Kishapu yapiga hatua utoaji chakula shuleni

Kishapu. Lishe bora kwa wanafunzi imeendelea kuimarika wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, huku idadi ya shule zinazotoa chakula ikipanda kutoka asilimia 90.5 katika robo ya tatu hadi asilimia 97.6 kwenye robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Ofisa Lishe wa Wilaya ya Kishapu, Hadija Nchakwi amesema leo Jumatano Julai 16, 2025, kuwa mafanikio hayo ni ishara ya juhudi kubwa za kuboresha lishe shuleni, hatua inayolenga kupunguza utoro na kuongeza ufaulu.

Akizungumza kwenye kikao maalumu cha tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha Aprili hadi Juni kilichofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Nchakwi amesema;

“Kuna shule 168 za msingi na sekondari wilayani hapa. Katika robo ya tatu shule 152, sawa na asilimia 90.5, zilikuwa zinatoa chakula. Robo ya nne tumefikia asilimia 97.62.”

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe ya wilaya ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Tano Malele amewataka watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo masuala ya lishe shuleni.

“Suala la lishe si jambo la pembeni. Serikali imelipa kipaumbele kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni. Robo ijayo hatutaki kusikia kuna shule haina uji au chakula cha mchana kwa wanafunzi wa sekondari,” amesisitiza Malele.

Pia amehimiza viongozi kuwa mfano bora kwa jamii kwa kuhamasisha uchangiaji wa chakula na kuwataka wasimamizi wa chakula shuleni kuwa waaminifu na kuwajibika.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala ametoa wito kwa wadau kuendelea kushirikiana na serikali katika kutoa elimu ya lishe kwa jamii ili kumaliza tatizo la udumavu miongoni mwa watoto.

“Tunaomba wadau waendelee kutoa elimu ya lishe kwa jamii kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa, hii itasaidia kupunguza na kuondoa kabisa udumavu,” amesema Swalala.

Kikao hicho kimehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya viongozi, jamii na wadau wa maendeleo katika kupunguza utoro na kuinua kiwango cha ufaulu.