JKU Academy na Luxury FC, zimetembeza vichapo kwa wapinzani wao katika mechi za jana Jumanne Julai 15, 2025 ikiwa ni mwendelezo wa mashindano ya Yamle Yamle Cup yanayofanyika kisiwani hapa huku yakichezwa Uwanja wa Mao A na B, Mjini Unguja.
Katika mchezo uliochezwa jana Jumanne Julai 15, 2025, saa 10 jioni, JKU Academy iliichapa Mambosasa kwa kuifunga mabao 4-0 ambapo Khalfan Ali alianza kucheka na nyavu dakika ya 25 akifuatiwa na Omar Kombo dakika ya 44 na 52, huku Suleiman Mbarouk akikamilisha bao la nne dakika ya 60.
Mchezo mwingine uliopigwa Mao A wakati huohuo, timu ya Al Qaeda imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Miembeni City, ambapo bao hilo lilifungwa na mchezaji Suweid Juma dakika ya 28.
Mashabiki wa Al Qaeda walifika uwanjani kwa mwonekano wa kipekee ambapo wanaume walivaa kanzu nyeupe na vilemba huku upande wa wanawake wakivaa baibui na nikabu.
Mzunguko wa kwanza wa Kundi B umemalizika huku msimamo ukionesha nafasi ya kwanza inashikiliwa na JKU Academy, inafuatiwa na Al Qaeda, Miembeni City na Mambosasa inashika nafasi ya nne.
Kwa upande wa mechi za Kundi D zilizochezwa jana saa 12:30 jioni, Timu ya Mwembe Makumbi FC imetoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Melinne City, huku bao hilo likifungwa na Mudrik Gonda dakika ya 25.
Mchezo huo uliokuwa wa jasho na damu katika dakika 90, timu zote zilionekana kuwa na hamu ya kutoka na pointi tatu ambazo zimechukuliwa na Mwembe Makumbi.
Katika hatua nyingine, Luxury FC imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kinazini, Mchezaji Haji Juma alisafisha njia kwa kuweka bao la kwanza dakika ya 17 wakati Harun Khamis akiweka la pili dakika ya 60 na tatu likikamilishwa na Sagaf Abdulrahman dakika ya 70.
Baada ya kukamilika kwa mechi hizo za Kundi D, msimamo unaonesha Luxury FC inashikilia nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Mwembe Makumbi, Melinne ya tatu na Kinazini ikishika ya nne.
Mashindano hayo yataendelea leo jioni ikizikutanisha timu za kundi E ambapo Welezo City itapambana na Real Nine FC huku Kipunguni FC ikivaana na Wadachi, wakati kundi F ni Mazombi FC vs Magari ya Mchanga FC na BG FC vs P/Mchangani.