ALIYEKUWA beki wa KMC, Raheem Shomari amesaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Ghazl El-Mehalla ya Misri.
Akizungumza na Mwanaspoti, beki huyo alisema tayari ameungana na timu hiyo na anaendelea na maandalizi ya msimu mpya ambao unatarajiwa kuanza wiki mbili zijazo.
“Ni kweli nimemalizana na timu hiyo na tayari nipo kambini tunaendelea na maandalizi ya msimu ujao ambao utaanza mapema tofauti na nilivyokuwa natarajia maana nilikuja huku kwaajili ya kusaini mkataba sikujua kama ligi itaanza mapema,” alisema na kuongeza;
“Nimezuiliwa kurudi huko, nipo kambini naambiwa hii nchi ina mashindano mengi hivyo ligi inaanza mapema ntarudi nchini Desemba ndio kunakuwa na mapumziko.”
Akizungumzia mchakato wa kufanikisha dili hilo alisema haikuwa rahisi kutokana na kufanya majaribio kabla ya kusaini.
“Sijasajiliwa kwa kutazamwa kwenye mechi za Ligi Kuu nikiwa na KMC nimepata hii nafasi baada ya kufanya majaribio nafurahi mambo yameenda vizuri naahidi kupambana ili niweze kufikia malengo.”
Shomari amesajiliwa akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na waajiri wake wa zamani KMC amejiunga na timu hiyo ambayo aliwahi kuitumikia kiungo Himid Mao.