Mikakati ya kuongeza kasi kupunguza vifo vya watoto wachanga yatajwa

Dodoma. Wadau wa masuala ya watoto wametaja mikakati itakayosaidia kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya watoto waliochini ya miaka mitano ikiwemo lishe, afya ya mama na mtoto kwa kuwajengea uwezo wahudumu wa afya.

Kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2025/26, vifo vya watoto wa umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 81 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2019/20 hadi kufkia vifo 43 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2022/23.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai 16, 2025, Msimamizi wa Sekta ya Afya na Lishe wa Shirika la Save the Children, Brenda Mshiu amesema katika kuhakikisha kasi ya kupunguza vifo inaongezeka, shirika hilo limeanza utekelezaji wa baadhi ya mikakati iliyoibuni.

Ametaja mikakati hiyo ni kuboresha ushiriki wa jamii katika kuhakikisha wanaibua wanawake wanaochelewa kwenda kliniki kabla na baada ya kujifungua na kutoa elimu ya afya kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii juu ya umuhimu gani wa kujifungulia vituoni.

Mingine ni kutoa elimu ya lishe ya wajawazito, wanaonyonyesha, watoto wachanga, vijana na vijana balehe, kushirikisha wadau mbalimbali wa asasi za kiraia katika kuhakikisha wanahamasisha upatikanaji wa huduma za afya na lishe pamoja na kushirikisha sekta mtambuka katika kupunguza udumavu nchini.

“Tunawawezesha wakinamama waliojifungua kwa mara ya kwanza katika umri wa miaka 15 hadi 24 kukabiliana na changamoto kuhusiana afya ya uzazi  na  inahusisha mfumo mzima wa afya kuhakikisha una utayari wa kutatua changamoto zinatokana na mila potofu ambazo zinasababisha kuathiri ubora wa huduma,”amesema.

Brenda ametaja mkakati mwingine ni kuwekeza kwenye ufuatiliaji wa utoaji huduma ili kuchechemua vituo vya afya kutenga raslimali kwa ajili ya kununua vifaa tiba na kuhamasisha unyonyeshaji unaofaa wa watoto wadogo.

Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (Wajiki), Janeth Mawinza amesema bado hakuna elimu ya kutosha ya afya ya uzazi kwa vijana wakike na wakiume.

Ameshauri kuanzishwa kwa mkakati wa kutoa elimu kwa vijana ili kuhakikisha wanafahamu vizuri afya ya uzazi, malezi na makuzi kabla kupata ujauzito.

Aidha, ametaka kuanzishwa kwa mfuko dhabiti wa kuwahudumia wajawazito na watoto wao na sio kuwadai wagharamikie matibabu yao.

 “Tunasema huduma ya mama na mtoto ipo bure, lakini ni ile ya maneno siyo huduma ya moja kwa moja wanapata. Ndio hao hao wakienda hospitali wanaulizwa una bima wakati huduma ya matibabu kwa mtoto chini ya miaka mitano ni bure,” amesema.

Mkazi wa Maili Mbili, Anna Musa amesema mkakati mwingine unaotakiwa kufanywa ni kuboresha miundombinu itakayomwezesha mama na mtoto kufika katika vituo vya kutolea huduma pindi anapovihitaji.

“Huko vijijini ni vigumu kufikia huduma za afya kutokana na barabara mbovu na sehemu nyingine hazipitiki wakati wa mvua hivyo zinasababisha wajawazito kujifungua njiani, hali ambayo inasababisha wakati mwingine kupoteza maisha wao na watoto wao,” amesema.

Julai 12, 2025 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, Mwenyekiti wa waganga hao, Dk Besta Magoma alitaka pia Sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa zijengewe uwezo na taasisi za utafiti kama vile Taaasi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwenye eneo hilo la kuokoa maisha ya watoto.

Pia, alitaka taasisi ya Ifakara ili zifanye tafiti za kubainia visababishi vya vifo vya watoto wachanga pamoja na uzazi kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira ya maeneo husika.