UONGOZI wa Dodoma Jiji, unaendelea na maboresho ya kikosi na umeanza mchakato wa kuongeza mikataba mipya kwa wachezaji waliomaliza, ikianza na beki wa kati wa timu hiyo, Mtanzania Abdi Banda.
Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho Januari 15, 2025, akitokea Baroka FC ya Afrika Kusini, alisaini mkataba wa miezi sita na sasa umemalizika rasmi, hivyo uongozi kuanza mazungumzo ya kumpa mwingine ikiwa watakubaliana masilahi binafsi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema wakati wanaendelea na maboresho pia ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao, wanafanya mazungumzo ya kuongezea wachezaji wengine ambao mikataba yao imeisha.
“Iddi Kipagwile na Yassin Mgaza walikuwa wamemaliza mikataba lakini tumewaongezea mingine zaidi ya kuendelea kukichezea kikosi chetu, tunaendelea na wengine na tukikubaliana kuhusu masilahi tutawaongezea akiwemo Banda,” alisema Fortunatus.
Fortunatus alisema licha ya maboresho ya timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao, ila hawataki kubomoa zaidi kikosi hicho na kusababisha kuanza upya kukitengeneza, hivyo watabaki na wachezaji muhimu na kuwapa mkono wa kwaheri watakaoshindwana.
Banda aliyewahi kucheza timu mbalimbali zikiwezo za Coastal Union, Simba na Mtibwa Sugar za Tanzania, Highlands Park, Chippa United na Richards Bay zote za Afrika Kusini, amekuwa muhimili wa kikosi hicho katika muda mchache aliokichezea.
Msimu huu wa 2024-2025, Banda alitengeneza pacha nzuri na beki mwenzake, Mukrim Issa ‘Miranda’ aliyesajiliwa kwa mkopo akitokea Singida Black Stars na walikiwezesha kikosi hicho cha Dodoma Jiji kumaliza nafasi ya 12 na pointi zake 34.
Mbali na kushughulikia suala la usajili, pia uongozi wa Dodoma Jiji umetoa mapendekezo ya kikosi hicho kitakapoweka kambi na huenda ikajichimbia kwenye visiwa vya Zanzibar au jijini Arusha.
Uamuzi wa kuchagua mojawapo kati ya maeneo hayo mawili unatokana na dhamira ya uongozi wa klabu hiyo kuweka mazingira bora ya kuijenga timu upya baada ya msimu uliopita kuwa na changamoto na Dodoma Jiji inalenga kuwa miongoni mwa timu zitakazoleta ushindani mkali msimu ujao, huku ikisaka mafanikio makubwa zaidi kwenye mashindano yote ya ndani itakayoshiriki ambayo ni Ligi Kuu na Kombe la FA.
Fortunatus alisema: “Tunapanga kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya Arusha au Zanzibar, maeneo yote haya yana mazingira bora yatakayochangia maandalizi mazuri ya kikosi chetu msimu mpya wa ligi.”
Msimu uliomalizika 20240-2025, Dodoma Jiji ilimaliza ligi nafasi ya 12, moja kutoka kwenye mstari wa kucheza play off ya kuepuka kushuka daraja ikiwa na pointi 34 baadaa ya kucheza mechi 30.
Timu hiyo tayari imetangaza kuwabakisha Idd Kipagwile na Daudi Milandu ambao wameongezewa mikataba kuelekea msimu ujao.