Klabu ya FAR Rabat imemalizana na beki wake Henock Inonga ‘Varane’ baada ya msimu mmoja ndani ya timu hiyo.
Inonga aliyetambulishwa ndani ya FAR Rabat Julai 13, 2024, amesitishiwa mkataba, kutokana na ripoti ya kocha Mreno Alexander Santos.
Beki huyo wa zamani wa Simba, hakuwa na maisha mazuri ndani ya timu hiyo, akianza kwenye mechi tano pekee msimu huu, zikiwemo nne za Ligi na Moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Inonga amekuwa akisotea benchi ndani ya FAR Rabat huku mechi nyingi akiwa anakaa jukwaani ingawa marakadhaa alikuwa akihusishwa na Yanga ambao hatahivyo inaonekana wengi wamemkataa.
Mapema Santos alionyesha hakubaliani na uwezo wake, ambapo aliwajulisha mabosi wa timu hiyo ya jeshi la Mfalme, kuachana na beki huyo Januari,2025.
Inonga ameachwa sambamba na nyota wengine wanne wakiwemo, Hicham Boussefiane,El Hassan Houbeib,Et-Tayeb Boukheriss na Larbi Naji.
Beki huyo Mkongomani aliwahi kutajwa kupigiwa hesabu na Yanga wakati ikisaka beki wa kati lakini habari za ndani zinasema kuwa nafasi yake ni finyu.