Mahakama yatupa maombi kupinga kanuni za maadili uchaguzi mkuu 2025

Dodoma. Mahakama Kuu ya Tanzania imetupilia mbali maombi ya Watanzania wawili, Kumbusho Kagine na Bubelwa Kaiza, waliokuwa wakiomba kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kupinga Kanuni za Maadili ya Uchaguzi Mkuu 2025.

Walifungua maombi namba 12670 ya mwaka 2025 dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakiomba waruhusiwe kufungua maombi kupinga matumizi ya kanuni hizo.

Kanuni hizo zimesainiwa na vyama 18 vya siasa nchini, isipokuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kinashinikiza mabadiliko ya mifumo na sheria ya uchaguzi, zikiwamo kanuni hizo.

Uamuzi huo ulitolewa Julai 11, 2025 na Jaji Abdi Kagomba wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma na kupatikana mtandaoni Julai 15, 2025.

Jaji Kagomba ameeleza kuwa kifungu namba 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, ambacho ndicho kilichotumika kutengeneza kanuni hizo, kinaonyesha kuwa waombaji si wadau wa kanuni hizo.

Kifungu kidogo (1) kinasema: “Kwa madhumuni ya kusimamia uchaguzi wa haki, huru na amani, na baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, tume itaandaa na kuchapisha katika gazeti la Serikali, kanuni hizo za maadili.”

Kanuni hizo ndizo zitakazoanisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na INEC wakati wa kampeni za uchaguzi, uchaguzi wenyewe, pamoja na utaratibu na utekelezaji wake.

Kifungu kidogo (2) kinasema kanuni za maadili ya uchaguzi zitasimamiwa na kila chama cha siasa, kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi, Serikali na tume, na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini kanuni hizo.

Jaji amesema kanuni hizo zinaeleza madhumuni ya kusimamia maadili na nani watashirikishwa kabla hazijatangazwa; na imetaja pia ni nani watazisaini, ambao ni vyama, INEC, Serikali na wagombea.

“Inaonekana wazi kwangu kwamba hii ni sheria maalumu kwa kundi maalumu la wadau, kama vile ambavyo uamuzi wa mahakama huwa unawabana pande zile tu ambazo zilihusika na shauri hilo,” amesema.

“Swali linaweza kuwa, ni kwa vipi kifungu 162 kinahusiana na masilahi ya kutosha ya waleta maombi katika shauri hili. Kama alivyoeleza Wakili wa Serikali, ni lazima muombaji aoneshe masilahi katika mapitio hayo ya mahakama anayoyaomba,” amesema na kuongeza:

“Sioni sababu zenye mashiko za kuishawishi mahakama hii ni kwa vipi (waombaji) ni washirika. Mtu anaweza kujiuliza, wako wapi wadau waliochukizwa ambao, bila kuwa na mashaka, mahakama inaweza kuwatambua.”

Amesema: “Bila wao kuwepo mbele ya mahakama hii, hiki kilichosemwa na waombaji katika sababu ya 6.1, 6.2, 6.3, 6.4 na 6.5 ya maelezo yao kinakuwa batili, kutokana na ukweli kuwa wao ni majirani tu na si wenye haki ya kushtaki.”

“Hata katika sababu ile ya 7.0 kwamba waombaji wana masilahi na uchaguzi wa huru na haki, inaweza tu kuonekana kama masilahi ya mbali na si masilahi ya kutosha katika masuala yaliyoibuliwa na waombaji,” amesema.

“Ni kutokana na sababu hizo, na ukweli kuwa kuna tofauti ya majina kama yanavyoonyeshwa kwenye kiapo chao na yale yanayoonekana katika vitambulisho vya kupigia kura, na hakuna kiapo kinachoonyesha kuwa majina hayo hutumika kwa pamoja, ninaona kabisa wameshindwa kuishawishi mahakama juu ya masilahi yao,” amesema na kuongeza:

“Hivyo, kutokana na uchambuzi huo, maombi ya kuzuia matumizi ya kanuni hizo yanakosa miguu ya kusimamia, na kwa sababu kanuni hizo ni kwa ajili ya wadau mahususi na waombaji hawamo, basi maombi yao yanatupiliwa mbali.”

Wakiomba kupatiwa kibali cha kufungua maombi ya kupinga kanuni hizo, waombaji walieleza kuwa Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 zilichapwa katika gazeti la Serikali la Aprili 18, 2025.

Wanazipinga wakidai zinakiuka utaratibu kwa kiasi kikubwa, hazina maana wala mantiki, zina makosa ya sheria kwenye kumbukumbu, na zinakiuka sheria na kanuni nyinginezo, pamoja na kutangazwa bila mashauriano.

Kupitia maombi hayo, kama wangepatiwa kibali, wangefungua maombi kuiomba mahakama izifute kanuni hizo na kumzuia mjibu maombi wa kwanza (INEC) kuendelea na mchakato wa uchaguzi kwa kutumia kanuni hizo.

Katika ombi la nyongeza kupitia kanuni ya 5(6) za mapitio ya mahakama kama ilivyotangazwa katika GN namba 324 ya 2014, waliomba kwamba kama maombi yao yatakubaliwa, basi kanuni hizo zisitumike hadi ombi lao lisikilizwe na kuamuliwa.

Wajibu maombi waliwasilisha kiapo kinzani kilichoapwa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa INEC, ambacho kilijibiwa na waombaji.

Katika usikilizwaji wa maombi, waombaji waliwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Jebra Kambole, huku wajibu maombi wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo, akisaidiana na mawakili Erigh Rumisha na Edwin Webiro.

Hoja za wanaopinga kanuni

Kambole aliieleza mahakama kuwa wateja wake si tu wamewasilisha ombi hilo ndani ya muda wa miezi sita unaotakiwa na sheria, bali wana kesi yenye mashiko ambayo wana masilahi nayo.

Alisema waombaji wana masilahi ya kutosha katika maombi hayo kwa sababu wanaamini kuwa, kama wapigakura walioandikishwa wanaotarajia kupiga kura, wataathiriwa na kanuni hizo.

Ili kuishawishi mahakama kuwa wana masilahi makubwa na maombi hayo, walijenga hoja sita zifuatazo:

Moja, maneno “washiriki wa uchaguzi” yaliyotumika katika utangulizi wa kanuni yanaulenga umma.

Pili, waombaji ni raia wa Tanzania wenye haki ya kupiga kura na kuchaguliwa.

Tatu, wao ni wapigakura walioandikishwa, hivyo wana haki ya kupiga kura na kuchaguliwa, na wana mpango wa kugombea.

Nne, wana masilahi na uchaguzi wa huru na haki katika nchi ya Tanzania.

Tano, wana masilahi kama wapigakura na haki ya kumchagua mgombea wanayemtaka katika uchaguzi huo.

Sita, kanuni hizo zinaweka msingi wa haki na wajibu kwa wagombea, wanachama wa vyama vya siasa na wafuasi wao, hivyo wajibu huo ni jukumu la kila raia kwa mujibu wa Ibara ya 26(1) ya Katiba ya Tanzania.

Wakili Mpoki aliiomba mahakama kupitia kanuni ya 5(6) ya GN namba 324 ya 2014 kwamba, mara tu mahakama itakapotoa kibali hicho, basi itumike kama zuio la matumizi ya kanuni hizo hadi shauri hilo litakapoamuliwa.

Alisema amri hiyo itasaidia kulinda maombi hayo yasiwe mabaya, kulinda masilahi ya waombaji ambayo hasara yake haiwezi kushughulikiwa, na kuwapa amani ya moyo waombaji wakati maombi yao yanashughulikiwa na mahakama.

Mpoki alisema lengo la waombaji si kusimamisha mchakato wa uchaguzi bali kuiwezesha mahakama kuangalia misingi ya kisheria ya kanuni hizo zitakazosimamia maadili, kwani kama wakishinda hawatafidiwa.

Wakili Rumisha alipinga hoja kuwa waombaji wameonyesha masilahi waliyonayo katika maombi hayo kwa sababu ni kigezo muhimu cha kuzingatiwa kabla ya mahakama kutoa kibali cha kufungua maombi hayo.

Alitoa hoja nne zifuatazo: Mosi, waombaji si wadau wa kanuni hizo, akifafanua kuwa wadau wa kanuni hizo ni Serikali, wagombea, vyama vya siasa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Pili, waombaji walieleza katika aya ya sita ya majibu ya kiapo kinzani kuwa wao si wadau wa kanuni hizo kwa kuwa wao ni wageni wa kanuni hizo, hivyo hawawezi kusema wana masilahi ya kutosha na kanuni za maadili ya uchaguzi.

Tatu, kuna tofauti ya majina ya waombaji: Kumbusho Kagine na Bubelwa Kaiza, na Kumbusho D. Kagine na Bubelwa E. Kaiza, yanayoonekana katika kadi za mpigakura.

Kwa kuwa ni watu tofauti na hakuna kiapo kinachoonyesha kuwa majina hayo hutumika kwa pamoja, hoja kwamba wameonyesha masilahi ya kutosha kama wapigakura walioandikishwa inakosa miguu ya kusimamia.

Nne, alipinga hoja ya waombaji kuwa wanatarajia kuwa wagombea wa nafasi mbalimbali kabla ya kufungwa kwa dirisha la uteuzi, akisema hiyo ni dhana tu na haipo katika kiapo cha waombaji.

Rumisha alisema kwa waombaji kuomba kusimamisha matumizi ya kanuni hizo, wanamaanisha kusiwepo kabisa na miiko ya maadili ya kusimamia uchaguzi mkuu, jambo ambalo litafanya wadau waendeshe mambo hewani.

Aliiomba mahakama itupilie mbali maombi ya waombaji kupewa kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kupinga kanuni hizo za maadili ya uchaguzi.

Awali, kabla ya kusikiliza maombi hayo, INEC na AG waliwasilisha pingamizi wakidai kuwa hati ya kiapo cha waleta maombi cha kuunga mkono ombi lao ilikuwa na dosari isiyoweza kutibika kwa kuwa na maoni, hoja na hitimisho kinyume cha sheria.

Baada ya mawasilisho ya hoja za mawakili wa pande zote mbili, jaji alilikataa pingamizi hilo.

Uamuzi huo uliwezesha kusikilizwa kwa maombi hayo ambayo yametupwa na mahakama kwa kukosa mashiko.

Related Posts