Dar es Salaam. Kilio cha muda mrefu cha madereva wa magari na bajaji waliounganisha mifumo ya gesi kwenye vyombo vyao vya moto, cha kukesha vituoni kusubiri nishati hiyo, kimepata ufumbuzi.
Ufumbuzi huo umeanza kuonekana kutokana na ongezeko la vituo vya kujaza gesi kwenye magari na bajaji, hali iliyoleta unafuu wa huduma kwa watumiaji.
Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), idadi ya vituo imeongezeka hadi saba kutoka vitatu vilivyokuwepo kwa muda mrefu.
Vituo hivyo saba sasa vimeleta unafuu kwa watumiaji wa gesi kwenye vyombo vya moto, cha kwanza kipo Uwanja wa Ndege, Tazara, TOT–Tabata vituo viwili, Ubungo na barabara ya Sam Nujoma vituo viwili.
Richard Kimaro, dereva wa teksi mtandao, anasema mwanzoni mwa mwaka huu na miaka ya nyuma alilazimika kukaa saa tatu hadi tano kusubiri kujaziwa gesi kwenye gari.
“Vituo vilikuwa vichache, ukikuta foleni Tazara, unalazimika kwenda Ubungo Maziwa ambako foleni ilikuwa kubwa zaidi. Nilikuwa napoteza mapato, unapata mteja unamruhusu atafute dereva mwingine kwa kuwa bado sijapata huduma ya gesi,” anasema.
Hali ilivyo sasa, Kimaro anasema anatumia dakika mbili au tano kujaza gesi kwenye gari lake na kuendelea na kazi yake.
Kimaro anasema idadi ya vituo ni vingi na ni mara chache kukuta magari kwenye foleni, hivyo muda wa kujaza nishati hiyo hauzidi dakika tano.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Emanuel Ishengoma, dereva wa teksi mtandao, anayesema awali alikuwa akipoteza saa saba kusubiri kujaza gesi kwenye gari lake.
Ishengoma anasema hali hiyo ilisababisha kupata walau safari mbili kwa siku na kupoteza asilimia 75 ya mapato aliyopaswa kuipata kama angefanya kazi kwa siku nzima.
“Sasa nafanya kazi siku nzima, kama nitakwenda kujaza gesi ni dakika mbili tu ndiyo natumia na kipato naingiza kuanzia asubuhi hadi jioni, sina muda ambao utapotea,” anasema.
Juma Rajabu, dereva wa bajaji jijini Dar es Salaam, anasema, “Kwa sasa sihitaji tena kusubiri kwa saa tatu au nne kama ilivyokuwa awali, vituo vimeongezeka na huduma ni ya haraka zaidi.”
Rajabu anasema maendeleo hayo yanachochea hamasa kwa madereva wengine kuhamia mfumo wa gesi, ambao una gharama nafuu na rafiki kwa mazingira ikilinganishwa na mafuta ya petroli au dizeli.
“Ongezeko la vituo vya kujaza gesi si tu limeleta unafuu kwa watumiaji, bali lina mchango mkubwa katika kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza usalama wa matumizi ya nishati hiyo kwa vyombo vya moto,” anasema.
Dereva mwingine wa bajaji na mkazi wa Mbagala, Cosmas Jacob, anasema anatumia dakika mbili pekee kujaza gesi.
“Kipindi cha nyuma nilikuwa nalala kituoni ili nipate gesi. Kwa sasa natumia muda mfupi. Ombi langu kwa Serikali, maeneo kama Mbagala na kwingineko ambako kuna vituo vya mafuta, vijengwe vingi zaidi ili tusitembee umbali mrefu kufuata huduma,” anasema.
Mkuu wa Idara ya Uhandisi Mitambo Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Dk Esebi Nyari, anasema ongezeko la vituo vya kujaza gesi kwenye magari lina faida.
Faida anayoitaja ni hamasa watakayopata madereva kuendelea kubadili mifumo yao kuhamia kwenye matumizi ya gesi.
“Changamoto ilikuwa vituo vya kujaza gesi kuwa vichache, sasa vimeongezeka, hakuna foleni. Jitihada hizi sasa zinapaswa kuendana na hamasa ya watu kubadili mifumo ya vyombo vyao vya moto,” anasema.
Dk Nyari anasema ni muhimu kuendelea kuhamasisha watu kubadili mifumo ya magari yao ili wawekezaji wanaojitokeza kujenga vituo waone uwepo wa soko la uhakika.
Anasema kipindi ambacho kulikuwa na changamoto ya uhaba wa vituo, hamasa ya watu kubadili mifumo ya magari yao ilikuwa ndogo, sasa wameanza kurejea.
“Tuendelee kuhamasisha watu kubadili mifumo ya magari yao. Bajaji sasa hivi si wengi kwa sababu kuna bajaji zinaingizwa ambazo tayari zimefungwa mitungi ya gesi.
Kwa mwezi tunapata magari 15 hadi 20 ambazo zina uhitaji wa kufungiwa mitungi ya gesi,” anasema.
Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi, Oscar Mkude, anasema ongezeko la vituo vya kujaza gesi kwenye vyombo vya moto ni mwitikio mzuri wa uwekezaji na una manufaa kwa Taifa.
“Ipo haja ya kutumia rasilimali zetu badala ya kuagiza mafuta kwa wingi kwa kutumia dola. Tukitumia CNG zaidi na kuokoa hata asilimia 50 ya fedha za kigeni kwenye uagizaji wa mafuta, ni hatua muhimu kwa kuchagiza uchumi wa ndani,” anasema.
Mkude anasema wingi wa vituo vya kujaza gesi kwenye vyombo vya moto utasaidia ustahimilivu wa bei, kwani gharama ya CNG haitakuwa inabadilika mara kwa mara kwa sababu ya masuala ya kisiasa duniani.
“Bila shaka tutaanza kuona watu wakivutwa kuagiza magari yenye mfumo wa CNG au kuboresha zaidi uwezo wa kuhuisha magari ya petroli/dizeli kwenda CNG,” anasema.
Mchumi Mwandamizi wa TPDC, Alex Nduye, anasema kituo kikuu cha kujaza gesi cha TPDC barabara ya Sam Nujoma kimepunguza foleni ya magari yaliyokuwa yakitumia muda mrefu kupata nishati hiyo.
“Kituo hicho kina uwezo wa kuhudumia magari 1,200 hadi 1,500 kwa siku. Niwaambie wawekezaji kuwa eneo la gesi kuwekeza ni fursa.
Tayari Serikali imeagiza mabasi 755 ya mwendokasi ambayo yatatumia gesi asilia, na mabasi haya yatajaza kwenye vituo vya gesi,” amesema.
Aprili mwaka huu, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kupitia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati ya 2025/2026, vibali 10 vimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya CNG.
Ukiwa ni utekelezaji wa ujenzi wa vituo hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi TPDC, Emmanuel Gilbert, anasema kampuni saba zinaendelea na ujenzi wa vituo nane vya gesi kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Gilbert anasema baadhi ya vituo hivyo ujenzi umeanza na matarajio ni kufikia Disemba mwaka huu vyote vianze kufanya kazi.
Anasema vituo vipya ambavyo ujenzi unaendelea ni vya Kampuni ya Mafuta ya Puma – vitatu katika maeneo ya Ubungo External, Tegeta na Tangi Bovu.
Vituo vingine vinajengwa na Kampuni ya Energo Tanzania (barabara ya Coca Cola), Kampuni ya BQ (Barabara ya Goba), Kampuni ya Tan Health (Mbezi Beach), Kampuni ya TAQA Dalbit (Barabara ya Bagamoyo).
Kingine kitajengwa Kigamboni, Kibada na Kampuni ya Anric Energy, huku Kampuni ya NAT Energy nayo ikijenga kituo Tabata. Pia Kampuni ya Victoria itajenga eneo la Kipawa.
“Katika kuongeza wigo wa utoaji huduma, tumeagiza vituo hamishika sita vya gesi vyenye thamani ya Sh8.5 bilioni. Hapa tupo kwenye hatua za kusaini mkataba; tukisaini,” anasema.
Gharama na matumizi yalivyo
Kwa magari yanayotumia gesi, TPDC inasema yapo 5,000 na bajaji ni zaidi ya 5,000.
Kwa eneo la gharama, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) inaonesha matumizi ya gesi asilia huokoa gharama kwa zaidi ya asilimia 50 ya gharama mtu anazotumia kwenye dizeli na petroli.
Kwa mfano, mtungi wa kilo 15 wa CNG hujazwa kwa Sh23,000 na hutembea wastani wa kilomita 250 kwa gari aina ya Toyota IST, ambazo zingegharimu wastani wa Sh80,000 kwa mafuta.
Mtaalamu wa uunganishaji wa ubadilishaji wa mifumo ya gari kutoka mafuta kutumia gesi, Satary Juma, anasema mtungi wa gesi wa kilo 11 huwafungia madereva kwa gharama ya Sh1.8 milioni na mtungi wa kilo 15 hufungwa kwa Sh2.15 milioni.