Heshima, maisha ya Rais mstaafu Buhari akizikwa kaburi kaiwada

Daura, Nigeria. Katika jiji la Daura, jimbo la Katsina mamia kwa maelfu ya waombolezaji wamejumuika kutoa heshima za mwisho kwa Rais wa zamani wa Nigeria, Hayati Muhammadu Buhari aliyefariki dunia Julai 13 jijini London akiwa na umri wa miaka 82, miezi sita na siku 26.

Mwili wa marehemu uliwasili nchini Nigeria Jumapili iliyopita kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Umaru Musa Yar’adua, ukisafirishwa kwa ndege ya Kijeshi ya Nigeria FGT 001.

Makamu wa Rais Kashim Shettima na Kiongozi wa Wafanyakazi wa Rais, Femi Gbajabiamila waliongoza msafara wa kumleta nyumbani.


Mjane wa marehemu, Aisha Buhari, pamoja na wanafamilia wengine walikuwa sehemu ya msafara huo.

Mamia ya watu walikusanyika uwanjani kupokea jeneza lililofunikwa kwa bendera ya taifa. Rais Bola Tinubu, akiwa ameambatana na viongozi wa kitaifa na kimataifa, akiwamo Rais wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo na Waziri Mkuu wa Niger, Ali Lamine Zeine, waliongoza mapokezi hayo ya heshima.

Baada ya kuwasili, jeneza lilipelekwa Daura kwa msafara wa saa moja, ambapo dua maalumu ya maziko ilifanyika katika uwanja wa PMB Helicopter, ikiongozwa na Sheikh Alhaji Salisu Rabiu, Imamu Mkuu wa Daura.

Mkusanyiko huo ulikuwa wa kihistoria, ukihudhuriwa na viongozi wa serikali kuu, magavana wa majimbo mbalimbali, viongozi wa mabunge yote mawili, familia, marafiki, wafanyabiashara wakubwa na maelfu ya wananchi waliokuwa wamefurika kila kona ya Daura.


Miongoni mwa waliohudhuria walikuwa Rais wa zamani wa Niger, Mahamadou Issoufou; Makamu wa Rais wa zamani Yemi Osinbajo; Makamu wa Rais wa zamani Atiku Abubakar; na viongozi wa zamani wa majimbo akiwemo Nasir El-Rufai (Kaduna), Yahaya Bello (Kogi), Aminu Waziri Tambuwal (Sokoto), na Ali Modu Sheriff (Borno).

Kutoka sekta binafsi, walikuwapo Alhaji Aliko Dangote, Alhaji Sayyu Dantata na Alhaji Dahiru Barau Mangal.

Wakati jeneza likiteremshwa kaburini saa 11:50 jioni, majonzi yalitawala kwa watu wengi waliokuwapo.

Gavana wa Katsina, Dikko Radda, alionekana akibubujikwa na machozi huku akifarijiwa na viongozi wenzake.

Makamu wa Rais Shettima na mtoto wa marehemu, Yusuf Buhari walishiriki katika kuulaza mwili wa baba yao kaburini.

Jeshi la Nigeria liliongoza heshima za mwisho kwa kupiga mizinga 21 ya heshima kabla ya kuzikwa.


Timu ya maofisa wa jeshi wakiongozwa na Meja Jenerali. Mike Alechenu waliendesha taratibu hizo kwa uangalifu mkubwa, wakisindikiza jeneza katika matembezi ya heshima hadi mahali pa mapumziko ya milele.

Katika hali ya unyenyekevu mkubwa, kaburi la Buhari halikutofautiana na lile la raia wa kawaida.

Mwili wake umezikwa ukiwa umefunikwa kwa sanda nyeupe, ndani ya kaburi la kawaida lililowekwa mbao, mkeka na kufukiwa kwa udongo.

Katika dua za pamoja, maombi yalielekezwa kwa Mwenyezi Mungu ili amsamehe marehemu madhambi yake na amjalie pepo ya ‘Firdaus’.


Maombi pia yaliombwa kwa ajili ya faraja kwa mjane wake Aisha, watoto, wajukuu, watu wa Daura na taifa zima la Nigeria.

Taarifa kutoka kwa Alhaji Mamman Daura, mmoja wa wanafamilia wa karibu na rafiki wa marehemu, zilieleza kuwa alikuwa pamoja na Buhari Jumamosi kabla ya umauti kumkuta Jumapili saa 10:30 jioni.

“Alikuwa katika hali nzuri, tulizungumza, tukacheka. Alikuwa na matumaini makubwa ya kurudi nyumbani wiki hiyo. Lakini hali ilibadilika ghafla Jumapili mchana ambapo alianza kupata shida ya kupumua na madaktari walishindwa kuokoa maisha yake,” alisema Daura alipoongea na gazeti ThisDay la Nigeria.

Wakati huo huo, wananchi wa Daura waliomfahamu marehemu kwa karibu walimkumbuka kama mtu mwenye heshima, anayejali watu wake na asiyejisifu kwa matendo yake ya huruma.

Wengi walielezea misaada aliyokuwa akiitoa kimyakimya ikiwamo kugharamia karo za wanafunzi, matibabu na kugawa chakula kwa wajane na yatima wakati wa Ramadhani na Sikukuu.


Aminu Daura, mzee wa mtaa, alisema: “Watu wengi walikula kwa sababu ya msaada wake, lakini hakuwahi kutangaza.”

Abdullahi Sani, mlemavu aliyepata baiskeli ya miguu mitatu kutoka Taasisi ya Buhari mwaka 2021, alilia na kusema, “Leo naweza kuzunguka na kulisha familia yangu kwa sababu ya Baba Buhari.”

Hajiya Fatima Yahaya naye alisema: “Buhari aliendelea kutukumbuka hata baada ya kutoka madarakani.”

Msisitizo juu ya ucha Mungu wa marehemu ulielezwa na Malam Ashiru Yusuf, ambaye alisema marehemu hakuwa akikosa sala za jamaa alipokuwa Daura.

“Wakati wowote tulipomtembelea na wakati wa sala ukifika, kikao kingesimamishwa ili kuswali,” alisema.

Kwa upande wa kimataifa, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, ambaye aliwahi kuhudumu chini ya utawala wa Buhari kama Waziri wa Mazingira, alitembelea Ofisi ya Nigeria jijini New York na kuandika salamu za rambirambi.

Akizungumza na The Guardian, la Nigeria, amesema: “Buhari alikuwa kiongozi mwenye nidhamu isiyotetereka, imani ya kweli na uzalendo wa dhati. Urithi wake utadumu zaidi ya mipaka ya Nigeria.”

Hatimaye, leo Jumatano, dua ya Fidau imefanyika kwa mujibu wa taratibu za Kiislamu, ikiwa ni ya siku ya tatu tangu kufariki kwake dunia, Qur’an Tukufu imesomwa na dua maalumu zikatolewa kwa ajili ya roho ya marehemu, na baraka kwa waliobaki.

Tukio hilo liliwavutia viongozi wa dini, ndugu wa marehemu na maelfu ya waumini kutoka sehemu mbalimbali.