Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amewalalamikia askari Magereza namna wanavyomdhibiti kwa kumnyima fursa ya kuwasiliana na mawakili wake na kumzuia kupewa hata nyaraka.
Lissu ameibua malalamiko hayo dhidi ya maofisa hao wa magereza, leo Jumatano, Julai 16, 2025, wakati wa usikilizwaji wa shauri lake la maombi ya mapitio alilolifungua Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Dar es Salaam.
Malalamiko hayo yameibua mgongano wa hoja za kisheria baina yake na mawakili wa Serikali kwa niaba ya mjibu maombi katika shauri hilo (Jamhuri).

Hata hivyo, mawakili wa Serikali wamepinga madai yake huku wakiwatetea maofisa wa magereza kuwa wako sahihi kumdhibiti wakidai wanafanya hivyo kwa ajili ya usalama na kwa mujibu wa sheria.
Lissu anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa YouTube, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, Kisutu, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Juni 9, 2025 Mahakama hiyo iliamuru kulindwa kwa baadhi ya mashahidi katika kesi hiyo, kwa kutokuwekwa wazi utambulisho wao wakati wa kutoa ushahidi wao, kufuatia maombi yaliyofunguliwa na Jamhuri.
Lissu hakuridhika na uamuzi huo, hivyo Juni 25, 2025, alifungua shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama.
Katika shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Elizabeth Mkwizu, Lissu anaiomba Mahakama hiyo iitishe jalada la kesi hiyo kuchunguza mwenendo na uamuzi huo kujiridhisha na uhalali na usahihi wake na hatimaye iutengue, ombi ambalo limesikilizwa leo.
Kabla ya kuanza usikilizwaji wa shauri hilo, kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Mpale Mpoki ameieleza Mahakama kuwa wanapata shida kuwasiliana na mteja wao kwa sababu wanazuiwa kuonana naye mahakamani hapo.
Lissu katika maelezo na malalamiko yake ameeleza kuwa tatizo hilo si la leo tu katika Mahakama hiyo, bali lilianza tangu Ijumaa (Julai 11, 2025) alipofika mahakamani hapo kusikiliza uamuzi wa shauri lake lingine alikuwa amelifungua ambalo pia lilisikilizwa na kuamuliwa na Jaji Mkwizu.
Amesema kuwa siku hiyo alifikishwa mahakamani hapo asubuhi kabla Mahakama haijafunguliwa, akapelekwa mahabusu ambako alikaa mpaka shauri lilipoitwa saa sita mchana.
Lissu amesema kuwa muda wote huo aliwaomba maaskari wamuitie wakili washauriane (kuhusu mwenendo wa shauri hilo) kwa sababu alikuwa hajakutana nao kabla ya kesi, lakini walimkatalia.
Amesema kuwa alipoingia mahakamani alimuuliza mmoja wa mawakili wake, Dk Rugemeleza Nshala akamjibu kuwa askari walimkatalia kuonana naye.
Lissu amesema baada ya uamuzi ule kusomwa, mawakili wake walitaka kuzungumza naye na kumpa nyaraka zake kwani alikuwa amewapa wamfanyie utafiti kwa ajili ya kesi nyingine aliyo nayo.
“Wakili Nkungu (Nashon) aliponiletea maaskari Magereza wakazinyakua kwa nguvu wakazipeleka nisikokujua na nilipozidai wakadai siruhusiwi,” amesema Lissu na kuongeza:
“Kwa hiyo hata kubadilishana nyaraka na mawakili wangu mpaka nipate ruhusu ya Magereza.”
Amesema kuwa leo Wakili Paul Kisabo amempelekea nyaraka za kesi zinazohusiana na shauri hilo, lakini amezuiliwa kumkabidh, hivyo Magereza ndio wanaamua kwenye chumba cha Mahakama Kuu.
“Hii si Mahakama ya kijeshi ni ya kiraia, lakini inavyoelekea hata kwa kuangalia tu hii Mahakama inageuzwa kuwa ya kijeshi,” ameeleza Lissu na kueleza kwa mujibu wa sheria mawasiliano ya mawakili na mteja wake ni haki kamili ambayo haiwezi kuamuliwa na askari magereza.
Lissu amesema kuwa leo ni siku ya 98 akiwa mahabusu na amekuwa akisumbuana na askari hao kuhusu haki hiyo ya uhuru wa mawasiliano na mawakili wake.

Hivyo, amerejea Sheria ya Magereza juu ya mawasiliano ya wakili na mteja wake pamoja na Kanuni za Magereza za Mwaka 1987.
Amesema kuwa kanuni ya 13 inatoa haki kwa mfungwa kuwasiliana na kutembelewa na wakili wake kwa ajili ya mashauriano.
Lissu amesema hayo yanayotokea mahakamani hapo si tu ukiukwaji wa sheria za nchi na za kimataifa, bali pia ni dharau kwa Mahakama kwa sababu yanatokea hapohapo.
“Kwa hiyo naomba mheshimiwa Jaji utuambie pengine wewe ukisema watakuelewa, wana haki ya kushika nyaraka zangu au kuna haki ya mawasiliano mimi na mawakili wangu au la au mpaka ipitie kwa Magereza?” amehoji Lissu na kusisitiza:
“Naiomba Mahakama yako tukufu isije ikaruhusu kugeuzwa kuwa mahakama ya kijeshi namna hii. Kwa hiyo naomba utoe uamuzi uthibitishe kwamba kwa sheria za nchi hii mawasiliano yangu na mawakili wangu hayatakiwi kuingiliwa na hawa mabwana jela.”
Akijibu madai hayo kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Nassoro Katuga ameyapinga huku akiunga mkono na kuwatetea askari magereza kuwa wako sahihi kwa wanayoyafanya, kwani ni kwa mujibu wa sheria.
Wakili Katuga amesema kuwa Magereza ni taasisi iliyokasimiwa mamlaka ya kuwahifadhi wafungwa na mahabusu, na kwamba pia kuna sheria na taratibu katika kuwahifadhi.
Amesema kuwa Sheria ya Magereza kifungu cha 77 (1) kinatoa ruhusa ya kununua au kupokea kutoka sehemu binafsi chakula na vitu vingine muhimu, lakini kwa kuzingatia masharti mengine ambayo Kamishna wa Magereza anaweza kuelekeza, kwa ajili ya ulinzi wa mtu huyo au gereza kwa ujumla.
Ameongeza kuwa kifungu cha 85 (1) (a-c) kinatengeneza kosa kwa mtu atayeingiza nyaraka yoyote, na (d) kinasema hata kuwasiliana bila utaratibu atakuwa ametenda kosa.
Vilevile Wakili Katuga amedai kuwa kifungu kidogo cha (2) kinaeleza kuwa hata ofisa wa Magereza ambaye ataruhusu nyaraka, barua atakuwa ametenda kosa.
“Hivi ni vifungu ambavyo viko kwenye sheria. Sasa sijajua hawa wenzetu wanataka hawa maofisa watende kosa kwa madhumuni yapi? Sijajua haya yanayotendeka hapa yanakuwa ni kwa mujibu wa sheria?” amehoji Wakili Katuga.
Wakili Katuga amesisitiza kuwa hayo yote yanafanywa kwa ajili ya usalama wa mfungwa mwenyewe au Magereza maana hata hiyo nyaraka inaweza kuwa hatari kwa usalama.
Kuhusu kanuni ya 13 aliyoisoma Lissu, amesema inampa haki ya kutembelewa na wakili gerezani na katika mazungumzo yao ofisa Magereza hatakiwi kuyasikiliza, lakini wanapaswa kuwa mahali ambako anawaona.
Hivyo amesema kanuni hiyo haizungumzii kuwasiliana na wakili mahakamani.
“Mheshimiwa Jaji, hii ndio tafsiri ya kifungu hiki, lakini sasa hata hapa (mahakamani) umeona kesi inaendelea lakini wakili anataka ampe karatasi na utaratibu wanapaswa waombe uwaruhusu. Kwa hiyo hawa watu (askari magereza) walinda vibarua vyao.”
Wakili Katuga amesisitiza kuwa wakiruhusu hizo nyaraka bila kuzingatia utaratibu zinaweza kuwa na madhara huku akisisitiza kuwa vitu hivyo vinapaswa kwanza kukaguliwa.
“Sasa wakati mwingine askari anataka akague lakini wanakataa, kwa hiyo sisi tunaona kwamba Magereza hawajakosea.”
Akijibu hoja hizo za mjibu maombi, Lissu amesema katika madai yake ni haki ya mawasiliano ya wakili na mteja wake aliye mahakamani au aliyepelekwa gerezani, mahabusu na si chakula, mavazi wala malazi.
Lissu amesema kuwa kifungu cha 77 cha Sheria ya Magereza kilichorejewa na Wakili Katuga kinahusu chakula, malazi na mavazi ya mahabusu na mambo mengine muhimu, kuwa ndio vinavyozuiliwa.
Kuhusu masharti ya kifungu cha 85 cha sheria hiyo amesema kuwa kinazungumzia adhabu kwa kuingiza vitu vya magendo vilivyokatazwa Magereza kwa watu wa nje na kwa mabwana jela wenyewe.

Amesisitiza kuwa katika Sheria ya Magereza hakuna mahali inapozungumzia uhusiano wa mwanasheria na mteja wake isipokuwa wa Waziri mwenye dhamana na Magereza chini ya kifungu cha 105 cha Sheria hiyo ana mamlaka ya kutengeneza kanuni na kwamba ndio ametengeneza kanuni hiyo ya 13.
“Sheria iko wazi lakini kuna watu wanafikiri kwa sababu ni maofisa Magereza wanadhani kuwa wako juu ya sheria,” amesema Lissu akihitimisha hoja zake za ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa na Jamhuri.
Jaji Mkwizu baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameruhusu kuendelea na usikilizwaji wa hoja za msingi za shauri hilo, huku akielekeza kuwa uamuzi wa malalamiko hayo ya Lissu utatolewa pamoja na uamuzi wa hoja za shauri lake la maombi ya mapitio.
Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu, anadaiwa kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutenguliwa kwa wagombea chama chake katika maeneo mbalimbali wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, 2024.
Pia, anadaiwa kuwatuhumu askari Polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.
Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.