BAADA ya Simba Queens kumpa mkono wa kwaheri kipa Gelwa Yona, inaelezwa Mashujaa Queens ipo kwenye hatua nzuri ya kumalizana naye.
Gelwa alijiunga na Simba msimu wa 2021/22 akitokea Ruvuma Queens na misimu miwili ya mwanzoni alionyesha kiwango bora. Hata hivyo, baada ya kuongezwa kwa kipa Carolyne Rufaa, Gelwa aliishia kukaa benchi.
Chanzo cha kuaminika kililiambia Mwanaspoti kipa huyo huenda akaibukia Mashujaa Queens, ambayo imetuma ofa ya kumhitaji kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.
“Ni kipa mzuri na Kocha Ally Ally amependekeza awepo. Kama unavyojua, amekuwa muda mrefu akifundisha soka la wanawake, kwa hiyo amepewa jukumu la usajili. Nafikiri Gelwa anaweza kuibukia huko,” kilisema chanzo hicho.
Ikumbukwe Mashujaa huenda ikamkosa kipa wake namba moja, Asha Mrisho, anayedaiwa kujiunga na JKT Queens, hivyo Gelwa anatazamwa kama mbadala wake.
Kama Mashujaa itafanikisha dili la kipa huyo, basi timu hiyo itafikisha nyota watatu kutoka Simba kujiunga nayo baada ya Koku Kipanga na Zainabu Dudu kusajiliwa msimu uliopita.