Jaji Kazi: Tume itahakikisha inaendesha uchaguzi wa huru na haki

Unguja. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi, amesema kuwa ufunguzi wa jengo jipya la Tume hiyo umeondoa changamoto kubwa kwa wafanyakazi, ambao kwa muda mrefu walitekeleza majukumu yao katika mazingira yasiyokuwa rafiki.

Jaji Kazi amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kunatimiza kiu ya muda mrefu ya watumishi wa Tume na kunatarajiwa kuboresha ufanisi wa kazi pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema, jengo hilo ni kielelezo cha ZEC kuwapatia wananchi huduma bora kwa sababu licha ya kuwa na majukumu makubwa bado Tume hiyo haikuwa na jengo linaloendana hadhi ya yake.

Jaji kazi ameyasema hayo leo Jumatano Julai 16, 2025 wakati wa ufunguzi wa jengo jipya la Ofisi Kuu ya ZEC lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.


“Tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1962, tume hii imekuwa ikiendesha majukumu yake katika ofisi ambazo sio rafiki kulingana na mahitaji yake na ililazimika kutumia majengo ya kukodi hasa katika kipindi cha uchaguzi Mkuu kwa shughuli za habari, uangalizi na kutangaza matokeo,” amesema Jaji Kazi.

Mbali na hayo, Jaji Kazi amesema Tume inaendelea kujipanga na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ikiwemo kuendesha uchaguzi huo kwa uhuru na haki na wenye kuzingatia sheria na kuhakikisha kila mwananchi anaitumia haki yake ya msingi kwa kujitokeza kwa wingi.

Pia, amesema, jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuchapisha machapisho yote yanayohusiana na Tume hiyo, pia alitoa wito kwa baadhi ya Tasisi ya Serikali kuchapisha hapo ili kuwa chanzo cha mapato.

Kwa upande wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alikiri kuwa jengo hilo lilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwa Rume hiyo kupatiwa ofisi zenye hadhi na viwango stahiki hivyo amefurahia kuona Serikali imetimiza ahadi hiyo ya ujenzi wa wenye mazingira mazuri yanayoendana na hadhi ya Tume.

Pia, Dk Mwinyi amesema ufunguzi wa jengo hilo ni hatua moja wapo ya kukuza demokrasia kiziwani humo kwani litatumika katika kuwarahisishia wananchi kupata huduma bora, za uhakika, kwa wakati na kuzingatia vigezo vyote vinavyohitajika katika masuala ya kiuchaguzi kutokana na miundombinu yake.

“Binafsi nilipata nafasi ya kukagua baadhi ya sehemu ya jengo hili, nimeridhika sana na hali ya mazingira niliyoyaona kwa kushuhudia Ofisi za kisasa za watendaji, studio ya kisasa ya Redio na Televisheni, Ghala kubwa la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi pamoja na chumba maalumu cha kuhifadhia vifaa nyeti,” amesema Dk Mwinyi.

Hivyo, Dk Mwinyi amesema amejiridhisha kuwa changamoto ya muda mrefu iliyokuwa ikiikabili Tume kuhama na kukodi ukumbi kwa ajili ya matokeo nje ya Ofisi, itakuwa imepatiwa ufumbuzi.

Dk Mwinyi ameipongeza ZEC kwa kuendelea vyema na matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa hatua mbali mbali.

Akitoa ripoti ya mradi huo, Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina amesema mradi huo umeandaliwa kwa lengo la kuiwezesha Tume hiyo kutoa huduma zake kwa ufanisi zaidi.

Amesema, jengo hilo lina ghorofa nne lenye ulinzi na usalama wa taarifa za wananchi pamoja na Tume hiyo ikiwemo ulinzi wa vifaa vya uchaguzi.

Amefafanua kuwa, jengo hilo lilianza kujengwa Januari, 2024 na lilitakiwa kujengwa kwa miezo tisa hadi kufikia Oktoba, 2024 hivyo kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza haikufanikiwa na walichukua hatua ya kuwangezea muda lakini ilishindana.

“Baada ya kuona mkandarasi wa mwanzo kushindwa kukamilisha mradi huo alitozwa Sh1.9 billioni baada ya ucheleweshaji wa uliojitokeza hapo awali,” amesema Faina.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Thabiti Idarous Faina (kulia) akimuonyesha jambo Rais wa  Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi wakati akikagua jengo la Tume alipolinzindua leo



Mkurgenzi Faina amesema mradi huo umeghairimu Sh14.1 billioni na hadi kufikia sasa Sh10.7 billioni zimeshalipwa kwa awamu nane kwa mujibu wa mkataba.

Amefafanua kuwa, Kampuni ya CRJE imefanikiwa kukamilisha ujenzi huo baada ya kusuasua kutoka kwa mkandarasi wa awali.

 Naye, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema pamoja na changamoto zote zilizojitokeza bado kampuni hiyo inapaswa kupewa pongezi kwa kazi kubwa walioifanya.

Amesema, miradi yote inayoendelea kwa sasa nchini inazingatia nidhamu ya fedha za matumizi ya majengo hayo hivyo ofisi hiyo itaendelea kusimamia miradi yote.


Katika hatua nyingine Chama cha ACT-Wazalendo kimesema hakijaridhishwa na hatua ya Rais Mwinyi kualikwa kuwa mgeni rasmi kuzindua jengo hilo Ilhali pamoja na kuwa kiongozi wa nchi lakini ni miongoni mwa wagombea urais ambao wanatarajiwa kupigiwa kura.

“Sisi ACT hatujaridhishwa na hatua hii, inaleta ukakasi kidogo kwani huyu ni miongoni mwa wagombea sasa kuzindua jengo tena katika wakati huu wa mchakato wa uchaguzi haioneshi usawa,” amesema Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo Salim Bimani.

Related Posts