Matarajio ya wananchi dira inapokwenda kuzinduliwa

Dar es Salaam. Ilianza mipango, ikafuata mikakati, baadaye maandalizi hadi kukamilika na sasa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inazinduliwa, huku wananchi wakiitarajia kuwa msingi wa ukuaji uchumi, usawa wa jinsia na maendeleo jumuishi.

Dira hiyo inayojumuisha malengo na mipango ya 25 kuanza 2025/50 ya Tanzania, inatarajiwa kuzinduliwa kesho Alhamisi, Julai 17, 2025 na inakuja baada ya kukamilika ya awali, iliyoandaliwa na kuzinduliwa mwaka 2000 chini ya Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa.

Kwa Tanzania hii ni dira ya pili kuzinduliwa baada ya ile ya mwaka 2025 inayotarajiwa kumaliza muda wake Juni 31, mwakani. Kabla ya mwaka 2000, Tanzania haikuwa na dira ya muda mrefu ya maendeleo, bali ilitegemea mipango ya muda mfupi na wa kati.

Mipango ya miaka mitano ya maendeleo ilianza rasmi mwaka 1964 na ilijikita kuelekeza rasilimali na vipaumbele vya Taifa kwa kipindi cha nusu muongo.

Dira inayomaliza muda wake, ilijikita kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda, huku malengo yake yakiwa ni kujenga jamii ya watu walioelimika na wenye maarifa.

Lengo jingine ni kujenga uchumi imara unaoendeshwa na sekta binafsi, utawala bora, miundombinu madhubuti, jamii inayozingatia amani, umoja na mshikamano.

Julai 2020, Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa mataifa yaliyokuwa kiuchumi na kufikia uchumi wa kati kiwango cha chini, ikiwa ni kutimiza malengo ya dira hiyo kabla ya muda uliopangwa.

Sambamba na hilo, Tanzania imejenga zaidi ya kilomita 10,000 za barabara kwa kipindi hicho cha miaka 25, huku kilomita 4,000 pekee zikijengwa kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Yanayoihusu dira ya mwaka 2025 yanakaribia kuhitimisha enzi zake na kesho Julai 17, 2025 inazinduliwa dira mpya kwa ajili ya miaka 25 ijayo na wananchi wanatumaini itakuwa jumuishi, msingi wa kukua kwa uchumi na usawa wa jinsia.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben amesema ni kiu yake kuona dira itakayokuwa na ujumuishi wa maoni ya makundi mbalimbali ya wananchi.

“Kwa sababu maandalizi ya dira yamehusisha ukusanyaji maoni kutoka makundi mbalimbali ya wananchi, natarajia hata kilichomo ndani yake, kitakuwa kimejumuisha maoni hayo ili kuleta maana ya dira ya wote,” amesema.

Sambamba na hilo, amesema anatarajia kuona kilichomo ndani ya dira kinatekelezeka, ili kusadifu lengo la Tanzania tunayoitaka ambalo aghalabu limekuwa likihusishwa na dira hiyo.

“Wiki iliyopita tumeambiwa dira itatupeleka kwenye Tanzania tunayoitaka baada ya miaka 25, ili kuifikia hiyo Tanzania lazima iwe dira inayotekelezeka,” ameeleza Dk Rose.

Kwa sababu dira ni mipango na malengo ya miaka 25, amesisitiza ni vema yasiishie kuwa katika maandishi, badala yake kuwe na mkakati wa utekelezaji kuhakikisha kila kilichopangwa kinakuwa hai kwa vitendo.

Itabeba ajenda ya usawa wa jinsia

Mwanazuoni na mwanaharakati wa haki za wanawake, Profesa Ruth Meena amesema tayari anafahamu dira hiyo imebeba mambo mengi kuhusu usawa wa jinsia na haki za wanawake.

Kwa sababu ya uhalisia huo, amesema anatarajia mambo hayo yataingizwa kwenye mpango wa utekelezaji ndani ya malengo ya miaka mitano au 25 kwa ujumla.

“Natarajia malengo, misingi na matarajio ndani ya dira husika yafikiwe. Dira imebeba kwa ukubwa masuala ya usawa wa kijinsia na wanawake,” ameeleza.

Profesa Ruth amesema ni matarajio ya wadau wote wa haki na usawa wa jinsia, ndani ya dira kutakuwa na mipango thabiti ya utekelezaji wa masuala hayo kwa masilahi ya uchumi na maendeleo ya Taifa.

Itatufikisha uchumi wa juu

Kwa upande wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Profesa Burton Mwamila amesema hatua ya kuzinduliwa kwa dira hiyo ni muhimu kwa Taifa.

Ukiacha umuhimu wa uzinduzi, amesema anatarajia dira hiyo itakuwa msingi wa ustawi wa nchi, kutoka hatua iliyofikiwa sasa kwenda juu zaidi.

Profesa Mwamila amesema dira inayofikia mwisho, pamoja na mafanikio mengine, imelifikisha Taifa katika uchumi wa kati ngazi ya chini, hivyo inayozinduliwa itakuza zaidi uchumi.

“Nafurahia hatua tu ya uzinduzi ni kubwa kwa Taifa letu, tulikuwa na dira iliyotufikisha katika uchumi wa kati ngazi ya chini, naamini hii inayozunduliwa imeandaliwa vizuri kuhakikisha tunapaa zaidi,” amesema.

Mwanazuoni huyo amesema jambo muhimu ni Serikali ijipange vema kuhusu utekelezaji wake, huku kila anayepewa jukumu la kuwawakilisha wananchi katika kutimiza malengo ahakikishe anatimiza wajibu kama anavyopaswa.

Related Posts