Mange, Aslay waburuzwa kortini wadaiwa fidia Sh5 bilioni

Dar es Salaam. Mwanaharakati maarufu katika mitandao ya kijamii aishiye Marekani, Mange Kimambi na nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini Isihaka Nassoro maarufu Aslay, wamefunguliwa kesi ya madai kortini, wakidaiwa fidia ya Sh5 bilioni.

Aslay pia anajulikana ka majina ya Dogo Aslay au Dingi Mtoto. Mange ni maarufu kwenye mitandao ya Instagram, X (zamani Twitter) na Mange Kimambi App inayopatikana Playstore.

Katika hati ya madai, Mange anatajwa kuwa mkazi wa Los Angeles, California nchini Marekani na Mbezi Beach, mkoani Dar es Salaam. Wito wa kuitwa kwake kortini unaweza pia kutangazwa kupitia vyombo vya habari.

Kesi hiyo ya madai namba 44359 ya mwaka 2025 iliyotajwa kwa mara ya kwanza Julai 15, 2025 mbele ya Jaji Awamu Mbagwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imefunguliwa na DJ maarufu nchini Tanzania, Hancy Mushy.

Mushy ni DJ wa kimataifa mwenye followers zaidi ya 23,000 katika mtandao wa Instagram, ambaye katika kesi hiyo ni mdai wa kwanza.

Mdai wa pili ambaye ni mfanyabiashara na mjasiriamali jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili na kisheria.

Nje ya mahakama baada ya kesi kutajwa mbele ya Jaji Mbagwa, wakili Daniel Kalasha anayewawakilisha wadai, alisema jaji amewaamuru Mange na mwenzake, kuwasilisha majibu ya madai ndani ya siku 21. Kesi imepangwa kutajwa Agosti 6, 2025.

Katika hati ya madai, walalamikaji wanadai Februari 13, 2024, Mange akiwa na nia ovu alishapicha taarifa kupitia akaunti yake ya Instagram na Mange Kimambi App, ambazo si sahihi na kuwavunjia heshima na utu wao.

Wanadai katika chapisho hilo la kashfa, Mange alidai DJ Mushy alikuwa akijihusisha na mapenzi kinyume cha maumbile na kuambatanisha sauti (audio clip), huku akifahamu taarifa hiyo ilikuwa ya uongo.

Wanadai chapisho hilo la kashfa kiini chake ni maudhui ya uongo yaliyotengenezwa na kuchapishwa kwa mara ya kwanza na mdaiwa wa kwanza (Mange) Februari 2, 2024 na kusambazwa kwa watumiaji milioni saba wanaotumia mitandao ya Mange.

“Machapisho na vyombo vya habari vinavyohusiana hayakuwa ya uongo tu, bali yalifanywa makusudi ili kuharibu jina la mlalamikaji wa kwanza (DJ Mushy), taaluma yake, ustawi wa kiakili na heshima yake katika jamii,” inaeleza hati ya madai.

“Chapisho hili lilisambazwa upya kwa wingi katika majukwaa ya kidijitali ya Tanzania, yakiwamo makundi ya Whatsapp, kurasa za Facebook na Intagram na kusababisha kejeli na kuchafua sifa nzuri aliyonayo mdai wa kwanza,” inaeleza hati ya madai.

Kutokana na matendo hayo, mdai wa kwanza katika shauri hilo inadaiwa alipata matatizo ya kisaikolojia, huzuni ndani ya familia yake, kupoteza uaminifu kutoka kwa jamii, kuachwa na washirika wa biashara na kiwewe cha kihisia.

Mdai ameambatanisha vyeti vya matibabu kutoka hospitali na ripoti inayoonyesha kuvunjika mikataba ya kibiashara.

Mdai wa pili, ambaye ni mwanamke anayejiheshimu anadai kuanzia mwaka 2020 alikuwa na mahusiano na mdaiwa wa pili (Aslay), lakini kati ya Aprili 11 na 12, 2024 alikumbana na jambo lililochafua heshima na utu wake.

Anadai Mange akishirikiana na mdaiwa wa pili, kwa makusudi na bila uhalali wa kisheria alichapisha kipande cha video kilichorekodiwa kikimuhusisha mdai wa pili kupitia mtandao wa kijamii wa mdaiwa wa kwanza wa Mange Kimambi App.

Maudhui ya video hiyo anadai yalionwa na umma mzima na walikuwa na ufahamu kuwa chapisho hilo haliruhusiwi, halijaidhinishwa na lilikuwa na maudhui ya kashfa na kuingilia faragha ya mdai wa kwanza na kuharibu utu na heshima yake.

Kutokana na chapisho hilo, mdai wa pili anadai kupata matatizo ya kisaikolojia, msongo wa mawazo na akili kutokana na kusambazwa kwa maudhui ya video hiyo, hali iliyomfanya asitishe masomo yake ya kitaaluma.

Wakili Kalasha anayewawakilisha wadai katika shauri hilo, anaeleza katika hati ya madai kuwa Mange Kimambi alieneza taarifa na machapisho ya uongo kuwa wadai walikuwa wakijihusisha na mwenendo mbaya na usio wa asili.

Kwamba machapisho hayo yalisambazwa katika mitandao ya kidijitali yenye wafuasi wengi, yalikusudiwa kuwafanya wadai kudharauliwa, kuchukiwa na kukejeliwa hadharani na yalichapishwa bila ufahamu wala idhini ya mdai wa pili.

Machapisho hayo kwa mujibu wa hati ya madai, yalisambazwa bila upande wa pili kuulizwa wala kuthibitisha na hayakuwa na uhalali wowote wa kisheria, hivyo kuwasababishia wadai madhara ya kiafya, fani, utu na maumivu ya kiakili.

Hivyo kwa pamoja, wadai wanaiomba mahakama iwaamuru wadaiwa kuwalipa Sh5 bilioni kama fidia ya madhara yaliyotokana na matendo ya mdaiwa wa kwanza (Mange) ambayo hayakuwa na uhalali wowote wa kisheria.

Wanadai mwenendo wa wadaiwa wa kuchapisha machapisho ya uongo yaliyorekodiwa na kusambaza taarifa za uongo na zilizowaumiza, ni kwamba waliwachafua kwa umma ili kuharibu heshima yao.

Hivyo, wanaiomba mahakama itamke kuwa machapisho yaliyofanywa na mdaiwa wa kwanza na wa pili yalikuwa ya uongo, ya kashfa na yalikiuka haki ya wadai kuhusu utu na faragha yao, hivyo wanastahili kuwalipa kiwango hicho cha fedha.

Related Posts