KATIKA kutoa hamasa kwa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda ameahidi kutoa tiketi 1,000 na mabasi matano ya kusafirisha mashabiki kutoka mkoani hapa kwenda Dar es Salaam kuishangilia timu hiyo.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano ya CHAN kwa kushirikiana na Uganda na Kenya ambayo yatafanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30, mwaka huu. Katika michuano hiyo, Agosti 2 Taifa Stars itacheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Burkina Faso kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mtanda ametoa hadi hiyo jana Jumanne Julai 15, 2025 wakati akizungumza na wadau wa michezo mkoani Mwanza, mashabiki na wanachama wa Simba na Yanga jijini hapa kuhusu maendeleo ya sekta ya michezo.
Amesema uamuzi huo ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya michezo, kutoa hamasa na kuwa wazalendo kwa timu ya taifa, huku akitoa wito kwa Wana Mwanza kutumia fursa hiyo kwenda kuishangilia Taifa Stars.
“Nitatoa kwa chama cha soka (MZFA) tiketi 1,000 kwa wale watakaotaka kwenda Dar es Salaam kuishangilia timu ya taifa, wao watagharamika tu chakula na malazi,” amesema Mtanda.
Ameongeza kuwa, atatoa mabasi matatu huku Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba akitoa mabasi mawili na kufanya jumla kuwa matano ambayo yatawapeleka mashabiki Dar es Salaam na kuwarudisha Mwanza.
“Wadau wa soka wa Mkoa wa Mwanza tuhamasishe mashabiki kwenda Dar es Salaam kuishangilia timu yetu ya taifa ambayo ni kielelezo na nembo ya utaifa wetu, lazima tujivunie timu yetu kwahiyo tutajaza mafuta mashabiki waende na kurudi wakafurahie mpira wa miguu,” amesema Mtanda na kuongeza.
“Sisi wana Mwanza tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kuiunga mkono timu yetu ya taifa. Kazi yenu nyinyi (viongozi wa matawi) ni kuwaandaa mashabiki na kuwahamasisha kwenda jijini Dar es Salaam.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, amesema: “Kama alivyosema Mkuu wa Mkoa, mabasi yatakuwepo, tutaweka bendera zetu kwenda kuisapoti timu ya taifa, na tunaomba mikoa mingine iige Mwanza katika kuunga mkono timu zetu za taifa.”
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Khalid Bitebo, amempongeza Mtanda kwa hatua hiyo ya kuwaunganisha wadau na mashabiki mkoani humo jambo linalotoa faraja na matumaini kuelekea msimu ujao.
Shabiki wa soka jijini Mwanza, Richard Watanda amempongeza Mtanda kwa hatua hiyo huku akiahidi kuhamasisha wenzake kuchangamkia tiketi hizo kwani imekuwa utamaduni wao kuhudhuria mechi za timu ya taifa na klabu zinapochezwa jijini Dar es Salaam.
“Kwa niaba ya tawi letu sisi tutakuwa bega kwa bega na klabu zote zinazoshiriki ligi, tutaandaa kila kitu kilicho ndani ya uwezo wetu, tutashirikiana kutoa sapoti,” amesema Watanda.