia alimteua Dk Emmanuel Nchimbi, kuwa mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tuendelee na Katiba ya CCM, ibara ya 101 (7), inaeleza: “Mkutano Mkuu wa CCM Taifa unaweza kukasimu madaraka yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kuhusu utekelezaji wa kazi zake kwa kadiri inavyoona inafaa, isipokuwa kwa kazi zifuatazo; kutunga au kubadili Katiba, kuchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, uteuzi wa wagombea urais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.”
Ukishaelewa ibara hiyo, moja kwa moja unakuwa na ufahamu kwamba uteuzi wa wagombea urais kupitia CCM, ni mamlaka ya Mkutano Mkuu Taifa. NEC na Kamati Kuu, hukasimu hatua za mwanzo, hadi yatakapopatikana majina yasiyozidi matatu. Mchakato ukishafika hapo, kumpata mgombea urais, Mkutano Mkuu umedhibitiwa kikatiba, kuruhusu mkutano mwingine wowote kuteua, isipokuwa wenyewe tu.
Polepole ni mwanachama wa CCM, alishawahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, mjumbe wa Sekretarieti ya CCM na mjumbe wa Kamati Kuu. Anaijua vizuri Katiba ya CCM.
Kipindi akiwa katikati ya mfumo wa Chama, hakuna wakati wowote aliguswa kuona Katiba imeupa Mkutano Mkuu Taifa mamlaka makubwa. Kila kitu alikiona kipo sawa.
Sanasana, namkumbuka Polepole aliyekuwa katikati ya mfumo wa CCM, alivyokuwa anaongoza kwa matamko. Mara kufuta uanachama wa wanachama waandamizi, kama Sophia Simba na wengine.
Kutambia magari ya kifahari CCM, injini ya V8 (vieite), kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao vya CCM, hasa NEC na Mkutano Mkuu. Hakuguswa na mamlaka makubwa ya Mkutano Mkuu.
Tupime mamlaka ya maadili (moral authority) ni misingi ya ukweli, uadilifu, uaminifu na nidhamu ya kimantiki.
Unapojitokeza kukemea jambo, sharti upimwe kama una mamlaka ya maadili katika suala husika. Mla rushwa, hawezi kuwa na mamlaka ya maadili ya kukemea rushwa.
Polepole kupitia barua yake ya kujivua ubalozi, amezungumzia ukiukwaji wa utamaduni na desturi za uteuzi wa wagombea ndani ya chama cahake cha CCM.
Lakini alipokuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, ndipo yalitokea mafuriko ya wabunge na madiwani wa kutoka vyama vya upinzani, kuhamia CCM. Halafu, wahamiaji walipewa upendeleo wa kugombea nafasi walizokuwa nazo kupitia CCM bila kupingwa.
Wana-CCM waliojaribu kuchukua fomu kupambana na wahamiaji, walidhibitiwa. Membe aliweka wazi nia yake ya kuchukua fomu CCM ili kuchuana na Magufuli kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, matokeo yake, Membe alifukuzwa uanachama.
Kingine, washindi wengi wa mchakato wa uteuzi ngazi za majimbo, waliondolewa. Wapo ambao hawakufika japo tatu bora, lakini ndiyo walipewa tiketi ya kusimama kwenye majimbo. Polepole alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, hakukemea, aliona sawa.
Ufafanuzi huo, uje kwenye swali hili; baada ya ukimya wake kipindi akiwa katikati ya kitovu cha uamuzi CCM, nyakati ambazo rafu za kikatiba zilichezwa waziwazi, je, sasa hivi Polepole anapoibuka na kukemea mchakato wa uteuzi wa wagombea CCM, anayo mamlaka ya maadili?
Aya ya nne ya barua ya Polepole, anakosoa kwamba uongozi wa sasa hausimamii haki za watu. Vema kukumbusha, Polepole alipokuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, matukio mengi yenye kusigina waziwazi haki za binadamu yalitendeka.
Bila kupuuza hoja zake, na kwa kutambua kweli matukio ya utekaji yanaendelea, swali la kujiuliza, Polepole anapoibuka leo na kukosoa ukiukwaji wa haki za watu, anayo mamlaka ya maadili?
Je, anayolalamikia sasa, kama angeendelea kuwa katikati ya kitovu cha mfumo wa uongozi, angejiuzulu? Maswali ni mengi na magumu, nyuma ya uamuzi wa Polepole kujivua ubalozi na utumishi wa umma, kwa sababu ambazo amezitaja.
Sehemu ya hitimisho la barua yake, Polepole amesema atabaki kuwa mwanachama mtiifu wa CCM. Chama ni Katiba.
Msingi wa uamuzi wake upo dhahiri kwamba alikwazwa na uteuzi wa Rais Samia kuwa mgombea urais mapema. Ikiwa Mkutano Mkuu CCM Taifa, ulitumia mamlaka yake ya kikatiba, maana yake Polepole anachukizwa na Katiba ya CCM.
Anakuwa vipi mtiifu kwa chama ambacho Katiba yake hakubaliani nayo?
Baada ya Polepole kuondolewa kwenye cheo cha Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, alianzisha harakati za kimtandao, kuusema uongozi wa Rais Samia na wasaidizi wake, akitumia programu aliyoiita “Shule ya Uongozi” Kisha, Rais Samia alimteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi. Je, baada ya kujivua ubalozi, anarudi na harakati zipi?
Kuna msomaji wa makala zangu gazetini aliniuliza kwa ujumbe mfupi wa maneno: “Kwani Polepole alikuwa na mpango gani kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, mpaka achukizwe na uteuzi wa Rais Samia kuwa mgombea urais wa CCM mapema, kabla ya kalenda ya chama iliyozoeleka?”
Swali hilo, kwa namna fulani, linakaribisha nadharia kwamba Polepole harudi Tanzania kutulia, bali yapo mapambano anataka kuyaelekea. Hivi karibuni alinukuliwa akitumia maneno ya Kispaniola (Cuban Spanish) “Hasta la victoria simpre”, akatafsiri kuwa “mpaka ushindi utakakapopatikana mapambano yanaendelea.”
Alitamba kuendelea kupambana na aliowaita wahuni kwenye mfumo wa uongozi.
Je, hayo ni matamshi ya anayerudi kupumzika na kuwa mwanachama mtiifu wa CCM? Sasa, hitimisho liwe kwenye nukuu ya Atisa kuwa hekima kuu inaona kupitia mwonekano. Maneno ya Polepole kupitia barua yake, ukiyatafsiri kupitia mwonekano wake tangu alipovuliwa
Ukatibu wa Itikadi na Uenezi CCM na vita yake kwamba anapambana na wahuni, utapata jawabu kuwa yupo vitani.
Je, anaingia vitani kama jeshi la mtu mmoja au analo kundi kubwa? Muda utaleta majibu.
Humphrey Polepole alizaliwa mwaka 1970, katika Mkoa wa Tabora, Kaskazini magharibi mwa Tanzania. Safari yake ya elimu ilianzia Shule ya Msingi Mbuyuni, kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Azania, jijini Dar es Salaam na baadaye Benjamin Mkapa Sekondari. Aliendelea na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alikochukua Shahada ya Sayansi ya Jamii, akijikita zaidi katika masuala ya maendeleo, siasa na uongozi.
Hapo ndipo mbegu za uanaharakati na upambanaji wa fikra zilipoanza kuchanua kwa kasi.
Polepole alianza kazi kwa kujitolea kwenye asasi mbalimbali za kiraia, huku akionyesha ukali wa hoja na uzalendo katika majukwaa ya mijadala. Umahiri wake ulimtambulisha hadi Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete akamteua kuwa mmoja wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2012, chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba. Alikuwepo katika mchakato huo muhimu, akiibua hoja zenye mashiko kuhusu haki za vijana, usawa wa kijinsia na uwajibikaji wa serikali kwa wananchi. Mwaka 2015, Rais John Magufuli alimwamini na kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma. Desemba 2016, Polepole aliteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Mwaka 2020, aliteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na alipata nafasi ya kuiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa. Mwaka 2022 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi, kisha baadaye akahamishiwa Cuba mwaka 2023.
Akiwa Cuba, Polepole alikuwa Balozi wa Tanzania lakini pia akiwakilisha nchi katika mataifa ya Venezuela, Colombia na Guyana.Alibaki kuwa mwakilishi wa taifa hadi Jumapili Julai 13, 2025, alipotangaza kujiuzulu kwa hiari nafasi ya ubalozi.