FYATU MFYATUZI: Kwanini tusiite kaya Chaitan au Tanghasia?

Juzi, katika kupitapita mitaani kutoa tongotongo, si nikachekwa kiasi cha kudhani naanza kuchizika. Kwanza, kituko kilianzia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole pale Addis.

Baada ya kutua kama kawa, hutoa tongotongo. Hivyo, nilikwenda kwenye ofisi za shirika la njiwa la Ethiopia lenye watumishi wa hovyo sina mfano. Mstuko ndo usipime.

Nikiwa nimejipanga mstarini tayari kusikilizwa, niliomba msaada kwa abiria mwengine aliyekuwa mbele yangu ambaye ni mmakonde kama mimi. Ukiachia yeye na wengine wachache, abiria tarajiwa wa njiwa hiyo waliobakia walikuwa wachainizi!

Nilimuuliza jamaa kama kuna njiwa mbili moja ya kuja Ufyatuni na nyingine ya kwenda Chaina. Jamaa alishangaa. badala ya kujibu swali, naye aliniuliza swali.

Si unajua tena mafyatu. Badala ya fyatu kujibu swali langu, naye aliswalika swali. Alisema “kwani wewe unelekea wapi?” Nilimjibu kuwa nilikuwa natia timu kaya. Badala ya kunipa jibu aliuliza tena “kwani tatizo lako nini? Baada ya kuona hivyo, nikanywea na kuamua kujiondokea nikangoja wakati ukifika wa njiwa wangu kupaa nitangoja mtangazaji anijuze ni ipi.

Baada ya kusota muda mrefu na muda wa kupaa kuwadia, nilienda tena kwenye geti la kupandia. Kwa mara nyingine, nilikuta wachaina kibao.

Hivyo, ilibidi nimuulize mfanyakazi mmojawapo kama njiwa iliyokuwa inaondoka ilikuwa inaelekea Chaina au Ufyatuni.

Akiwa ameshangaa kidogo, alijibu kuwa ilikuwa inaelekea Ufyatuni na si Chaina. Du! Nilianza kuskuti lau nipate jibu nisipate.

Basi, Fyatu nilifyata nikingoja pipa litue nione yaliyokuwa yakinisibu kuhusiana na hawa wachaina. Kutua, tu, nikasikia wengine wakitema uswa japo wakichainachaina.

Nilichukua ndinga yangu kuzama zangu Utashani kwa wenzangu. We bwana! Kufika, si nikakuta hata apartments za kupangisha baadhi yake zinamilkiwa na wachaina. Kabla mstuko kuniisha si nikasikia mmoja akipita akisema ‘nauja ice cream!” “Du” nilijisemea “utadhani niko zangu Uchainani na si Ufyatuni!”

Baada ya hapo, maswali lukuki yalianza kunishambulia. Hivi huu ndiyo uwekezaji au uchukuaji kama siyo exportation of jobless army from Chaina au ugenishaji?”

Nisameheni kwa kitasha. Maana, siku hizi hata Kiswahili naongea kwa taabu sana kiasi cha kuandika haya madude kwa msaada wa mshikaji wangu Siri.

Hayo tuyaache. Kwa kuzingatia haya, kwanini Ufyatuni isiitwe Chaitan?

Mbali na kuitwa Chaitan, maybe, chai tamu, lipo hili sekeseke na timbwili kama siyo mtiti wa haya jamaa zangu waendesha baiskili za umeme au Toyo.

Da! Hawa jamaa walinikanganya hadi nikaongopa hata kuendesha ndinga yangu kwa wanavyoonyesha umahiri wa kuvunja na kuvuruga sheria za barabarani. Kwanza, nilijiuliza kifyatufyatu. Inakuwaje mafyatu wazima wenye akili timamu kama siyo kuchizika, na nguvu wafanye vitu ambavyo kwa kisambaa huitwa suicidal? Je ni kuchizika, ukosefu wa akili timamu (UAT), ukosefu wa ubunifu au kujichoka na kuchoka kuishi? Pili, ni kwanini wahusika hawaoni denja wanayocheza nayo?

 Tatu, inakuwajekuwaje wanene hawaoni balaa hili ambalo naona ni kama bomu linalotika likingoja kuitafuna kaya?

Nne, kwanini hawaoni uchafuzi wa mazingira mbali na uwezekano wa kutengeneza kizazi au taifa la viwete kutokana na uvunjaji wa sheria na uendeshaji wa ovyo na hatarishi wa toyo unavyosababisha vifo vya waendeshaji na abiria?

Tano, imekuwaje tumejichoka na kuruhusu ghasia kuwa ndiyo mfumo wetu wa maisha kama mafyatu?

Kusema ukweli, sikuamini kuwa fyatu mwenye akili timamu ana anayetaka kuishi angeweza kupanda haya majeneza yasiyofunikwa yaitwayo toyo. Sikuamini kuwa kidude kinachopaswa kubeba mafyatu wawili tena wakiwa, kisheria, wanapaswa kuvaa helmet kwa usalama wao, kingeweza kupakizwa mafyatu watatu na wakati mwingine wanne.

Funga kazi ni pale niliposhuhudia abiria wakipanda haya madude ya kifo bila kuvaa helmets. Je, hapa tatizo ni wahusika au mfumo mzima usiofuata maadili wala sheria bali madili na shari? Kwa mujibu wa hali na jinai, kwanini Ufyatuni isiitwe Tanghasia?

Jambo la tatu ambalo ningepata nilidurusu japo kwa ufupi ni upigaji wa kizwazwa na wa kutisha, au tuseme wizi wa kimfumo.

Mwajua kuwa juzi llikuwa Saba Saba? Siendi kwenye historia yake na kuzaliwa kwa chata la TANU.

Katika kutoa tongotongo, si nikatinga nikiwa na lengo la kwenda kuwafaidi waanimo hasa lion. Kama kawa, nilificha njuluku na rukono yangu bila kusahau wallet yangu ili wale washenzi wasinisachi na kusepa.

Kwa vile ni bonge la mjanja, njuluku niliweka sehemu nyeti na kusepa. Kufika tu, huo msongamano usipime. Katika kusukuti, si nilikuta kuwa ni wa kutengenezwa ili wahusika wapate kuuza hata tiketi feki na kusepa? Nani alilistukia hili? Hili halikunihangaisha kwa vile ulaji na madili ni sehemu ya mfumo wa Danganyika na Zaa inzi, we koma.

Nilitaka kushambuliwa na presha pale nilipolipia tikiti ya kuingilia na kuishia kulipishwa tena kuwaona waanimo?

Je huu siyo uanimo kunipiga kuwaona waanimo wakati nshalipia kuingia ku-enjoy kila kitu? Kumbe nina jet lag inayochizisha akili?

Related Posts