Morogoro. Ekari 614 za mashamba ya bangi, kilogramu 3,741.9 za bangi kavu na kilogramu 1,706 za mbegu za bangi zimeteketezwa katika ushoroba ulio kati ya Hifadhi za Taifa za Mikumi na Nyerere.
Kuteketezwa kwa mashamba hayo, bangi na mbegu hizo ni matokeo ya operesheni iliyofanyika kwa siku tisa mkoani Morogoro kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma ambayo imetolewa leo Julai 16, 2025 na DCEA imesema operesheni hiyo iliyowahusisha pia wananchi imewezesha kuvunjwa kwa kambi 72 za wakulima wa bangi na kukamatwa kwa watuhumiwa tisa wanaohusishwa na zao hilo haramu.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amesema kuwa operesheni hiyo ni sehemu ya mapambano endelevu dhidi ya dawa za kulevya nchini, hususan katika maeneo yanayozunguka hifadhi za taifa.
Amesema maeneo hayo yameanza kuwa maficho ya wahalifu wakiyatumia kulima zao hilo haramu ambalo huishia kuleta athari kubwa kwenye jamii.
Kufuatia hilo kamishna Lyimo amesema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti maeneo yote yanayotumika kwa kilimo cha bangi.

“Operesheni hii imeonesha mafanikio makubwa. Mashamba ya bangi yamepungua ikilinganishwa na awali na wakulima wa bangi wameendelea kusogea mbali zaidi na hivyo kuonesha kwamba operesheni tunazofanya zinaleta mafanikio chanya.” amesema na kuongeza
“Tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kujenga uelewa juu ya madhara ya dawa za kulevya hususan bangi, hatuwezi kuruhusu dawa za kulevya ziendelea kuharibu jamii yetu. Tunawaomba wananchi wote waendelee kushirikiana nasi kwa kutoa taarifa ili kuhakikisha tunamaliza kabisa tatizo hili.”
Kwa upande wake Kamanda Mkuu Msaidizi Kikosi Tanapa Moses Oko Onyango amesema ya kupata taarifa kuhusu kuwepo kwa mashamba makubwa la bangi katika eneo la Nyarutanga, karibu na mipaka ya Hifadhi za Nyerere na Mikumi, waliona ni vema kushiriki kwenye uteketezaji huo.
“Tanapa inalinda uhifadhi endelevu wa maliasili, hatutakubali watu kutumia maeneo ya hifadhi kwa shughuli haramu. Kwa kushirikiana na DCEA tutaongeza nguvu ya kudhibiti uhalifu kwenye ushoroba ikiwa ni pamoja na kufanya doria katika maeneo yote yanayozunguka hifadhi,” amesema Onyango.