TIMU mbili za Jeshi, JKT Tanzania na Mashujaa zinamfuatilia kwa ukaribu kinda wa Yanga, Isack Mtengwa na kama mambo yakienda sawa huenda akaibukia kwenye timu mojawapo.
Msimu uliopita nyota huyo aliichezea Wakiso Giants ya Uganda kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Yanga U-20 akiungana na beki mwenzie Shaibu Mtita.
Mmoja wa watu wa karibu wa kinda huyo, alisema wanaangalia ofa gani nzuri, pia sehemu atakayocheza zaidi ili kupata uzoefu kwenye Ligi Kuu.
“Mazungumzo bado yanaendelea, kama mambo yatakuwa sawa basi anaweza kuibuka sehemu mojawapo, amecheza Uganda hivyo matakwa ya mchezaji angalau apate sehemu ya kuendeleza ubora wake mbali na ofa zitakazokuja ambazo sio kipaumbele sana,” alisema mtu huyo na kuongeza.
“Hata hivyo kwa JKT kocha Ahmad Ally anamuhitaji zaidi kwani amewasilisha ripoti ya kutaka damu changa kwenye eneo la pembeni hasa kulia na tayari wameanza kuwasiliana na viongozi.”
Beki huyo wa kulia aliyecheza timu za vijana za Simba na Yanga, msimu uliopita akiwa Wakiso alicheza mechi tisa za Ligi Kuu kwa dakika 494.