KONA YA MALOTO: Karata za urais 2030 CCM, zinachezwa 2025

Mayowe na miluzi ni mingi kuzunguka uteuzi wa wagombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Taarifa za waliokatwa na waliopenya zinatawala mitandao ya kijamii.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, ameshatoa tamko kuwa hakuna ambaye ameshakatwa.

Zipo taarifa zinasambaa pia kuhusu waliotangazwa kukatwa, kisha kurejeshwa.

Habari yoyote inaweza kutolewa, kusimuliwa, kupotoshwa au kutengenezwa, jambo la msingi kutambua ni kwa nini Uchaguzi Mkuu 2025 ni muhimu. Ni makosa makubwa kama utatazamwa kama jukwaa la kupata wabunge na madiwani wapya.

Uchaguzi Mkuu 2025 ni muhimu kwa ajili ya kupata viongozi wa muhula mpya, lakini muhimu zaidi unajenga taswira ya mnyukano kuelekea Uchaguzi Mkuu 2030. Wanaotaka urais baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, wapo kazini kuchanga karata.

Kushinda urais ni mikakati. Yeyote ambaye anajipanga kugombea na kushinda urais kupitia CCM 2030, lazima awe na mipango ya mapema ya kuungwa mkono. Anaungwaje mkono bila maandalizi?

Mwanasiasa anayeutaka urais kupitia CCM Uchaguzi Mkuu 2030, kwanza atahakikisha anakuwapo bungeni, katika Bunge la 13 ambalo uhai ni kuanzia Novemba 2025. Uwepo wake bungeni utamwezesha kujenga ushawishi kwa wabunge wenzake ili kutanua kukubalika kwake.

Hii inafanya vita iwe kubwa. Mtu ambaye ana mipango ya urais, lazima atumie nguvu kubwa kushinda ubunge Uchaguzi Mkuu 2025. Wanaojitokeza kushindana naye kwenye ubunge, hawachukulii kama washindani wa kawaida, bali watu wanaojaribu kukwamisha ndoto zake za urais.

Mwenye mawazo ya kushindania urais hawi peke yake. Wapo wengine wana ndoto hiyo. Kila mtu angependa afanikiwe kushinda ubunge, halafu mpinzani wake wa urais Uchaguzi Mkuu 2030, aanguke kwenye jimbo lake.

Mbunge ni mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa. Kwa maana hiyo, ukiwa mbunge, ni fursa ya kuwa karibu na wapigakura muhimu, ngazi ya uteuzi wa mwisho kumpata mgombea urais kupitia CCM.

Ukiwa mbunge, unakuwa na mtaji mkubwa wa kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM. Mbunge mwenye dhamira ya kushinda urais Uchaguzi Mkuu 2030, akiweza kushawishi wabunge 100 kugombea ujumbe wa NEC, hapo anakuwa ametengeneza kura kiasi gani?

Nafasi ya ubunge ni nyeti na mbunge mwenye malengo ya kugombea na kushinda urais kupitia CCM, akiwa na maarifa pamoja na nguvu ya ushawishi, ataweza kutengeneza uungwaji mkono ndani ya Kamati Kuu ya CCM. Na mikutano mitatu; Kamati Kuu, NEC na Mkutano Mkuu, ndiyo huchakata hadi kumpata mgombea urais.

Ukishatambua hilo, wewe elewa kwamba kwa sasa rafu zinachezwa jimbo kwa jimbo. Wapo wanaotumia nguvu kubwa kwenye majimbo mengine kuliko yale ambayo wanagombea. Ni kwa sababu wanachanga karata zao kwa ajili ya urais baada ya Rais Samia kuondoka madarakani.

Yupo kiongozi alikuwa ameshatangaza kuwania ubunge kwa muhula mwingine. Hata hivyo, kwa kuonekana angekuwa kikwazo kwa wengine wakati wa kinyang’anyiro cha urais 2030, alipigwa fitina, hadi akaamua yeye mwenyewe atangaze kuachana na dhamira yake ya kurejea bungeni. Ni mapambano ya urais.

Hiki ni kipindi ambacho, wanaopiga hesabu za kushinda urais 2030 na ambao tayari wameshajiweka sawa kifedha, wanazimwaga kwenye majimbo wanayogombea na wanawekeza kwa wabunge wengine watarajiwa, kwa imani kuwa wataweza kujenga ngome thabiti katika mapambano ya kuitwaa Ikulu baada ya Uchaguzi Mkuu 2030.

Kipindi hiki Kamati Kuu ya CCM inakwenda kupitia majina ya watiania wa ubunge kwa ajili ya uteuzi, ni vema kutambua jinsi ambavyo Uchaguzi Mkuu 2025 ulivyo muhimu.

Ni uchaguzi ambao unaweza kujenga makundi ndani ya CCM na siasa za ushindani bungeni, ndani ya kambi ya wabunge wa chama hicho (CCM caucus), wenyewe kwa wenyewe!

Anayewaza urais na ikiwa shabaha yake itakuwa Uchaguzi Mkuu 2030, lazima atajikita Uchaguzi Mkuu 2025 halafu baada ya hapo, jeshi lake atalielekeza Uchaguzi Mkuu CCM 2027. Huwezi kuwa unataka urais kupitia CCM, kama huchezi mizungu kwenye Uchaguzi Mkuu wa chama.

Atakayecheza karata zake vizuri kwenye Uchaguzi Mkuu CCM 2027, ndiye atakayekuwa na nguvu kubwa ndani ya vikao vyote vikubwa vya uamuzi. Ataweza kuingiza Nec wajumbe wanaomuunga mkono, vivyo hivyo Kamati Kuu na Mkutano Mkuu.

Kamati Kuu CCM inavyoendelea kuchakata majina ya watiania ya ubunge, watambue kuwa wapo ambao ubunge kwao ni njia ya kufanikisha ndoto kubwa wanazoota mbele ya safari.

Watu wa aina hiyo, muhula mzima ujao wa uongozi watautumia kufanikisha malengo yao hayo, kuliko kuwatumikia wananchi ambao watakuwa wamechaguliwa kuwawakilisha.

Huu ni Uchaguzi Mkuu wa kimkakati kwa kila anayeota urais. Kuna wanaokula viapo kwamba wakishinda ubunge, utakuwa muhula wao wa mwisho bungeni. Ni kwa sababu wanakwenda kwenye mapambano ya kuusaka urais, iwe kwa kufa au kupona. Ni vita.

Tahadhari inapaswa kuwa kubwa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, vilevile Uchaguzi Mkuu CCM 2027. Ni vipindi ambavyo CCM wanaweza kuyumba kwa kiasi kikubwa.

Maana makundi yatakuwa yameshazalishwa, kuna watu wataibuka na kupewa utii kuliko mamlaka za chama. Wataheshimiwa waongoza makundi, ambao ni marais watarajiwa.

Afya au udhaifu wa CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu 2030, itategemea jinsi ambavyo chama hicho kitavuka hatua hizo mbili za kiuchaguzi. Wakiimarisha misingi ya chama kuwa kikubwa kuliko mapembe ya wasaka urais, watafanikiwa, vinginevyo, kuna watu watakuwa na nguvu kuliko mamlaka na itaonekana kuwaadhibu ni kuua chama.

Related Posts