Bunge la Afrika Mashariki lahitimisha vikao vyake kwa viporo

Arusha. Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) limehitimisha vikao maalumu vya mtandaoni, lakini halikufanikisha kumaliza majadiliano ya hoja zilizopangwa kujadiliwa.

Vikao hivyo vilivyoanza mwezi uliopita vilijikita katika mambo mbalimbali, hoja kubwa ilikuwa kujadili na kupitisha bajeti ya Jumuiya kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Hoja hiyo ilifanikiwa baada ya kupendekeza, kujadili na kuidhinisha bajeti ya jumla ya dola za Marekani 109,047,861 kwa mwaka huo.

Mbali na hilo, pia vikao vilipitisha bajeti mbili za nyongeza kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Ikumbukwe kuwa uamuzi wa kufanya vikao hivyo kwa njia ya mtandao, tofauti na miaka mingine ambapo wabunge hukutana ana kwa ana, ulitokana na ukata wa kifedha unaoikabili taasisi hiyo muhimu.

Zaidi ya kuidhinisha bajeti, wabunge wa EALA walijadili ripoti mbalimbali za kamati zinazohusu masuala nyeti ya kikanda kama vile usalama, kilimo cha ikolojia, ujumuishaji wa mifumo ya malipo ya kikanda na kampeni dhidi ya ukeketaji wa wanawake (FGM).

Hata hivyo, hadi Spika wa EALA, Joseph Ntakirutimana, alipoahirisha Bunge hilo jana, hoja kadhaa bado hazikufanikisha kujadiliwa wala kufikia mwafaka.

Miongoni mwa masuala yaliyosalia ni hoja ya kutaka Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitisha na kurefusha mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wa muda mfupi.

Vilevile, Muswada wa kuanzisha Ofisi ya Takwimu ya EAC wa mwaka 2018 pamoja na Muswada wa Viwango, Uidhinishaji na Tathmini ya Ulinganifu wa mwaka 2023, pia yaliahirishwa.

Ajenda nyingine iliyosubiriwa kwa hamu ni ripoti ya Kamati ya Sheria, Kanuni na Haki kuhusu tuhuma dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa EAC, Dk Peter Mathuki, ambayo nayo iliahirishwa.

Hata hivyo, Spika wa EALA, Ntakirutimana amesema kuwa suala hilo linangojea mashauriano zaidi na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC kabla ya ripoti hiyo kusomwa rasmi.

Aidha, Dk Peter Mathuki, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Februari 27, 2021 na wakuu wa nchi wanachama wa EAC, ndiye mtu wa kwanza kuondolewa kwenye wadhifa huo kabla ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitano.

Dk Mathuki alifukuzwa kazi Machi 2024 kufuatia tuhuma nzito za ukiukaji wa maadili na usimamizi mbovu wa madaraka. Baadaye, aliteuliwa na Rais wa Kenya, William Ruto, kuwa Balozi wa Kenya nchini Urusi.

Uchunguzi uliofanywa na Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) ulionyesha kuwa mwenendo wa Dk Mathuki ulisababisha Jumuiya kupoteza zaidi ya dola milioni sita za Kimarekani.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Kanuni na Haki ya EAC, Mashaka Ngole, amedai kuwa tuhuma nyingine dhidi ya Dk Mathuki ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za usalama, uuzaji wa mali za Jumuiya bila idhini, ikiwemo magari, ajira na uhamisho wa wafanyakazi kinyume cha utaratibu, kuajiri walinzi bila kufuata taratibu sahihi, pamoja na kuendesha akaunti za fedha nje ya mifumo iliyokubaliwa na kuidhinishwa.

Katika hotuba yake ya kufunga vikao, Spika wa EALA, Joseph Ntakirutimana, aliwapongeza wabunge kwa kujitolea na bidii yao, hasa katika kupitisha bajeti ya EAC licha ya changamoto za vikao vya mtandaoni.

Hata hivyo, alitoa tahadhari kuhusu kutegemea vikao vya mtandao kwa wingi siku za usoni bila kuwepo kwa dharura halisi.

“Ni matumaini yetu kwamba wadau wote sasa wanaelewa changamoto zinazohusiana na mfumo huu. Hatupaswi kuufanya kuwa kawaida, isipokuwa kwa mazingira maalumu pekee,” amesema.

Related Posts