Kisa gharama, Pamba nusura iuzwe ipigwe bei

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amesema wanakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za uendeshaji wa timu ya Pamba Jiji jambo ambalo lilisababisha msimu ulioisha watake kuiuza baada ya kutofanya vizuri.

Kibamba alitoa kauli hiyo juzi jijini hapa katika mkutano na wadau wa michezo ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, huku akisisitiza kuwa gharama hizo wakati mwingine ni mzigo mkubwa kwa halmashauri hiyo.

“Kuendesha hii timu siyo mchezo, nilishaanza kutema bungo lakini Mkuu wa Mkoa akanikomalia kuibeba, sasa mkubwa akishasema hakuna namna lazima mambo yaende lakini acheni masihara kumiliki timu siyo mchezo,” alisema Kibamba.

Alisema wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuweka viingilio vya chini Sh500 na Sh1,000 ili mashabiki wajae uwanjani na kusaidia kupata mapato lakini mambo yamekuwa kinyume chake kwa mashabiki kutojitokeza viwanjani.

“Kama kweli wana Mwanza tunaipenda Pamba tujae uwanjani, kama tungekuwa wengi tunajaza ule uwanja (CCM Kirumba) mashabiki 30,000 tungekuwa tunaipunguzia mzigo halmashauri katika kuendesha timu,” alisema mkurugenzi huyo.

Kwa upande wa RC wa Mwanza, Said Mtanda ambaye ni mlezi wa timu hiyo alisema baada ya Pamba Jiji kufanya vibaya mwanzoni mwa msimu halmashauri ya jiji la Mwanza ilimuomba waiuze lakini akagoma.

“Kazi ya mpira ni kazi ya uwenda wazimu kweli inataka ile hamasa kwa sababu mpira unamaliza pesa ndiyo maaana watu wanaokuwa waraibu wa mpira ni ambao wanakubali kufilisika kwa sababu ya mpira,” alisema Mtanda na kuongeza;

 “Kama na sisi wengine tungeamua kukaa pembeni tungeshuka mapema kabisa. Zimetengenezwa jezi hazifiki hata pisi 5,000 hakuna wanaoununua, kwahiyo mmemuachia timu mwenyekiti (Bhiku Kotecha) anapata presha.”

Mtanda aliwataka wafanyabiashara na matajiri mbalimbali katika jiji hilo kuziunga mkono timu za Mwanza kwa kuzipa udhamini hata wa kusaidia kusafirisha timu, huku akiwaomba mashabiki kuzisapoti kwa kwenda viwanjani na kununua jezi.

“Kuendesha timu ndugu zangu siyo jambo jepesi ninawaomba tuzisadie hizi timu kama tunataka kuwa wakweli wafanyabiashara wenye kampuni mbalimbali kwanini msielekeze udhamini mdogo tu wa kawaida kwenye hizi timu.”

Related Posts