Mashahidi wa Jamhuri kesi ya Lissu wadaiwa kutishiwa

‎Dar es Salaam. Mashahidi wa Jamhuri katika kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ya kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni, wasio askari Polisi wamedai kutishiwa ili wasitoe ushahidi kwenye kesi hiyo.

Madai ya mashahidi hao kutishiwa, ambayo ndio sababu ya Mahakama kutoa amri ya kuwalinda yamebainishwa hadharani mahakamani leo Jumatano Juni Julai 16, 2025, wakati wa usikilizwaji wa shauri la Lissu kupinga uamuzi huo.

‎Lissu anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mtandao wa Youtube, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, Kisutu, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini

‎Juni 9, 2025 Mahakama hiyo iliiamuru kulindwa kwa baadhi ya mashahidi katika kesi hiyo, kwa kutokuwekwa wazi utambulisho wao wakati wa kutoa ushahidi wao, kufuatia maombi yaliyofunguliwa na Jamhuri, ambayo yalisikilizwa na kuamuliwa upande mmoja.

Licha ya uamuzi huo wa kuwalinda mashahidi hao kuelezwa wazi mahakamani na upande wa mashtaka kwenye mwenendo wa kesi ya msingi, lakini sababu za maombi hayo ya Jamhuri na hatimaye uamuzi huo hazikuwahi kubainika.

Hata hivyo, kutokana uamuzi huo, Lissu hakuridhika nao, hivyo Juni 25, 2025,  alifungua Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, shauri la maombi ya  mapitio ya Mahakama dhidi ya uamuzi huo.

‎Katika shauri hilo lililosikilizwa na Jaji Elizabeth Mkwizu, Lissu anaiomba mahakama hiyo iitishe jalada la kesi hiyo kuchunguza mwenendo na uamuzi huo kujiridhisha na uhalali na usahihi wake na hatimaye iutengue.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo ndipo sababu za Jamhuri kuomba ulinzi kwa mashahidi hao na hatimaye uamuzi huo wa Mahakama zikawekwa wazi kwa umma, kuwa walidai kutishiwa.

Hata hivyo, mawakili wa Lissu wamepinga uamuzi huo wakidai hapakuwa na sababu za msingi zilizotolewa, kwa madai mashahidi hao waliodai kutishiwa hakuna viapo vyao walivyoviwasilisha mahakamani kama ushahidi wa madai hayo.

Wakili wa Lissu, Dk Rugemeleza Nshala amesema Jamhuri katika maombi hayo ya ulinzi wa mashahidi, zilielezwa katika kiapo cha Wakili wa Serikali, Tawabu Issa na Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam, Fsustine Mafwele.

Dk Nshala amesema katika kiapo hicho cha Wakili Tawabu kilieleza baadhi ya mashahidi ambao si askari Polisi wako katika hatari kutoka kwa wafuasi wanaomuunga mkono mwombaji/mshtakiwa kwa kuwatisha ili wasitoe ushahidi.

Amesema viapo vya hao mashahidi ambao walidai walitishiwa vilipaswa viwepo ili Hakimu aweze kutoa uamuzi wa haki, lakini hilo halikufanyika.

‎Hivyo Hakimu amesema Hakimu Mhina alifanya kosa linalogusa hata uaminifu wa mahakama kwani hakutegemewa kutoa uamuzi kama huo.

Wakili Jebra ‎Kambole katika hoja zake amesema katika uamuzi ule hakimu hakufanya uchambuzi wa kiwango cha upande wa mashtaka kuthibitisha madai yao kwa kiwango kinachotakiwa ambacho bila kuacha mashaka.

‎Amesema kama hakimu angefanya uchambuzi sawasawa angebaini hakukuwa na haja ya kutoa uamuzi huo kulingana na mashtaka yaliyoibuliwa katika hoja za Wakili Nshala.

‎Amesisitiza uamuzi ule wa upande mmoja ulihitaji uthibitisho kwani uliathiri haki za mshtakiwa za usikilizwaji sawa, kwani Mahakama haipati fursa ya kumtathimini shahidi kuaminika kwake wakati akitoa ushahidi kizimbani wala mshtakiwa kupata fursa ya kumkabili ana kwa ana.

‎Amesema mashtaka yanayomkabili mwombaji yanasikilizwa na Mahakama ya chini ambako mshtakiwa huwa hapewi nyaraka (maelezo yoyote) hivyo kama shahidi hatafahamika haki ya mshtakiwa kusikilizwa inaathirika.

Vilevile amedai ‎hakuna maelezo kutoka kwa ofisa wa Polisi kuwa hawakuweza kuwalinda mashahidi, hivyo mahakama hii haipaswi kuruhusu Polisi kujiondoa katika wajibu wao wa msingi kuwalinda watu kwa gharama za mwombaji na kwa gharama ya usikilizwaji kwa usawa.

“‎Kuwatishia mashahidi ni kosa la jinai hivyo upande wa mashtaka walipaswa kutimiza wajibu wao na si kwa gharama ya mwombaji kwa wao kutokutimiza wajibu wao,” amesema Wakili Kambole.

Kwa upande wake, Wakili Jeremiah ‎Mtobesya amesema sababu zilizotolewa haziwezi kuondoa umuhimu wa Mahakama kuangalia mwenendo wa nje wa shahidi wakati akitoa ushahidi kizimbani (demeanor).

Akijibu hoja hizo, Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Kuu, Nassoro  Katuga ameomba Mahakama itupilie mbali maombi ya Lissu na kueleza wanaomba mahakaka hiyo ijiridhishe na kile kilichowasilishwa na waleta maombi.

‎”Mheshimiwa jaji, tumesikiliza mawasilisho yao na upande wa Jamhuri tumejiuliza kifungu 372 kuwa sehemu iliyotumika kuipa mahakama hiyo mamlaka yako kutoa uamuzi,” amedai Katuga.

‎Katuga amedai uamuzi wa Mahakama ya Kisutu ambao inalalamikiwa, ulitolewa kwa mujibu wa sheria na kwamba Mahakama ilijikita katika ushahidi wa viapo viwili vilivyotolewa Wakili wa Serikali ZCO, Mafwele.

‎Katika kiapo cha Mafwele, kilieleza amepokea taarifa fiche kuwa kuna mashahidi ambao sio polisi kuwa wamekuwa wakipokea vitisho vya kutoa ushahidi katika kesi hizo.

‎Alidai kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023 ni kosa kisheria kumtishia shahidi.

‎Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema pamoja na mambo mengine ameiomba Mahakama hiyo ikapitie uamuzi uliotolewa na Mahakama ya chini ili kujiridhisha na malalamiko ya mwombaji kama yana mashiko, lakini anaiomba isiingie kwenye mtego.

‎”Tunaomba mahakama hii isiingie katika mtego wa kumchanganywa kwa kuletewa maombi ambayo ukienda kuyasoma ndani yake yanasura ya rufaa,” amedai.

Jaji Mkwizu baada ya kusikiliza hoja za pande zote amepanga kutoa uamuzi Agosti 12, 2025 mchana.

‎Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu. Katika mashtaka hayo Lissu anadaiwa kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania na kutenguliwa kwa wagombea chama chake katika maeneo mbalimbali wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2024.

‎‎Pia anadaiwa kuwatuhumu askari Polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.

‎‎Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.